JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MIAKA 10 INATOSHA KWA YEYOTE KUTUMIKIA URAIS – RAIS KIKWETE

Share This
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Miaka 10 inatosha kwa yeyote kutumikia Urais – Rais Kikwete
·        Awataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye kwa ari na nguvu zaidi kuliko walivyomsaidia yeye.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa miaka 10 ya uongozi inatosha kabisa kwa mkuu wa nchi kufanya mambo mengi na kuwa hahitaji muda zaidi kuweza kumaliza ajenda yake.

Aidha, Rais Kikwete amewataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye hata kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata walimvyosaidia yeye katika miaka yake yote 10 ya uongozi wake.

Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa  Ijumaa, Oktoba 16, 2015, wakati alipozungumza na watumishi wa Ikulu katika hafla ya chakula cha jioni ambako watumishi hao waliagana na Rais Kikwete ambaye wamemtumikia kwa vipindi tofauti, wengine wakiwa wamekaa naye kwa miaka yote 10 ya uongozi wake.

Akizungumza na watumishi hao, Rais Kikwete amesema kuwa anaondoka madarakani kwa furaha sana hata kama anaona huzuni kuagana na watumishi hao wa Ikulu ambao amekaa nao kwa miaka mingi, baadhi miaka 10.

“Kwa hakika, naondoka mwenye furaha sana. Ni kweli nasikitika kuwa tunaachana lakini mambo yote mazuri yana mwisho wake. Nimeifanya kazi ya urais kwa miaka 10, nyie mnajua aina ya kazi hii.

 Miaka 10 ni mingi. Ni miaka inayotosha kabisa kwa mkuu wa nchi kukamilisha ajenda yake. Sidhani kama mtu anahitaji zaidi ya miaka 10 kutekeleza ajenda yake ya msingi,” amesema na kuongeza:

“Na hata ukitaka kukaa zaidi huwezi kuyamaliza yote. Mzee Nyerere alikaa miaka 23 hakumaliza yote na yaliyobakia alimwachia Mzee Mwinyi ambaye naye alimwachia yaliyobakia Mzee Mkapa. Rais Mkapa naye alifanya mengi lakini hakumaliza yote na akaniachia mimi. Na mimi nitamwachia yaliyobakia Rais ajaye.”

Kuhusu Rais ajaye ambaye atakuwa mkazi mpya ndani ya Ikulu, Rais Kikwete amesema: “Napenda kuwaombeni msaidieni sana Rais wetu ajaye. Kwa hakika nawaombeni tumsaidie kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata mlivyonisaidia mimi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad