WIZARA YA KAZI NA AJIRA
1. Serikali imepata taarifa za kuwepo kwa mpango wa mafunzo kwa madereva nchini kote, ulioandaliwa na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania-Tanzania Drivers Workers Union (TADWU) kuanzia wiki ijayo. Mpango huo umeelezwa kuwa njia mbadala ya tishio la mgomo lililotolewa na viongozi wa Chama hicho hapo awali, ili kuweza kupata suluhisho la malalamiko yao.
Malalamiko hayo yalihusu Mkataba ya Ajira inayokidhi matakwa ya kisheria, nyongeza ya posho na viwango vya mishahara juu ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta ya usafirishaji na kero nyinginezo za barabarani.
2. Taratibu za Chama kuendesha mafunzo na shughuli nyinginezo za kichama katika sehemu za kazi kwa mujibu wa Sheria ni kama ifuatavyo:-
(i) Wawakilishi wa Vyama vya wafanyakazi wanayo haki ya kuwaarifu Waajiri na kuingia katika eneo la kazi ili kuandikisha wanachama, kuwasiliana na wanachama wao, kukutana na wanachama kujadili masuala yanayohusu mahusiano na Waajiri wao au kwa ajili ya kufanya chaguzi au upigaji kura kwa mujibu Katiba za Vyama vyao.
(ii) Katika kutekeleza haki hiyo, ni lazima Wawakilishi hao wa Vyama wapate ridhaa ya Waajiri kwa kuzingatia vigezo na masharti (utaratibu) yanayolenga kulinda maisha ya watu na mali au kuzuia uvurugaji wa taratibu za kazi au utendaji kazi,
(iii) Vyama vya Wafanyakazi vina haki ya kutoa mafunzo katika sehemu za kazi ambazo kuna matawi yake au kuna wanachama wake wanaotambulika kisheria.
3. Baada ya kutafakari taarifa hiyo ya viongozi wa TADWU na kuzingatia matakwa ya Sheria za Kazi nchini, Serikali imejiridhisha kwamba, taarifa iliyotolewa na uongozi wa TADWU imekiuka matakwa ya Sheria za Kazi. Taarifa hiyo haikuwasilishwa kwa Waajiri husika sehemu ya kazi, ambao TADWU ina wanachama wake inaokusudia kuwahusisha kwenye mafunzo hayo.
Taarifa hiyo haikubainisha ni wafanyakazi gani, wala idadi ya wafanyakazi hao watakaohusika na mafunzo hayo. Hakuna ratiba iliyoidhinishwa na Waajiri, inayohakikisha kuwa hakuna chombo cha usafiri kitakachosimama kufanya kazi na kuepusha usumbufu kwa watumia huduma.
4. Hivyo, Serikali inasisitiza na kuwakumbusha viongozi wa Chama hicho cha TADWU na madereva kwa ujumla, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Sheria za Nchi na kujiepusha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa mali na maisha ya watumia huduma. Aidha, watambue kuwa umakini wao ni muhimu katika kuepusha hatua ambazo zina uelekeo wa kudumaza shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.
5. Kushiriki katika mafunzo yaliyoelezwa na viongozi wa TADWU kwa utaratibu walioueleza ni sawa na kuitisha au kufanya mgomo usio halali.
6. Serikali imefanya jitihada mbali mbali za kuwaelimisha na kuwaelekeza, ikiwemo semina, mafunzo, ushauri na kugawa vijarida/vipeperushi. Elimu hiyo ilihusu taratibu za majadiliano ya pamoja ya kuboresha maslahi na utendaji kazi na utatuzi wa migogoro ya kikazi kisheria ili kuepusha madhara na usumbufu usio wa lazima kwa wanachi wasio husika na utatuzi wa malalamiko yao.
7. Hitimisho: Serikali inapenda kutoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya wafanyakazi vya madereva pamoja na madereva wote nchini kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa hadi sasa katika vikao vya Kamati ya Waziri Mkuu. Aidha, Serikali pamoja na Taasisi zake itaendelea kutoa elimu pamoja na kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitachulikwa dhidi ya wale watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo.
Eric F. Shitindi
KATIBU MKUU
20/08/2015
No comments:
Post a Comment