JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


RAIS ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MWANDISHI WA TBC -DYAULI

Share This

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Clement Mshana, wafanyakazi wake na waandishi wote kwa ujumla kufuatia kifo cha mtangazaji na mwandishi mwandamizi wa TBC Bi. Florence Dyauli.
“Pokea rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na mwandishi mwandamizi na mahiri Bi. Florence” Rais amesema.

“Mbali na uandishi na utangazaji wake mahiri, Bi. Florence alikua mzalendo wa kweli aliyetumikia taasisi hii ya serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake. 

Ni wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”. Amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa: 

“Hakika Florence tutamkumbuka, nawapa pole wafanyakazi wote wa TBC na waandishi wote kwa kuondokewa na mwenzao katika tasnia ya Habari”. Rais ameongeza.

“Salaam pia ziwafikie ndugu na jamaa wa Bi. Florence ambao msiba huu ni mkubwa sana kwao na unawagusa sana, naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa pamoja ni wakati wa kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”. 

Rais amesema na kuwatakia roho ya subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao.

Bi. Florence ambaye amefariki jana  18 Juni, 2015 jijini Dar-es-Salaam alizaliwa Julai 27, 1961. Bi. Florence alianza kazi katika Radio ya Taifa, Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD) na baadaye  Televisheni ya Taifa (TVT) na kwa sasa TBC .

Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
19 Juni, 2015

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad