Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi yanayopelekwa mahakamani. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman na Kulia ni Jaji Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
JAJI Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi yaliyopelekwa mahakamani kwa mwaka wa sheria uliopita wa 2015 na kutoa wito kwa watendaji wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kufanya vizuri licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Jaji Mkuu wa Kenya ametoa pongezi hizo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya kukutana na kuongea na Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Tanzania kufuatia mwaliko alioupata wa kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yatakayofanyika Februari 4 mwaka huu.
Mhe. Dkt. Mutunga amesema kuwa nchi ya Kenya mpaka sasa ina mashauri yapatayo 300,000 ambayo bado hayajaamuliwa na kuongeza kuwa asilimia 5 ya wananchi wa Kenya ndio hupeleka mashauri yao Mahakamani huku asilimia 95 iliyobaki wakitafuta ufumbuzi wa kesi zao nje ya Mahakama.
“Ni kweli Tanzania mnafanya vizuri katika katika kusikiliza mashauri kwa haraka, asilimia 95 ya Wakenya hutafuta ufumbuzi wa kesi zao kwa viongozi wa kidini na Kimila kutokana na baadhi yao kukosa fedha za kutosha za kufuatilia na kugharamia kesi zao” Amesema.
Ameongeza kuwa Mahakama ya Kenya kwa mwaka huu 2016 imejipangia malengo ya kuhakikisha kuwa inasuluhisha mashauri yote ndani ya mwaka mmoja ili kuongeza ufanisi na imani kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Tanzania ina jambo la kujifunza kutoka Kenya kufuatia mageuzi ya Katiba iliyoyafanya mwaka 2010 hususan kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo na nafasi ya Mahakama kwenye Katiba Mpya ambayo Tanzania inaendelea na mchakato wake.
Akizungumzia mageuzi hayo ambayo tayari Kenya imeyafanya kufuatia kuwepo kwa Katiba mpya Mhe. Mutunga amesema kuwa ni pamoja kupungua kwa madaraka ya Rais katika kuteua Majaji, na nafasi za Majaji kutangazwa na watu kupeleka maombi na sifa zao kujadiliwa ambapo wananchi huruhusiwa kutoa maoni kwa Tume ya Mahakama ya Kenya kuhusu majaji hao kabla ya kuapishwa.
Aidha, ameeleza kuwa Watanzania wana kila sababu ya kujivunia umoja na mshikamano uliopo ambao umesababishwa na waasisi wa taifa hilo huku akibainisha kuwa majadiliano na upatikanaji wa Katiba Mpya utafanywa na Watanzania wenyewe kwa kuwa Watanzania ni walimu na mfano wa kuigwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa Kenya amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imenufaika na ujio wake kwa kuwa iko kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo huwakutanisha wadau mbalimbali wa sharia kujadili changamoto na mafanikio ya Sekta ya Sheria nchini.
Amesema kuwa kufuatia ziara ya Jaji Mkuu wa Kenya Mahakama ya Tanzania imejifunza masuala mbalimbali ambayo ni muhimu katika ufanisi wa shughuli zake ikiwemo Maslahi ya Watumishi wa Mahakama, Jukumu la Mahakama kutafsiri Katiba kwa kuangalia historian a uchumi pia kuazima baadhi ya hukumu zilizotolewa nchini Kenya kama ushauri.
Aidha, amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kuendelea kuongeza uwazi katika upatikanaji wa watendaji wake wenye nia ya kuwatumikia wananchi na kuboresha njia za kuwapata majaji.
No comments:
Post a Comment