GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Professa Benno Ndulu (Pichani), ameshinda tuzo ya ‘Gavana Bora wa Afrika kwa mwaka 2015.
Tuzo hiyo inayojulikana kama ‘Central Bank Governor of the Year’ ilitolewa na taasisi ya Africa Investor (Ai) jijini New York, Marekani hivi karibuni katika mkutano wake wa nane uliohudhuriwa na zaidi watu 250 maarufu katika biashara, serikali, maendeleo, sekta ya fedha na wakuu wa nchi tano za Afrika.
Prof. Ndulu aliibuka kidedea kwa kuwashinda magavana wa benki kuu 10 zingine za Afrika za Afrika Kusini, Uganda, Botswana, Sierra Leone, Rwanda, Nigeria, Namibia, Misri na gavana wa Benki Kuu ya nchi za Afrika ya Kati inahudumia nchi sita za Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Guinea ya Ikweta, Gabon na Jamhuri ya Congo.
Ai ni taasisi inayoongoza ya uwekezaji na mawasiliano barani Afrika ambayo inawaleta pamoja wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani wenye vitega uchumi vyao barani Afrika.
Vigezo viliyotumika kumpata gavana bora wa mwaka wa Afrika ni umahiri katika eneo la kazi na kuonesha jinsi umahiri huo ulivyonufaisha sekta ya uwekezaji katika nchi husika na mchango wa magavana katika kuendeleza mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na kikanda (sub-region).
Vingine ni mchango wa magavana katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu ya nchi zao na nafasi zao katika kukuza mtazamo wa Afrika kama kituo bora cha kupokea vitega uchumi.
Katika taarifa yake ya ushindi, Ai ilimpongeza Gavana Ndulu kwa ushindi katika kipengele hicho cha Gavana Bora wa mwaka barani Afrika.
“Mafanikio yako bila shaka yataendelea kutoa hamasa na kivutio kwa viongozi wakuu wa serikali na sekta ya biashara wanaofanya juhudi za kuikuza taswira ya sekta ya uwekezaji barani Afrika,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Ai.
Hii ni mara ya pili kwa Profesa Ndulu kushinda tuzo ya kimataifa tangu alipoteuliwa kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2008. Mwaka 2009, jarida maarufu la Emerging Markets linalochapishwa jijini London, Uingereza, lilimtangaza Profesa Ndulu kuwa ‘Gavana Bora wa Bara la Afrika kwa mwaka huo. Jarida hilo hutambua mafanikio yanayofanywa na watendaji wakuu wa benki kuu na mawaziri wa fedha na kuwapa tuzo wakati wa mikutano ya Benki Kuu ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika kila mwaka.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
Oktoba 12, 2015
No comments:
Post a Comment