JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


PALESTINA KUPEPESHA BENDERA YAKE MAKAO MAKUU YA UMOJA WA MATAIFA

Share This
   Bendera ya  Palestine itapepea nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,   hii inafuatia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  kupitisha azimio ambalo linatoa fursa kwa nchi ambazo si  mwanachama kamili wa Umoja huo  kupeperusha bendera yake Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Ubao wa Matangazo ndani ya Ukumbi Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  ukionyesha matokeo ya kura katika tukio la kihistoria  kufanyika ambapo Baraza hilo  limepitisha azimio linalotoa fursa kwa Palestina kupeperusha bendera yake. Nchi wanachama walipiga makofi kushangilia kupitishwa kwa azimio hilo, ambalo Israel imesema Palestina inatafuta umaarufu kwa njia za mkato badala  ya kurejea kwenye meza ya mazugumzo.
 
Na Mwandishi Maalum New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  jana Alhamis, limepitisha Azimio ambalo kwa mara ya kwanza   tangu kuanzishwa kwa Umoja huo, litaruhusu nchi ambazo  siyo  mwanachama kamili kupeperusha  bendera yake katika  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kupitishwa kwa azimio hilo ambalo  limepigiwa kura  za ndiyo 119 za hapana  nane  na zisizofungamana na upande wowote 45 kunaipa   fursa Palestina kupeperusha  bendera yake nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya  matokeo ya kura kutangazwa rasmi, Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa walipiga makofi kama ishara ya kufurahia kupitishwa kura nyingi azimio hilo.

Palestina   kama ilivyo kwa Vatican inahadhi ya Nchi Mwangalizi isiyo Mwanachama wa Umoja wa Mataifa (Non -Member Observer States)
Kwa mujibu wa  Azimio hilo nambaA/69/L.87 linaloelezwa kuwa ni la kihistoria,  linamtaka   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba Bendera  ya Palestina inapeperushwa ndani ya siku 20  ( septemba 30)wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la  70 la Umoja wa Mataifa.

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya  wajumbe,  Mwakilishi wa Kudumu wa  Iraq na ambaye ni mwenyekiti wa kundi la nchi za kiarabu alisema  kupeperushwa kwa bendera ya   Palestina ni kielelezo  cha utekelezaji wa matakwa yaliyomo ndani ya  Katiba ya Umoja wa Mataifa ya kwamba, nchi zote  na watu wake wako sawa na  wana haki  sawa.
 

Hata hiyo si mataifa yote yaliyoridhika ya uamuzi huo, kwa kile ambacho wengine wameeleza kuwa ni ukiukwaji wa  kanuni za Umoja wa Mataifa ambazo zinaeleza wazi wazi kwamba bendera zinazopashwa kupeperushwa katika  Umoja wa Mataifa ni zile tu  za nchi ambazo ni wanachama kamili.

Kwa upande wake,  Mwakilishi wa Kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa,  yeye   alisema kwamba kupeperushwa  kwa bendera ya  Paletina katika  Umoja wa Mataifa, hakubadilishi hali halisi na mazingira ya sintofahamu yanayoendelea kati yake na Palestina.

 Akizungumza kwa  hisia kali  huku akizilaumu nchi ambazo zimeunga mkono azimio hilo, Mwakilishi huyo wa Israel, ameeleza kwamba Palestina inatakiwa kufanya maamuzi magumu yakiwamo ya kurejea katika meza ya mazungumo  badala ya kutafuta njia za mkato  zikiwamo hizo za kupeperusha  bendera katika Umoja wa Mataifa.

Akasema  yeye kama mwakilishi wa Israel picha ambayo anaamini ndiyo inayostahili kuwa maarufu ni ile ya viongozi wa Israel na Palestine watakapokuwa kwa pamoja wanapandisha bendera ya matumaini  inayoonesha mataifa hayo mawili yakiishi kwa  pamoja kwa  Amani na usalama.
Hoja ya kutaka  Israel na Palestina kurejea kwenye mazugungumo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu baina ya pande hizo mbili  imeungwa mkono na wazungumzaji wengi wakiwamo wale waliopiga  waliopiga kura   ya hapana kama  vile  Marekani .

Kwa  upande wa wale waliounga mkono azimio hilo, walieleza kwamba nchi inapo peperusha bendera yake hata   ni kielelezo cha ufahari, utambulisho na uwepo wake na kwa sababu hiyo Palestine ilikuwa na kila sababu ya  kupeperusha bendera yake ambayo kwayo haibadilishi hadhi yake ya kuwa nchi mwangalizi, lakini ikiandika historia nyingine.

Mwakilishi wa Palestina akiwa na  furaha tele amezishukuru nchi zote ambazo zimeunga mkono azimio  hilo.

Pamoja na  kupitishwa kwa Azimio hilo linalotoa fursa kwa  nchi ambazo si wanachama  kamili kupeperusha  bendera,  Wajumbe wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa pia walipitisha kwa  kupiga kura azimio linalotaka kuangaliwa kwa misingi ya  utaratibu  wa marekebisho ya  ulipaji wa madeni kwa nchi zinazodaiwa.

Azimio hilo   namba A/69/L.84   lililowasilishwa  na Mwenyekiti wa Kundi la Nchi 77 na China ( G77&China) lilipita kuwa kura 136 za ndiyo, sita za hapa na  41 zisizofungamana na  upande wowote

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad