Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepongezwa kwa kuendelea kuboresha utoaji wa mafunzo katika vyuo vyake kote nchini, ikiwemo kuimarisha mitaala inayozingatia mahitaji ya soko la ajira.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, alipotembelea banda la VETA Agosti 12, 2026, katika Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Dimbani, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Wanu alisema VETA imeendelea kufanya vizuri katika kuboresha mazingira ya utoaji wa mafunzo ya ufundi, pamoja na kuhuisha mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira.
“Nawapongeza kwa kuendelea kuboresha hali ya utoaji mafunzo ya ufundi katika vyuo, hali ya uboreshaji wa mitaala yenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira, lakini pia kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Kundi la wanawake na vijana linaendelea kunufaika na mafunzo haya,” alisema Wanu
Kwa upande wake, Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle, alisema Mamlaka hiyo inaendelea kutoa mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira, hatua inayolenga kuwawezesha wahitimu kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine.
VETA inashiriki katika Tamasha la Kizimkazi lenye kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga, Shangwe na Fursa,” ambalo ufunguzi wake rasmi ulifanyika Agosti 12, 2026, huku kilele cha tamasha hilo kikitarajiwa kufanyika Agosti 14, 2026.
Mamlaka hiyo imeendelea kuwaalika wananchi kutembelea banda lake katika viwanja vya Dimbani, kupata taarifa kuhusu fursa za mafunzo ya ufundi stadi, kuona bidhaa mbalimbali za ubunifu pamoja na kupata huduma za ufundi wa simu za mkononi.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment