JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WIZARA YA AFYA YATAJA SABABU ZA SERIKALI KUJA NA SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Share This


Na Mwandishi Wetu ,Michuzi TV

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu ameelezea hatua kwa hatua sababu za msingi ambazo zimefanya kuwasilisha mapendekezo Bungeni ya kutaka kuwepo kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma za afya kwa kulipia kabla ya kupatwa na maradhi.

Aidha amesema katika mapendekezo yaliyomo kwenye muswada wa sheria hiyo ambayo tayari imesomwa kwa mara ya kwanza Bungeni hakutakuwa na kushurutishwa kwa mwananchi kuwa na bima ya afya ingawa wamefungamanisha bima ya afya na baadhi ya huduma nyingine muhimu akitolea mfano wa leseni za magari au leseni ya biashara.

Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Septemba 27,2022 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote huku akitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wananchi kuhusu bima hiyo na utaratibu utakaotumika katika kujiunga.

Akifafanua zaidi Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa pamoja na hatua mbalimbali ambazo Serikali imechukua katika kuboresha huduma za afyakwa kujenga miundombinu, kukunua dawa na vifaa tiba, changamoto kubwa ipo katika wananchi kumudu gharama za matibabu.

“Moja ya changamoto ni kuhusu uwezo wa wananchi kugharamia huduma za afya, kwa hiyo tumeangalia kwa upande wa ugharamiaji wa huduma za afya kwa mfano kwa mwaka 2019 matumizi ya malipo ya papo kwa papo yaani mwananchi akienda hospitali kulipia huduma za afya kwa kaya moja ya watu sita walikuwa wanatumia wastani wa kama sh.560,000 na ukipiga hesabu nis sawa na Sh. trilioni 1.7 kwa mwaka mzima .

“Tumeona wananchi wengi wanatumia fedha nyingi kulipia huduma za afya , sasa utaratibu huu wa malipo ya papo kwa papo imekuwa changamoto kubwa inayosababisha wananchi wengi kutokuwa na uhakika wa huduma za afya pindi wanapougua na tumekuta wananchi wanauza mashamba, pikipiki na wengine wanauza nyumba kwa ajili ya matibabu ya huduma za afya,”amesema Waziri Ummy.

Amefafanua mfumo wa kupata huduma za afya kwa kulipa kutoka mfukoni papo kwa hapo zinaingiza kaya nyingi katika umasikini mkubwa na hilo ni jambo ambalo wamejiridhisha wamethibitisha pasi na shaka akitoa mfano sasa hivi kuna ongezeko kubwa la magonjwa haya yasiyo ya kuambikiza ambayo matibabu yake yanagharimu fedha nyingi.

“Mathalani gharama ya mgonjwa saratani ni Sh.milioni 26 kwa mwaka , gharama ya kusafisha damu uwe na tatizo la figo unatakiwa kusafisha damu kwa mwaka kwa mgonjwa mmoja kama Sh.milioni 32 , watanzania wangapi wanaweza kulipa Sh.milioni 32 ,watanzania wangapi wanaweza kulipa Sh.milioni 26.

“Kwa hiyo kutokana na gharama kubwa hizi wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama hizo na kupata athari zaidi za kiafya na wakati mwingine kupoteza maisha.Kutokana na changamoto hiyo Serikali imedhamiria kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kuimarisha mfumo wa bima ya afya na kuwawezesha wananchi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua kwa kujiunga na bima ya afya.

“Na hivyo kuwawezesha kupata huduma za afya wakati wote wanapozihitaji karibu na maeneo yao. Kwa hiyo tumeangalia takwimu za mwaka 2021 mpaka Desema , wananchi ambao wanatumia bima ya afya na hapa nimehesabu mpaka bima ya afya ya Mfuko wa Jamii (CHF) ambao malalamiko ni mengi , wanakata CHF wanalipa Sh.30,000 lakini bado wakienda hospitali wanaambiwa hakuna dawa, hakuna vipimo , kwa hiyo kati ya watanzania takriban 60,000 ni asilimia 15 tu wanapata huduma za afya mfumo wa kulipia kabla ya kuugua , kulipia bima ya afya.

“Kwa hiyo kila watanzania 100, watanzania 15 tu ndio wana bima ya afya na katika hao 15 ni watanzania nane tu ndio wana bima ya afya hizi kubwa za NHIF na bima binafsi .NHIF asilimia 8 , bima binafsi ni kama asilimia 1. Kwa sababu hata CHF yenyewe inachangamoto na ndio maana mapendekezo haya tumeyapeleka Bungeni tumefuta HF tutakuja na utaratibu mwingine,”amesema.

Ameongeza kwasababu CHF kama umekata kwenye halmashauri ya Jiji la Tanga inatumika tu pale ndani ya halmashauri ya jiji hiyo, haiwezi kutumika katika halmashauri nyingine lakini kuna baadhi ya mikoa wameona wameanza inatumika ndani ya Mkoa akitoa mfano wa Mkoa wa Dar es Salaam .

“Lakini kwa ujumla wananchi wamekuwa wakilalamikia hii bima ya afya ya jamii kwamba wametoa Sh.30,000 zao kwa kaya ya watu sita lakini hakuna matibabu au huduma nzuri ambazo wanazipata , kutokana na ukweli huu Serikali ilianza mchakato wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ikiwa ni kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kikwazo.

“Kwa hiyo haya maandalizi yalianza mwaka 2012 na kutokana na umuhimu wa suala hili tulifanya uchambuzi wa mapitio mbalimbali na suala la kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na tunakumbushwa kitaifa na kimataifa.Tulikuwa tunafanya majadiliano na makundi mbalimbali ndani ya Serikali, juzi tulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri mapendekezo ya haraka na tukapata baraka , tumeenda kuomba twende bungeni na sasa hivi tuna tayari muswada wa sheria ya bima afya kwa wote umeshasomwa kwa mara ya kwanza bungeni.

“Sasa uko chini au mikono ya Bunge , taratibu za Bunge kwamba kamati husika ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itakwenda kusikiliza maoni na ushauari wa wananchi .Tumependekeza kwa hiyo ni mapendekezo na mapendekezo yetu sisi tumejifunza kutokana na uzoefu kwani ukisema bima ya afya isiwe lazima wengi hawatajiunga,”amesema.

Amesema kwasababu watumishi wa Serikali ni lazima iwe kwa anayeumwa , asiyeumwa ana wote bima ya afya , hivyo ukifanya hiyari wanaojiunga ni asilimia 99 karibu ni wagonjwa.“Kwa maana hiyo bima ya afya mnakuwa watu 100 mnachangiana katika 100 wataumwa watu 20, wale 80 watawalipia watu 20 wanaoumwa , lakini sasa tukienda na dhana ya uhiyari uzoefu uanesha mko watu 100 wanaumwa 80 ,na hao 20 wanawachangia watu 100.

“Hakuna bima ya afya, hakuna uendelevu wa bima ya afya kwa wote, hivyo tumependekeza Bunge ndio litapitisha Sheria, sisi kama Serikali tumependekeza hili suala liwe ni lazima lakini ulazima ndio umenifanya nizungumze na wana habari , hakuna mtanzania ambaye atakamatwa, atafungwa , atalipishwa faini kwa kutokuwa na bima ya afya.

“Hakuna hicho kifungu lakini tunawapataje Watanzania ambao hawaumwi wajiunge na bima ya afya ndio maana tumependekeza kuifungamanisha na baadhi ya huduma , kwa hiyo tumefungamanisha na baadhi ya huduma , na huduma hizo tumesema unataka leseni ya biashara unaulizwa bima ya afya iko wapi kwani inakuwa moja ya kigezo hitaji tena baadae nikasema labda tuondoe tuseme leseni ya udereva, hivi unawapata wapi watanzania ambao hawaumwi , hawaingii kwenye kitambulisho, inabidi umsubiri kwenye leseni ya udereva.

“Leseni ya biashara kwasabau sio lazima hakuna mtu atakamatwa hakuna mtu atafungwa kwa hiyo lazima na tumefanya utafiti tumeenda Ghana , Rwanda, Ethiopia , tumefanya utafiti ili watu waingie lazima tuifungamanishe na baadhi ya huduma , kwa hiyo mapendekezo ambayo tumeyapeleka kwenye Bunge na Bunge litapokea maon,”amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Ameongeza kuwa ameona jambo hilo aliweke sawa ili kuwatoa hofu Watanzania, lengo la Serikali ni kuwapunguzia mzigo Watanzania, ni wajibu wa Serikali na kwamba kilio kimekuwa kikubwa kuhudu gharama za huduma za afya.

“Kilichothibitika kitaifa na kimataifa wananchi wamudu gharama za matibabu ni kulipa kabla ya kuugua na sisi tumewaambia kwenye hii bima haitakuwa eti watu wote lazima wajiunge kwenye NHIF utachagua mwenyewe.Pia kwenye huu muswada tunapendekeza mambo kadhaa kwa mfano kuweka kitita cha mafao chenye usawa ambacho kila mwananchi atakayejiunga na bima ya afya atakuwa na uhakika wa kukipata .

“Maana tukisema tu bima ya afya fungulia mbwa kila mtu aanzishe bima ya afya wananchi wachukuliwe 10,000 zao bado hawatapata huduma bora, kwa hiyo tutaweka kitita cha msingi kwamba ni kipi ndicho tutakiweka kwenye kanuni,”amesema.

Waziri wa Afya Mhe, Ummy Mwalimu akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari leo Septemba 27,2022 jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote huku akitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wananchi kuhusu bima hiyo na utaratibu utakaotumika katika kujiunga.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad