JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MAJALIWA: TUTAYAENZI MAONO, JITIHADA NA JUHUDI ZA HAYATI MAGUFULI

Share This

 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza kwamba Serikali itaenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli hususan katika ulinzi wa rasilimali za Taifa pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Pia, Waziri Mkuu ametaja mambo mengine yatakayoendelezwa ni pamoja na  nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, kuunganisha na kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa Kitaifa.

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 13, 2021) wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

 

Amesema Serikali itatekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira. “Kwa kasi tuliyoanza nayo, Serikali itaendelea kuongeza nguvu zake na hatimaye kukamilisha miradi hiyo.”

 

“Serikali itaendelea kuimarisha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya. Pia itaimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii na kuchukua hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo  yanayotolewa na wataalam.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini na kikabila waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa ili waweze kulinda mafanikio waliyoyapata. “Jitihada hizo ndizo zimetuwezesha kuingia katika nchi za uchumi wa kati.”


Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh.116,784,244,000.00 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa matumizi ya mwaka 2021/2022. Amesema kati ya fedha hizo, sh. 93,303,370,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 23,480,874,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

 

“Mheshimiwa Spika, vilevile naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 128,873,377,000.00 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 121,875,906,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na shilingi 6,997,471,000.00 ni kwa ajili ya maendeleo.”


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA

JUMANNE, APRILI 13, 2021.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad