JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Vodacom Tanzania PLC Yaleta Huduma ya Kulipia Mafuta kwa M-Pesa, Vituo vyote vya Mafuta vya Oryx Nchini.

Share This

Wateja kurudishiwa asilimia 5 ya kiasi watakacholipia mafuta kupitia M-Pesa papo hapo.

  Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza kiteknolojia nchini, Vodacom Tanzania PLC na kampuni ya kuuza mafuta ya Oryx Oil Tanzania wameingia katika ushirikiano mpya kusaidia wateja wao wa M-Pesa kupitia huduma ya 'Lipa kwa Simu' kulipia mafuta.  Huduma ya 'Lipa kwa Simu' itapatikana katika vituo vyote vya mafuta vya Oryx nchi nzima. Zaidi ya malipo, huduma hii inakusudiwa kuongeza urahisi kwa wateja wakati huo huo ikimarisha mfumo wa malipo

Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hii  uliofanyika katika kituo cha mafuta cha Oryx kilichoko Mwenge jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Oil, Chris Swart amesisitiza katika umuhimu wa kutumia vifaa vya kidijitali kama vile M-Pesa katika kuchakata miamala na kukusanya mapato akisema kwamba mwenendo huu utaboresha usalama, urahisi na uwazi kwa wateja na biashara. 

"Tunaendelea kupeleka njia mbadala za malipo kwenye vituo vyetu vyote vya mafuta kwa dhumuni la kuwapa wateja wetu urahisi na pia usalama. Ninaishukuru Vodacom M-Pesa kwa kushirikiana na Oryx katika jitihada hizi ili kuhakikisha huduma ya malipo kwa njia ya simu za mkononi inapatikana kwa wateja wetu wote bila kujali mtandao anaotumia. Nina uhakika kwamba huduma hii itafanya malipo kuwa rahisi na kutunufaisha sisi kwa kuboresha ufanisi katika utunzaji wa kumbukumbu za miamala na kuboresha usalama wa kifedha katika vituo vyetu vyote nchini", alibainisha bw. Swart wakati akiwahamasisha wateja kutumia huduma hii. 

Vodacom Tanzania PLC imekuwa ni kampuni ya kwanza kuwezesha ushirikiano wa malipo kati ya mtu binafsi na biashara jambo linalosaidia zaidi katika kukuza ushirikishwaji wa kifedha katika eneo la malipo.  Kwa kupitia huduma ya 'Lipa kwa Simu' mteja anaweza kutumia App ya M-Pesa yenye QR Code na waleti zingine zilizoko katika simu za mkononi kufanya malipo na kupata thamani zaidi katika vituo vya mafuta vya Oryx kwa sababu malipo yanakuja na bonasi ya kurudishiwa papo hapo asilimia 5 ya malipo yote utakayofanya kupitia M-Pesa.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Vodacom M-Pesa, Mkuu wa mipango na Biashara wa M-Pesa, Nelusigwe Mwangota amebainisha kwamba huduma ya 'Lipa kwa Simu’ inashuhudia kiwango kikubwa cha utumikaji nchi nzima kutokana na wafanyabiashara wengi zaidi na wauzaji wa rejareja kukusanya malipo kwa urahisi wakati huo huo wakiwasaidia wateja kuepukana na hatari zinazoambatana na ubebaji wa fedha taslimu. Amesema kampuni itaendelea kukuza mifumo ya malipo ya kidijitali ili kuwezesha mauzo ya rejareja nchini, hili litafanyika kwa kupanua huduma hii kwa taasisi nyingi zaidi za serikali na za binafsi. 

Zaidi ya Watanzania milioni 10 tayari wanatumia huduma ya M-Pesa kwa ajili ya kufanya aina mbalimbali za malipo kama vile kulipa bili au Ankara za aina mbalimbali, malipo ya serikali, usafiri, manunuzi ya rejareja na mengine mengi. “Vodacom Tanzania PLC kama kampuni tunahamasisha agenda ya kuwa na jamii ambayo haitumii fedha taslimu. Kwa hiyo malengo yetu ni kuongeza wigo wa miamala isiyo ya fedha taslimu kwa  kuongeza njia mbadala za malipo kupitia simu za mkononi” alisema Mwangota.

“Kwa kupitia ushirikiano huu watanzania wataweza kufanya malipo kwa kupitia simu za mkononi kwa kutumia huduma ya ‘Lipa kwa Simu’ katika vituo vya Oryx na vituo vingine vya mafuta ambavyo tunashirikiana navyo kwa madhumuni ya kufanya maisha kuwa rahisi, salama na yenye ufanisi zaidi,” aliongeza Mwangota.
Mkuu wa Idara ya Lipa kwa simu kutoka M-Pesa, Kilian Kamota (kulia) akiwa na mteja, Elia Richard wakizindua huduma mpya ya "Lipa kwa simu" jijini Dar es Salaam, inayomuwezesha mteja kulipia mafuta kwenye vituo vya mafuta vya Oryx nchini kote kupitia simu yake ya mkononi kwa kutumia App ya M-Pesa yenye QR Code na kurejeshewa asilimia 5 za malipo papo hapo.

Mkuu wa Idara ya Lipa kwa simu kutoka M-Pesa, Kilian Kamota (kulia) akipeana mkono na mteja, Elia Richard mara baada ya kuzindua huduma mpya ya "Lipa kwa simu" jijini Dar es Salaam, inayomuwezesha mteja kulipia mafuta kwenye vituo vya mafuta vya Oryx nchini kote kupitia simu yake ya mkononi kwa kutumia App ya M-Pesa yenye QR Code na kurejeshewa asilimia 5 za malipo papo hapo. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Oil, Chris Swart (wapili kulia) na Mkuu wa mipango na Biashara wa M-Pesa, Nelusigwe Mwangota.

Mkuu wa mipango na Biashara wa M-Pesa, Nelusigwe Mwangota akizungumza na wanahabari na wadau waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa huduma ya "Lipia kwa simu" kutoka M-Pesa

Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Oil, Chris Swart akizungumza na wanahabari na wadau waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa huduma ya "Lipia kwa simu" kutoka M-Pesa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad