JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAKULIMA WATAKIWA KUWA NA VITAMBULISHO- WAZIRI HASUNGA

Share This
     Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akisoma hotuba ya Ufunguzi rasmi  wa masoko ya Tumbaku kwa msimu mpya 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya.
   Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akielezea masuala ya Ushirika wakati wa Ufunguzi wa masoko ya Tumbaku Mkoani Mbeya  

   Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mary Prisca Mahundi akiongea wakati wa ufunguzi wa wa masoko ya Tumbaku kwa msimu mpya 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya.
    Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akielezea masuala ya Ushirika wakati wa Ufunguzi wa masoko ya Tumbaku Mkoani Mbeya
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ametoa wito kwa wakulima nchini kuwa na Vitambulisho ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mkulima kwa urahisi kama vile aina ya kilimo anachofanya, eneo analotoka, mazao anayolima na taarifa nyingine muhimu za utambulisho wake. 

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa masoko ya minada ya Tumbaku wa mwaka 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita Juni 26, 2020. Akifungua masoko hayo Waziri alisisitiza kuwa ni muhimu wakulima kuwa na vitambulisho kwani kilimo ni moja ya Sekta muhimu za uchumi wa Taifa letu kutokana na kilimo kuchangia pato la Taifa pamoja na asilimia 30 ya fedha za kigeni kwa mahitaji ya kibiashara, ajira, chakula, na malighafi za viwandani. 

“Kila mkulima asajiliwe, ajulikane yuko wapi analima kiasi gani, analima zao gani, analima ukubwa gani wa shamba, kiwango cha mavuno anachopata pamoja na changamoto alizonazo,” alisisitiza Waziri 

Katika hotuba ya ufunguzi huo, Waziri alitoa maelekezo kwa maafisa Ugani wafanye kazi zao kwa bidii wakizingatia kuwahudumia wakulima mashambani. Aliongeza kuwa maafisa ugani watumie muda wao mwingi mashambani ambapo ndipo wanapohitajika kutumia taaluma zao kuongeza uzalishaji wa kilimo chenye tija nchini. 

Aidha, ameitaka Bodi ya Tumbaku nchini kuongeza kasi ya utafutaji wa masoko ya tumbaku inayozalishwa nchini kutokana na changamoto ya kupungua kwa wanunuzi wa zao la tumbaku pamoja na bei ya zao hilo kuendelea kushuka hivi karibuni. Jambo ambalo linasababisha kipato kwa wakulima kuadhirika na mapato ya Serikali kupungua. 

Pamoja na mambo mengine ameagiza Viwanda vya tumbaku visiuzwe bali vifufuliwe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuendeleza na kuimarisha Uchumi wa viwanda, ambapo viwanda hivyo vitatumia mazao na malighafi za kilimo, kuongeza ajira na kukuza Sekta ya Viwanda. 

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akizungumza katika uzinduzi huo amesisitiza Vyama vya Ushirika kuendelea kujikita katika kujenga na kuimarisha mitaji yake ya ndani ili kuwa na nguvu zaidi za kiuchumi katika Vyama itakayowezesha kukopesheka vizuri kwa riba nafuu kutoka kwenye taasisi za Kifedha na mabenki. 

Dkt. Ndiege alieleza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wale wote watakaobainika kufanya shughuli za ushirika katika vyama bila kufuata taratibu au watumishi watakaokiuka maadili ya utumishi wa Umma, akimalizia kwa kuwaomba wadau kuendelea kutoa ushirikiano. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa tumbaku Bw. Emmanuel Charahani (T.C.J.E) katika hotuba yake ameelezea baadhi ya changamoto katika kilimo hicho ni kuendelea kuporomoka kwa wastani wa bei ya tumbaku. Akifafanua kuwa msimu wa 2016/17 wastani wa bei ulikuwa dola 2.06 lakini msimu huu ambao soko la tumbaku limefunguliwa bei ya wastani ni dola 1.60. Hali inayopelekea wanunuzi na wakulima wa tumbaku kuzidi kupungua na kuiomba Serikali kusaidia kunusuru hali hiyo kwa kutafuta wanunuzi zaidi wa tumbaku. 

Charahani amesema matarajio ya kitaifa ni kuzalisha kilo millioni 57 za tumbaku ambazo zinauzwa sasa, hii ikiwa imetokana na hali ya hewa mwaka huu ya mvua nyingi zilizosababisha mbolea kupotea ardhini. 

Aidha Mwenyekiti Charahani ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi inavyoendesha na kusimamia shughuli mbambali za kilimo kwa kutetea maslahi ya watu wanyonge. Aliongeza pongezi mahususi kwa Serikali kuondoa baadhi ya tozo na kodi za tumbaku ambazo zitasaidia kujenga hoja zenye nguvu katika kujadiliana bei ya tumbaku 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad