JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


RAIS DKT MAGUFULI MGENI RASMI KWENYE MASHINDANO MAALUMU YA 20 YA QUR-AAN TUKUFU AFRIKA

Share This
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano ya Qur’aan Tukufu yaliyojumuisha nchi mbalimbali za Afrika, na kwa kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 19 Mei, 2019 wakati akihutubia katika Mashindano Maalum ya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyohusisha washiriki kutoka nchi 18 za Afrika na kufanyika katika Uwanja Mkubwa wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga Misikiti 50 hapa nchini, Serikali inatambua kuwa Taasisi ya Al-Hikma imesaidia jamii kwa kuchimba visima vya maji 110, imejenga shule 1 ya msingi na shule 2 za Sekondari na inawasomesha watoto yatima 400.

Kutokana na mchango huo, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru taasisi hiyo pamoja na taasisi zingine mbalimbali zinazomilikiwa na Madhehebu ya Dini ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuhudumia jamii kwenye sekta za elimu, afya na kutoa misaada ya kibinadamu.

Kufuatia maombi yaliyotolewa na Taasisi ya Al-Hikma, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo kuhakikisha taasisi hiyo inapatiwa hati ya umiliki wa eneo ililoomba libadilishiwe matumizi kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kitakachotoa huduma kwa wananchi wote ifikapo Ijumaa (24 Mei, 2019).

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza washiriki wote wa mashindano hayo ya Qur’aan Tukufu, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Serikali ya Saudi Arabia na wadau mbalimbali kwa kufanikisha mashindano hayo ambayo licha ya kuimarisha misingi ya kumcha Mwenyezi Mungu, yanaimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Saudia Arabia pamoja na Mataifa yote yanayoshiriki.

Amemtaka Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Saudi Arabia Mhe. Dkt. Swalehe Al-Sheikh (ambaye amehudhuria katika mashindano hayo) kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia, ambapo pamoja na shukrani kwa uhusiano mzuri wa Tanzania na Saudia Arabia ameomba nchi hiyo ijenge Msikiti mkubwa hapa nchini kwa ajili ya Waislamu kufanya Ibada zao.

Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri Waislamu wote katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na amezitaka mamlaka za Serikali kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wenye tabia ya kupandisha bei za vyakula wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana na Waislamu katika mashindano hayo na amewataka Watanzania kuendelea kumuombea kutokana na kazi nzuri anazozifanya za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa kasi kubwa na kudumisha umoja wa Watanzania.

Nae Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema uwepo wa Mhe. Rais Magufuli katika mashindano hayo na hotuba aliyoitoa imedhihirisha dhamira yake ya kuimarisha umoja na mshikamano kwa Watanzania wote na kwamba Waislamu wote wamefarijika sana.
Mhe. Rais Magufuli amekabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ambapo aliyeibuka mshindi wa kwanza ni Mouhamed Diallo (Senegal), wa pili ni Faruq Kabiru Yakubu (Nigeria), wa tatu ni Shamsuddin Hussein Ally (Zanzibar), wa nne ni Idrissa Ousmane (Niger) na wa tano ni Sumaiya Juma Abdallah (Pwani, Tanzania).

Pamoja na viongozi hao, mashindano hayo yamehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na viongozi mbalimbali wa Madhehebu ya Dini na vyama vya siasa.
  
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Mei, 2019 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimzawadia Bw. Mohamed El Moujabba Diallo wa Senegal baada ya kuzoa Alama 99.88 na kuibuka mshindi wa Kwanza wa Washindi wa Kuhifadhi Juzuu 30 katika mashindano maalumu ya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika
yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Jumapili Mei 19, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimzawadia Bi. Sumayyah Juma Abdallah wa Tanzania baada ya kupata alama 98.66 na kuibuka mshindi wa tano wa Washindi wa Kuhifadhi Juzuu 30 katika mashindano maalum ya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Jumapili Mei 19, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimzawadia Bw. Idrissa Ousmane wa Niger baada ya kupata Alama 98.67 na kunyakua ushindi wa nne wa Washindi wa Kuhifadhi Juzuu 30 katika mashindano maalumuya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Jumapili Mei 19, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimzawadia Bw. Shamshuddin Hussein Ali wa Zanzibar baada ya kuzoa Alama 98.83 na kuibuka mshindi wa tatu wa Washindi wa Kuhifadhi Juzuu 30 katika mashindano maalumuya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika
yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Jumapili Mei 19, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia maelfu ya waumini wa Kiislamu na wadau wengine wakati akihitimisha mashindano maalumuya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Jumapili Mei
19, 2019.PICHA NA IKULU

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad