MAMILIONI YA WATAZANIA WALIOKOSA MATUMAINI YA KUPONA MAGONJWA MBALIMBALI,SASA KUPATA TUMAINI JIPYA - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

MAMILIONI YA WATAZANIA WALIOKOSA MATUMAINI YA KUPONA MAGONJWA MBALIMBALI,SASA KUPATA TUMAINI JIPYA

Share This

Picha ya pamoja.
Mwenyekiti wa IPP Dkt.Reginald Mengi akizungumza na wadau mbalimbali katika mkutano wa kimataifa wa wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa IPP Dkt.Reginald Mengi jana jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na wadau mbalimbali  katika mkutano wa kimataifa wa wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka,MMG)

 
 
MAMILIONI ya watu waliokosa matumaini ya kupona magonjwa mbalimbali hapa nchini, ambayo yaliaminika kuwa hayaponi kwa tiba ya kawaida sasa watapata tumaini jipya kufuatia ujio wa maabara ya kisasa ya tiba inayotumia teknolojia ya seli shina 'Stem Cell'.

Kwa teknolojia hiyo mpya, ambayo inatumia chembechembe za seli za mwanadamu kutibu kiungo chochote katika mwili husika, inatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa mpaka yasiyoambukiza yakiwemo saratani zote, utindio wa ubongo, seli mundu, kisukari, ualbino na kupooza.

Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, alibainisha tiba hiyo ya seli shina ina uwezo mkubwa na tayari imethibitika duniani kumrudisha mtu aliyefika hatua ya uzee kuwa kijana mwenye afya njema.

Dk. Mengi kupitia kampuni yake ya IPP - Utafiti, Teknolojia na Ugunduzi, akishirikiana na wataalamu mbalimbali duniani, amesema ataanzisha maabara hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni upatikanaji wa vibali kutoka serikalini.

Alisema kuanzishwa kwa maabara hiyo hakuna maana kwamba anapingana na uumbaji wa Mungu kuwa ni lazima binadamu afe, lakini lengo ni kuhakikisha wale wanaopitia maumivu na tabu kubwa kutokana na kukosa tiba ya magonjwa yanayowasumbua yakiwemo yanayotokana na umri mkubwa wanapata tiba hapa hapa nchini.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema serikali haina tatizo juu ya hilo, kwa sababu ni maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya nchini na kumtoa hofu Dk. Mengi kuwa vibali hivyo vitapatikana haraka.

Lakini pia alisema kuwa serikali imetumia nguvu kubwa kuboresha sekta ya afya kwenye uboreshaji miundombinu na kuanzisha tiba mpya ambazo awali hazikuwepo hapa nchini ikiwemo upandikizi wa figo, uongezaji wa bajeti, upandikizi wa ini na ute wa mifupa 'Bone Marrow'.

Alisema tiba ya seli shina ni ya kisasa, ikiwa na uwezo mkubwa wa kutibu mtu kutokana na seli zake mwenyewe lakini alitahadharisha kuwa kwenye kila hatua ya tiba hiyo lazima maadili yazingatiwe na miiko ya kitabibu kama zinavyoelekeza kanuni za kada hiyo kote duniani.

Dk. Ndugulile alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwenye uboreshaji wa sekta ya afya ili kuhakikisha kunakuwa na kasi kubwa ya maendeleo kwenye eneo hilo lililo uti wa mgongo wa maendeleo ya sekta zingine zinazotengemea nguvu kazi ya binadamu kwenye ukuaji wake.

Kwa upande wake Dk. Michael Magoti ambaye ni Mratibu mipango wa IPP Utafiti, Teknolojia na Uvumbuzi, alisema mkutano huo wa kwanza wa kimataifa umejumuisha wadau wa tiba kutokana nchi za Marekani, Australia, India, Thailand, Vietnam na Egypt.

Alisema pamoja na maabara ya utafiti, Dk. Mengi kupitia kampuni yake ya IPP Utafiti, Teknolojia na Uvumbuzi ana mpango wa kuanzisha kliniki ya tiba kwa watoto wenye utindio wa ubongo ambayo itasaidia sehemu kubwa ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya kiakili kwa kutumia matibabu ya seli shina hapa nchini.

Naye Profesa Dk. Kampon Sriwatanakul, raia wa Thailand ambaye pia ni mtaalamu mshauri wa teknolojia hiyo ya tiba kutoka IPP, alisema amejitoa kuja Tanzania kumsaidia Dk. Mengi kufikia ndoto yake ya kuwafikia mamilioni ya watu wenye shida za kiafya ambazo tayari wamekata tamaa ya kupona.

Alisema kupitia teknolojia ya tiba ya seli shina, wana uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa mengi sugu ambayo kwa tiba za kawaida imeaminika kuwa hayawezekani kwenye hospitali nyingi kubwa zikiwemo zile za kimataifa zisizotumia teknolojia hiyo ya kisasa ya tiba.

Katika mkutano huo, jumla ya mada tisa zinazohusiana na tiba ya seli shina ziliwasilishwa na wataalamu waliobobea kwenye kada ya afya kutoka nchi kadhaa za Ulaya, Marekani na Asia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad