WAZIRI PROFESA NDALICHAKO AAGIZA VYUO VINAVYOTOA ELIMU YA 'UBABASHAJI' VIFUTWE - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

WAZIRI PROFESA NDALICHAKO AAGIZA VYUO VINAVYOTOA ELIMU YA 'UBABASHAJI' VIFUTWE

Share This

 Na Said Mwishehe, Globu ya jamii 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa maagizo kwa Baraza la Elimu ya Ufundi(Nacte)kutosita kuchukua hatua ikiwamo ya kuvifuta vyuo ambavyo vitabainika kutoa elimu kwa ubabaishaji.

Pia amelishauri Baraza hilo kuhakikisha linasimamia na kutoa muongozo kuhusu program mbalimbali za utoaji elimu ya ufundi ambayo ametaka iwe inaendana na soko la ajira nchini ili kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kuajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi katika miradi mikubwa inayoendelea nchini.

Profesa Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anazindua rasmi Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi nchini ambalo Mwenyekiti wake ni Profesa John Kandoro.

Kuhusu vyuo ambavyo vinashindwa kutoa elimu bora, Profesa Ndalichako amesema baraza hilo lisisite kuchukua hatua ikiwamo ya kuvifutia usajili vyuo ambavyo vitabainika kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Amefafanua haiwezekani vijana wawe wanalipa fedha kwenye vyuo ambavyo elimu wanayotoa ni ya ubabaishaji na kwamba hilo halikubaliki na lazima hatua zichukuliwe.

“Kuna vyuo ambavyo vipo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kutoa elimu bora lakini pia kuna vyuo ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya biashara na hivyo ndivyo vyenye matatizo.“Kama kuna mtu aliamua kuwekeza kwenye kunzisha chuo kwa ajili ya kufanyabiashara basi atambue ni bora atafute kazi nyingine ya kufanya na sio hiyo tena,”amesema Profesa Ndalichako.

Amesisitiza kuwa anafahamu kuwa kuna vyuo ambavyo tayari vimefutiwa usajili lakini akalitaka baraza hilo kuendelea kuvifuatilia vyuo na vile ambavyo vitabainika kutokidhi vigezo basi navyo vifutiwe usajili.Ameongeza ni jambo la kusitikisha unapoona mtu amehitimu katika chuo fulani lakini uwezo wa kufanya kazi haupo na ukiuliza sababu utaambiwa ni ubabaishaji wa elimu inayotolewa na kwamba lazima hilo lifike mwisho.

Wakati huo huo Profesa Ndalichako ametoa ushauri kwa baraza hilo kuhakikisha elimu ya ufundi ambayo inatolewa kwenye vyuo vilivyopo nchini inakwenda sambamba na mahitaji ya Serikali ya Awamu ya Tano inayozungumzia Serikali ya viwanda nchini.

Amesema ili kufanikisha Serikali ya viwanda maana yake wanahitaji na watalaamu katika fani mbalimbali na hivyo ni jukumu la baraza kuandaa program za mafunzo ambazo zitaleta tija kwa Taifa.“Baraza ni vema mkafanya tafiti ambazo zitawapa picha halisi ya nini ambacho vijana wa Tanzania wanatakiwa kujifunza katika eneo hili la elimu ya ufundi kwa maslahi mapana ya nchi.

“Tunatarajia mafunzo ambayo mwanafunzi atayapata akiwa chuoni na baada ya kumaliza hapati changamoto ya kutafuta ajira.Lazima muandae program ambazo zitawawezesha vijana kuajirika kwa urahisi na hasa kipindi hiki ambacho kuna miradi mikubwa ya kihistoria inatarajia kuanza na mingine inaendelea,”amesema .

Amewakumbusha kuwa pamoja na maelezo ambayo ameyatoa kwa baraza hilo ni vema wataendelea kutekeleza majukumu yao kama ambavyo sheria, miongozo na kanuni inavyoelekeza.Kuhusu baraza hilo Profesa Ndalichako amesema analipongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo ya kuhakikisha wanasimamia vyuo vya elimu ya ufundi chini kwa lengo la kuona elimu inayopatikana inakuwa bora.

Kwa upande wake Profesa Kandoro amesema baraza hilo hilo litasimamia vema majukumu yake na kwamba ushauri na maagizo ya Waziri Ndalichako watayafanyia kazi.Pia uongozi wa Baraza hilo nalo limemhakikishia Profesa Ndalichako kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha huku wakitumia nafasi hiyo kuelezea baadhi ya changamoto ikiwamo ya uhaba wa watumishi.
 Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungunza leo jijini Dar es Salaam wakati anazindua rasmi Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
 Baadhi ya washiriki kwenye uzinduzi wa Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi wakimsikiliza mgeni rasmi Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako(hayupo pichani).
 Mkurugenzi wa Nacte akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Profesa John Kandoro akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad