NZEGA MJI YAHAMISHA STENDI YA ZAMANI KUONDOKA MSONGAMANO KATIKATI YA MJI - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

NZEGA MJI YAHAMISHA STENDI YA ZAMANI KUONDOKA MSONGAMANO KATIKATI YA MJI

Share This
NA TIGANYA VINCENT,TABORA

HALMASHAURI ya Mji Nzega imefanikiwa kuhamisha mabasi yote ya abiria ambayo yalikuwa yakitumia Stendi ya zamani katika upakiaji na ushushaji wa abiria kutoka mjini kwenda katika eneo la Sagara ambalo lina ukubwa wa ekari 10 kwa ajili kuondoa msongamano katikati ya Mji huo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Halmashauri hiyo kufanikiwa kuweka miundo mbinu yenye thamani ya milioni 277.7 ambayo imesaidia katika hatua za awali za ufunguzi wa Stendi hiyo mpya ambayo itatoa huduma kwa magari ya abiria yanayopitia Mkoani Tabora na yake kutoka Mkoani humo.

Kauli hiyo ilitolewa jana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Nzega Philemon Magesa wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa Stendi hiyo iliyopo kando kando ya barabara kuu ya kwenda Shinyanga na Singida na maeneo mengine .

Alisema kwa kuwa Nzega iko kwenye ni njia panda eneo la Stendi ya mabasi ya zamani lilikuwa dogo na kulifanya kushinwa kuhimili wingi wa mabasi yaliyokuwa yakitoka nje ya Nchi na yale ya mikoa mbalimbali ambayo yalikuwa yakipitia Nzega na kusababisha msongamano na karaha kwa wasafiri na watumiaji wengine wa barabara.

Magesa alisema baada ya kuona hawawezi kukamilisha kazi zote kwa wakati mmoja waliamua kutumia fedha hizo kidogo kuanza na hatua za awali za kujenga jengo la kupumzikia abiria, Kituo Kiodogo cha Polisi, vibanda sita(6) vya kukatia tiketi, vyoo na ofisi, vibanda vya askari , Mamlaka ya Usafirishaji Tanzania(SUMATRA) na kulipa fidia wananchi waliokuwa katika eneo ilipojengwa Stendi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kazi nyingine ilikuwa ni kujenga uzio wa nyaya kuzunguka eneo la stendi,vibanda vya askari wa usalama barabarani, wakusanyaji mapato ya Halmashauri, kuweka taa za mwanga wa jua katika Ofisi na kwa ajili ya kuimarisha usalama nyakati za usiku .

Alisema gharama halisi ya kujenga hadi Stendi hiyo hadi kukamilika kwa kiwango cha juu kulingana na michoro ya ubunifu zinahitajika bilioni 7.7 ambapo kwa kutumia mapato ya Halmashauri hiyo ya ndani itawachukua miaka 10 ili kukamilisha ujenzi wake.

Magesa alisema kutokana kuhitajika fedha nyingi kukamilisha ujenzi wote walifanya uamuzi wa kuandika andiko maalumu kwa ajili ya mradi huo na kuuwasilisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo limeshawalishwa Wizara ya Fedha na Mipango ili waweze kupatiwa fedha za kukamilisha ujenzi wa mradi huo mapema.

Alisema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake kutaweza kusaidia Halmashauri hiyo kuongeza uwezo wa kukusanya mapato yake na ndeani na kuiwezesha katika kuelekea katika kujitegemea.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema wako katika hatua ya mwisho ya kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 15 kwa ajili ya kuweka maegesho ya magari ya mizigo ambalo nalo litasaidia kuingizia Halmashauri hiyo mapato yake ya ndani.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alilitaka Jeshi la Polisi Wilaya ya Nzega kushirikiana na Halmashauri hiyo kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika eneo hilo saa zote kwa kuwa ni jipya na liko mbali na makazi ya watu upo uwezekano watu ambao sio wema wakatumia nafasi hiyo kutenda uovu wa aina mbalimbali ikiwemo kuwapora abiria.

Alisema uhalifu wa aina yoyote ukitokea unaweza kuwakatisha tamaa wasafiri na wawekezaji ambao wangependa kutumia Stendi hiyo jambo ambalo linaweza kusababisha mapato ya Halmashauri kupungua kutokana na wasafiri kuwa na hofu .Aidha Mkuu wa Mkoa alioutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha huduma mbalimbali kama vile vyoo na kuweka taka zinakuwepo ili kuepuka magonjwa ya mlipuko wakati wa masika.

Naye abiria kutoka Yelayela wilayani Urambo kwenda Dar es salaam Mashaka Maganga aliipongeza Halmashauri hiyo kwa uamuzi wake wa kuihamisha Stendi kutoka mjini kuiweka eneo la Sagara kwani limesaidia kuondoa msongano sio tu magari hata abiria walikuwa wanapata shida kutoka na kuwa wengi katika eneo dogo.
 Baadhi ya Wafanyabiashara ndogondogo wakiendelea na shughuli zao jana  baada ya uzinduzi wa Kituo Kipya cha Mabasi cha Sagara kwenye Halmashauri ya Mji Nzega.
 Magari ya abiria kutoka sehemu mbalimbali yakipita katika Geti la Ukaguzi na malipo ya ushuru katika Kituo Kipya cha Mabasi cha Sagara kwenye Halmashauri ya Mji Nzega baada ya kuzinduliwa jana.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Nzega Philemon Magesa (mbele waliosimama), Mkuu wa Wilaya ya Nzega Godfrey Ngupula(wa pili waliosimama) na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (wa tatu waliosimama) na abira wengine wakiwa katika gari la abiria ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Kituo Kipya cha Mabasi cha Sagara katika Halmashauri ya Mji Nzega jana.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (mbele) akiwaongoza viongozi mbalimbali kutembelea Kibanda cha Ukaguzi wa Magari na kile cha Malipo ya Ushuru wakati wa uzinduzi wa Kituo Kipya cha Mabasi cha Sagara katika Halmashauri ya Mji Nzega jana.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Nzega Philemon Magesa (katikati walio mbele) akitoa maelezo mafupi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey (kulia walio mbele)mara baada ya uzinduzi jana wa Kituo Kipya ch Mabasi ya Abiria cha Sagara cha Halmashauri hiyo. Kushoto mbele ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Godfrey Ngupula.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad