NAONA MBOWE NAYE AMEAMUA KUWAFUATA WAITARA, MTATIRO ! - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

NAONA MBOWE NAYE AMEAMUA KUWAFUATA WAITARA, MTATIRO !

Share This
Na Said Mwishehe

SITAKI kuamini hiki...yaani hata Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe naye ameamua kuhamia CCM.

Ni nini kimetokea kwa Mbowe?Hivi kweli ameamua kwa ridhaa yake kujiunga CCM? Amenunuliwa?Ujue unaposikia Mbowe naye ameamua kujiunga CCM lazima kuna maswali ya msingi ambayo utajiuliza tu.

Au Mbowe ameamua kuondoka Chadema kutokana na kulalamikiwa na baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa anaendesha chama kwa maamuzi yake.Hili sidhani.Haiwezi kuwasababu ya kumfanya Mbowe kujiunga na CCM.

Au ameamua kuondoka Chadema na kuachana na nafasi zake zote alizonazo kwasababu tu ya kuchoshwa na tuhuma ambazo zinaelekezwa kwake kila kukicha na wale wanaohama kuwa hataki kuachia Uenyekiti kwa wengine.Hata hivyo kwa kuwa Mbowe yupo nitaelewa tu sababu zilizomfanya naye aondoke Chadema na kwenda kujiunga na CCM.

Hata hivyo wakati hayo yakiendelea nikawa natafakari hivi ni kweli Mbowe hizi habari za kwamba ameondoka Chadema na kujiunga na CCM.Binafsi sawa nilishangaa kusikia Mbowe kaondoka Chadema lakini kwa hali ya kisiasa nchini inavyoendelea nikaona huenda anaweza kuwa na uamuzi huo na ni haki yake kimsingi.

Wakati bado naendelea kutafakari sababu za Mbowe kuondoka Chadema ...napigiwa simu na marafiki zangu wengine wakiniambia Mbowe ameitisha mkutano anazungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake.Habari za Mbowe kuamua kuitisha mkutano zikaanza kunipa picha na kuanza kuamini huenda ikawa kweli.

Nikaona isiwe tabu acha niende nikamsikilize angalau niwe na cha kuwaambia watanzania kupitia chombo changu cha habari ninachofanyia kazi.Nikauliza muda wa mkutano nikaambiwa. Sikutaka kupoteza muda nikachukua 'not book' yangu na kalamu na kwa kuhakikisha napata tukio vizuri nikabeba na kamera kwa ajili ya picha.

Nikaingia kwenye daladala huyo hadi nyumbani kwa Mbowe.Nilipofika nikakutuna na waandishi wengine wengi tena wengi kweli kuliko hata wale waliojitokeza wakati ule anazungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.Muda ulipowadia Mbowe akaingia eneo la mkutano.Wakati anaingia kwenye eneo la mkutano hakuwa na kiongozi yoyote maana aliingia peke yake tu.

Hata hivyo usoni akawa anaonekana ni mwenye furaha na bashasha kama vile mtu ambaye alikuwa anahitaji jambo fulani kwa muda mrefu na hatimaye amelipata.Nikaona ngoja nikae vizuri kwanza nimsikilize Mbowe .Ni kiongozi mwenye heshima kubwa katika siasa za Tanzania.Kama kawaida yake hakutaka kupoteza muda kwani baada yakuwasalimia waandishi wa habari moja kwa moja akaanza kuzungumza.

Mbowe hakuwa na papara wakati anazungumza .Akaanza na historia ya Chadema tangu ilipoanzishwa huku akitumia nafasi hiyo kuelezea namna ambavyo amekipigania chama hicho.Mbowe akaelezea namna ambavyo Chadema imepita magumu mengi na namna ambavyo walifanikiwa kuyavuka.Hakusita kuzungumzia walivyopambana kuvuna makada wa CCM kwa nyakati tofauti na hasa kuelekea uchaguzi mkuu uliopita ambapo waliamua kubadili gia angani na kumchukua Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.

Pia akaeleza walivyomchukua pia aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu Frederick Sumaye pamoja na makada wengine kibao wa CCM akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja.Wakati Mbowe anazungumza binafsi nikawa makini kumsikiliza anataka kutuambia nini leo.Nikawaangalia waandishi wengine nao kila mmoja yupo makini kumsikiliza.

Baada ya kukizungumzia chama chake Mbowe akaanza kuzungumzia hama hama ya wabunge wa upinzani na madiwani kwenda CCM.Hapa nikashtuka na kuanza kujiuliza anataka kueleza nini? Hata hivyo nikaona acha nijipe muda na kuongeza umakini.Mbowe hakusita kumzungumzia aliyekuwa Mbunge wa Ukonga kupitia Chadema Mwita Waitara.Akaonesha kukasirishwa na tuhuma ambazo Waitara amezitoa dhidi yake.

Hata hivyo baada ya maelezo mengi Mbowe naye akaanza kueleza namna ambavyo kasi ya Rais inavyomsukuma naye kushirikiana naye katika kuleta maendeleo ya Watanzania.Nikaanza kujiuliza kimoyo moyo ni kweli huyu Mbowe ninayemjua leo hii naye anasifu kazi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli.

Wakati Mbowe anaendelea kuzungumza na hasa kutokana na maendeleo akawa anatoa mifano pia ya miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa fly over pale Tazara jijini Dar es Salaam.Mbowe akaanza kuzungumzia kazi nzuri ambayo Rais ameifanya katika kukomesha rushwa, kurudisha nidhamu mahala pa kazi, kukomesha ufisadi na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Waandishi kila mmoja akawa ananong'ona kwa chini chini Mbowe leo amepatwa na nini.Wakati wanajiuliza Mbowe ndipo akaomba waandishi kumsikiliza kwa umakini anachotaka kusema baada ya maelezo yote.Nakumbuka alisema hivi "Kwa ridhaa yangu mwenyewe bila kushawishiwa na mtu nami nimeamua kujiunga CCM.Nataka kushirikiana na Serikali ya CCM kuleta maendeleo kwani Rais anafanya kazi nzuri na nijukumu la Watanzania kumuunga mkono kwa kuwa upande wake."

Hakuishia hapo akasema anajua Waitara tayari amejiunga CCM , hivyo si dhabi naye kwenda huko huko aliko Waitara.Pia akasema anafahamu na Julius Mtatiro naye ameshakwenda CCM kwa ajili ya kushiriki kikamilifu kuleta maendeleo ya Watanzania.

Maneno hayo ya Mbowe yakaanza kunifanya niwaze ...nikawaaaza weee.nikawaaaaza sana tu.Nikawa nawaza sasa kama Mbowe ameamua kujiunga CCM hivi waliobakia huko wanasubiri nini.Pamoja na Mbowe kutangaza kujiunga CCM bado kwangu niliendelea kuwaza .Hata hivyo wakati naendelea kutafakari siasa za upinzani nikajikuta napiga kelele kwa sauti kubwa.

Sauti ya mshangao.Si ndio nikakurupuka.Niko wapi?Mbona siko nyumbani kwa Mbowe? Mbona huu ni usiku? Hili la Mbowe kuhama nimelitoa wapi?

Wakati najiuliza maswali yote haya nikabaini kumbe nilikuwa naota tu.Ilikuwa ndoto, tena ni ndoto ya kipuuzi na hauna sababu ya kuiamini.Siunajua tena mambo ya ndoto.Kumbe koote huko nilikuwa naota?Usingizi baada ya kwisha kabisa na kubaki mwenye akili timamu nikajiridhisha kumbe Mbowe bado yupo Chadema.Kumbe Mbowe bado ni Mwenyekiti wa Chadema na bado mbunge wa Hai.

Ninachojilaumu hii ndoto imenipotezea muda wangu na kusumbua tu usingizi bila sababu ya msingi.Nikiri katika kipindi hiki ambacho wanasiasa wengi wa upinzani wameamua kurudi CCM kwa ridhaa zao muda mwingi nimekuwa nikitafakari hatma ya upinzani.

Huenda kutafakari huko kumenifanya niote hiyo ndoto ambayo kimsing ni ya kijinga.Na kwa kuwa ni ndoto achana nayo .Acha tusubiri.Wewe unakasirika kitu gani?Unaikasirikia hata ndoto ...utakuwa wa ajabu sana.

Acha maisha yaendelee ila leo sitalala kabisa maana naweza kuota na Lowassa naye karudi CCM.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad