BENKI YA KILIMO NCHINI YAWAHIMIZA WATANZANIA KUJIKITA KWENYE KILIMO - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

BENKI YA KILIMO NCHINI YAWAHIMIZA WATANZANIA KUJIKITA KWENYE KILIMO

Share This
Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo (TADB) Bw. Japheth Justine akizungumza mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James wakati wa kukabidhi Matrekta kwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine SUA cha Mkoani Morogoro leo kwenye kiwanda cha TEMCO Kibaha Mkoani Pwani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo (TADB) Bw. Japheth Justine mwenye miwani nyuma pamoja na viongozi wengine mara baada ya makabidhiano hayo yaliyofanyika mjini Kibaha.Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KAIMU Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo(TADB) Japheth Justine ameshauri Watanzania kujikita kwenye kilimo kwani kinalipa huku akifafanua wao wapo tayari kutoa fedha asilimia 80 kwa wanaohitaji kukopa matrekta na asilimia 20 iliyobaki itatolewa na mnunuzi.

Akizungumza leo wilayani Kibaha mkoani Pwani mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James , Mkurugenzi wa TADB Justine amefafanua kikubwa ambacho wanataka kuona ni mkulima kufanikiwa kupitia mazao yake na ndilo miongoni mwa jukumu lao.

Akifafanua zaidi Justine amesema wameshatoa mkopo wa Sh.bilioni 41.1 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo na wapo kwenye mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma na siku za karibuni watafungua tawi lingine mkoani Mbeya na lengo lao ni kuwafikia wananchi kokote walipo

Pia amesema wameshafanya makubaliano na Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) kwa lengo la kusaidia wale wanaonunua matrekta kwamba benki ya kilimo itaingiza asilimia 80 ya mkopo na mnunuzi atatoa asilimia 20.Ameongeza kwamba wakulima wamefanya vizuri kwenye zao la pamba huku akielezea lengo lao ni kuchoche hamasa kwenye kilimo na kubwa zaidi ni kumuondoa mkulima kwenye jembe la mkono.

“Pale ambapo tutafanikiwa kumtoa mkulima kwenye jembe la mkono na kumpa mashine ambazo zitamsaidia kuongeza tija na kumpa faida hicho ndicho ambacho tunakihitaji.“Kilimo au mkulima ni muwekezaji na hivyo tunataka kuona mkulima anapata faida .Hivyo kwa wakulima waliokuwa kwenye bodi ya pamba watapa mkopo wa asilimia 80,”amesema.

Ameongeza wataanza na matrekta 500 ambayo hiyo itafanyika muda si mrefu kwa kuwapa wakulima waliofanya vema kwenye kilimo cha pamba.Justine amesema mpango wao mkubwa ni kwenda kuziambia benki za biashara kuingiza asilimia 50 na wao wataweka asilimia 50 katika kumkopesha mkulima.

Pia amesema wanaishukuru Serikali kwa kuzindua mpango wa pili kwenye sekta ya kilimo na watahakikisha wanafanikisha malengo ya Serikali.Amesema benki ya kilimo itahakikisha inawakopesha wakulima kwa bei nafuu na kusisitiza kuwa kilimo kinalipa na hivyo Watanzania wajikite kwenye kilimo.

Amesisitiza wameanza na wakulima wa pamba katika kutoa hiyo asilimia 80 na iwapo mpango huo utafanikiwa basi watakwenda kwenye maeneo mengine.Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango , James amempongeza Mkurugenzi huyo wa benki ya kilimo kwani tangu alipoteuliwa na Rais amesimamia mambo mengi aliyoagizwa kuyafanya.

Amesema kwa sasa benki hiyo ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wakulima nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad