UTENDAJI, SIASA ZA JPM ZALETA MKUTANO WA CPC TANZANIA - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

UTENDAJI, SIASA ZA JPM ZALETA MKUTANO WA CPC TANZANIA

Share This
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii


NAOMBA kutumia nafasi hii kwanza kabisa kutoa salamu kwa Watanzania wote.

Pili naomba nitoe salamu zangu za unyenyekevu kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Dk. John Magufuli.

Baada ya salamu hizo pia naomba nitumie nafasi hii kupongeza jitihada za Rais Magufuli katika kuwatumikia Watanzania wote na kubwa zaidi harakati zake za kuhakikisha tunapiga hatua.

Pia, ahsante Rais Magufuli kwa jitihada zako ambazo umekuwa ukizifanya katika kuhakikisha tunakuwa nchi ya kujitegemea kupitia rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujaalia katika nchi yetu.

Ila Rais nikunong'oneze kuwa ujio wa Dreamliner umenikosha sana kama si kunifurahisha. Ni juzi tu macho ya Watanzania yameshuhudia ujio wa ndege hiyo kubwa na ya kisasa.Inahitaji uwe na akili za wendawazimu ili uweze kukosoa ujio wa ndege hiyo. Pia, inahitaji kujitoa ufahamu ili upate nafasi ya kuupotosha umma kuwa ujio wa Dreamliner haustahili.

Kwa mwenye akili timamu na anayejua nini maana ya maendeleo ataungana  na watanzania wote kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wa kununua ndege kwa lengo la kuliboresha Shirika la Ndege la ATCL. Ahsante Rais.Baada ya utangulizi huo nielezee hivi leo hii nimeamua kujikita katika kuzungumzia urafiki kati ya nchi za Tanzania na China. 

Nazungumzia urafiki huo nikitambua kuwa Julai 17 mpaka Julai 18 mwaka huu Tanzania inapokea ugeni mkubwa ambao utahudhuria mkutano wa kidunia ambao unahusisha vyama vya kisiasa ambavyo vilikuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

Mkutano huo utafanyika jijini Dar es Saalam. Ni mkutano ambao umeandaliwa na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Ni mkutano  mkubwa haswaa. Yaani mkubwa naomba unielewe. Kwa msisitizo niandike kwa herufi kubwa kwamba NI MKUTANO MKUBWA SANA.

Hivyo kabla ya kuzungumzia mkutano huo niombe nizungumzie alau kwa uchache urafiki wa miaka mingi kati ya Tanzania na China. Kwa kukumbusha tu uhusiano kati ya Tanzania na China umeleta faida kubwa za kimaendeleo.

Kupitia urafiki huo kuna mambo mengi Watanzania tumenufaika nayo na wao China yapo mambo mengi ambayo wamenufaika nayo kutoka na urafiki wao na sisi.Uhusiano wa China na Tanzania umekuwa na mafanikio makubwa ya kuziunganisha nchi hizo katika kusaidiana katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Kila mmoja anaweza kuelezea namna anavyoona inafaa kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili lakini jambo la msingi na la kuzingatiwa Tanzania na China wamekuwa na urafiki wa muda mrefu uliofanikisha mambo mengi kufanyika.

Kumbukumbu zinaonesha baada tu ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, wataalam wa kilimo, ujenzi na madini walifika kusaidia wenzao wa Tanzania katika fani zao.

Baadae, mamia kwa maelfu ya wafanyakazi wa reli walifika kujenga kilomita 1,860 za Reli ya Tanzania hadi Zambia, ambayo inajulikana zaidi kama TAZARA.

Unaweza kuona urafiki wa nchi hizo mbili ulivyo na pengine unaweza usifananishwe na nchi yoyote ile ingawa nikiri Tanzania inao uhusiano mzuri na nchi mbalimbali duniani.


Wakati kukiwa na uhusiano mzuri kati ya China na Tanzania pia umenogeshwa zaidi na uhusiano ulitokuka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Vyama hivyo vimekuwa na urafiki wa muda mrefu na urafiki wao umesababisha mambo mengi kuonekana kuingilia hasa katika mfumo wa utendaji wake.

Ni vyama ambavyo vimekuwa na misimamo hasa linapokuja suala la usawa na haki kwa wote. Ni vyama ambavyo kila kimoja kwa nafasi yake kinapambana kujenga hali bora za watu wake. 

Itoshe kusema kuna uhusiano mkubwa kati ya CCM na CPC katika kutekeleza majukumu yao. 

Ni jambo la kawaida viongozi wa CPC kutembelea ofisi za CCM na hivyo hivyo kwa viongozi wa CCM kutembelea ofisi za CPC nchini China tena kwa raha zao. Hakika ni urafiki ambao unaakisi udugu ndani yake.

Nimegusia kidogo kuhusu mkutano wa vyama vilivyoshiriki kukomboa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika. Iko hivi China imeamua kuichagua tena Tanzania kwa ajili ya kufanyika mkutano huo mkubwa wa kidunia ambao utahusisha vyama vyote ambavyo vilikuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

Kama nilivyotangulia kueleza awali mkutano huo unatarajiwa kufanyika Julai 17 mpaka Julai 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Hivyo vyama vyote ambavyo vilishiriki katika kukomboa nchi za ukanda huo watakuwa jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha CPC cha nchini China kwa kushirikiana na CCM.

Na hivyo kutakuwa na ugeni mkubwa wa viongozi wa kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika. Wageni zaidi 130 kutoka nje ya Afrika watahuhlshuria mkutano

Mwenyeji wa mkutano huo ni  Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli.

Kwa lugha ya mjini ni kwamba Julai 17 mpaka Julai 18 dunia itaelekeza macho yake nchini Tanzania. 

Kikubwa itataka kujua nini kimejadiliwa na hasa ukizingatia China ni moja ya Taifa ambalo lipo juu kiuchumi.

Binafsi kuna mambo kadhaa nayatarajia kuona yakitokea kwenye mkutano huo wa vyama vya ukombozi wakiongozwa na CCM.

Naamini mbali ya kujadili kwa kina masuala ya vyama hivyo na mchango wao pia itakuwa nafasi nzuri ya kujadili namna ya kuendeleza nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.

Ndio ukweli huo maana vyama hivyo vinamchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya nchi zao.

Nani anabisha kuhusu mchango wa CCM katika ustawi wa maendeleo ya nchi. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli imeendeleea kutekeleza Ilani ya CCM. 
P
Rais Magufuli anaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.Utendaji wake ndani ya CCM huenda nayo umekuwa chachu kwa China kuamua mkutano huo ufanyike katika aridhi ya Tanzania.

Kasi yake katika kuleta maendeleo ni kubwa na inaleta matumaini kuwa Tanzania tunakwenda kuwa Taifa kubwa katika medani za kimaendeleo.

Kupitia rasilimali zilizopo Rais Magufuli anafanya mambo makubwa na wakati mwingine unajiuliza anawezaje? Lakini anaongozwa na dhamira ya kweli ya kuona Taifa lake linapiga hatua na hatimaye tunashuhudia mambo makubwa yanafanyika.

Achilia mbali suala la elimu bure ambalo Serikali ya CCM inatekeleza pia kupitia Rais Magufuli kuna miradi mikubwa ya ujenzi inaendelea kila kona ya nchi yetu.

Unapomuangalia Rais Magufuli unamuona namna ambavyo anaona kabisa Tanzania kuwa na maendeleo ni jambo ambalo linawezekana. Ukimtazama usoni unamuona namna ambavyo anafikiria zaidi nchi yake katika kuelekea uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati. Kwa namna ambavyo anakwenda kikubwa ni kumuombea kwa Mungu.

Unajua kwa nini nimeweka kando kidogo kuzungumzia mkutano wa vyama hivyo ni kwa sababu naona kabisa viongozi wa vyama hivyo ambavyo vitakuwepo nchini kwenye mkutano huo watatumia nafasi hiyo kumpkongeza Rais Magufuli kwa kazi ambayo anaifanya tangu ameingia madarakani.

Kwa ujinga wangu au ufinyu wa akili nilionao kuna mambo ambayo nayaona kabisa Rais Magufuli anayafanya kwa ajili ya nchi yeke kumbe kuna mataifa mengine makubwa yanaiga.

Hata hivyo kuiga jambo jema si dhambi. Kwa mfano wakati Rais Magufuli moja ya mkakati wake ni kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya mawasiliano inayounganisha Tanzania na nchi nyingine iliyo imara na ya uhakika Rais wa China naye amekuja na mkakati wa kuiunganisha china na nchi nyingine duniani.

Huwa nakaa na kisha natafakari namna ambavyo Rais Magufuli ambavyo anachukia rushwa .Namna ambavyo anataka nchi yake ipige hatua kwa kasi kubwa. 

Namna ambavyo Rais Magufuli anasimamia uwajibikaji na utumishi wa umma wenye uadilifu.

Naangalia namna ambavyo Rais Magufuli ameamua kuleta mageuzi ya kimaendeleo kwa nchi yake. 

Ndivyo hivyo hvyo ambavyo pia namuona Rais wa China naye anapita njia ambayo Rais Magufuli ameamua kuipitia kwa ajili ya maendeleo.

Nikiri China ni taifa ambalo ndani ya miaka 73 limefanikiwa kuwa taifa kubwa na lenye uchumi imara duniani. Ndivyo ambavyo namuona Rais Magufuli ambavyo anataka kutumia muda mfupi kuipeleka  Tanzania kuwa taifa lenye uchumi imara. Inawezakana kikubwa ni kumuombea afya njema.

Tofauti iliyopo kati ya Rais Magufuli na Rais Xi Jinping ni kwamba China wamemua Rais wao akae madarakani hadi mwenyewe atakaposema basi.

Lakini kwa Rais Magufuli kwa kuheshimu Katiba amekuwa akieleza mara kwa mara muda wake kwa mujibu wa Katiba ukimalizika basi atakwenda kupumzika.

Ukiondoa tofauti hiyo huwa nakaa na kuona kama vile ndani ya kichwa cha Rais Magufuli kwa maana ya mipango aliyonayo kwa nchi yake haina tofauti kabisa na mipango ambayo Rais wa China anayo kwa watu wake. 

Ni kama vile namuona Rais wa China katika kichwa cha Rais Magufuli.

Nihitimishe kwa kuelezea msingi wa kueleza yooote hayo ni kwamba Julai 17 mpaka Julai 18 mwaka huu Tanzania inapokea ugeni mzito kwa ajili ya mkutano huo.

 Msemaji wa CCM Humphrey Polepole tayari ameulezea vema mkutano huo.Bado naamini Utendaji kazi wa Rais Magufuli umechangia kumfanya Katibu Mkuu wa CPC na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China kuamua mkutano huo kufanyika nchini Tanzania.

Nikushukuru kwa kunisoma kuanzia mwanzo hadi hapa nilipoishia. Ahsante kwa uvumilivu wako maana ni maelezo ya kutosha lakini yenye nia njema na hasa katika hili la urafiki kati ya Tanzania na China.

Pia ni kuhusu mkutano huo unaofanyika Julai 17 hadi Julai 18 mwaka huu. 

Maoni 0713833822
Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa katika mazungumzo na Mjumbe wa Kamati Kuu na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Mhe Guo Jinlong na ujumbe wake  walipowasili Ikulu jijini Dar es salaam Machi 22, 2017 
Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli akiongozana na Mjumbe wa Kamati Kuu na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Mhe Guo Jinlong  walipowasili Ikulu jijini Dar es salaam Machi 22, 2017.PICHA NA IKULU

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad