RPC ARUSHA ATAJA VIPAUMBELE VITANO KUELEKEA KUUSHINDA UHALIFU - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

RPC ARUSHA ATAJA VIPAUMBELE VITANO KUELEKEA KUUSHINDA UHALIFU

Share This
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia Kamanda wake wa mkoa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi, limetaja mambo matano ambayo yakifanyika basi kutakuwa na mafanikio zaidi katika kuushinda uhalifu.

Akizungumza katika mahojiano yaliyofanywa na Redio Sunrise ya Jijini hapa kupitia kipindi chake cha “Kwa ajili ya Nchi yako” kinachorushwa hewani kila siku ya Ijumaa kuanzia saa 9:00 Alasiri hadi saa 10:00, Kamanda Ng’anzi alisema, kwanza kabisa kila mwananchi anatakiwa ajue ana wajibu wa kutoa taarifa za matukio ya Uhalifu na Wahalifu zinatokea katika eneo lake.

Pili alisema ni lazima askari wa Jeshi hilo watoe huduma bora na kwa kiwango cha juu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza pindi wanapoeleza shida zao lakini pia kwenda haraka katika maeneo yaliyoripotiwa kutokea uhalifu.

Tatu alisema lazima kila askari adumishe na kuongeza kiwango cha nidhamu hali ambayo itasaidia baadhi ya wanaokwenda kinyume kutofanya kazi kwa mazoea na hivyo watafanya kazi kwa kufuata taratibu zilizopo.

Nne alisema askari watatakiwa kufanya kazi kwa kuheshimu Utu pamoja na kufuata Maadili ya kazi yao na tano kufanya kazi kwa Uweledi na Usasa ambapo askari atafanya kwa namna alivyofunzwa lakini pia kuendana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia na mwisho wa siku waone kwa jinsi gani wananchi mkoani hapa wanaridhishwa na utendaji wa Jeshi hilo.

Mbali na kutaja vipaumbele hivyo Kamanda Ng’anzi alisema Jeshi hilo litaendelea kutunza siri za watoa taarifa kwani ni sehemu ya miongoni mwa viapo vya kazi yao lakini pia aliwaeleza wananchi wenye mashaka juu ya kuvujishwa kwa siri zao wanaweza kuzitoa moja kwa moja kwa viongozi wa ngazi za juu.

“Kwa wenye mashaka juu ya taarifa zenu toeni kwangu au viongozi wa juu wa ngazi ya mkoa mfano RCO “Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa “, RTO “Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoa” na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa Polisi mkoa na kwa ngazi ya wilaya toeni taarifa kwa OCD “Mkuu wa Polisi wilaya au OC-CID “Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya”. Alisema Kamanda Ng’anzi.

Aidha Kamanda Ng’anzi alisema kwamba Jeshi hilo lina mkakati wa kutekeleza Progamu ya MUONGORIKA kwa kushirikiana na wadau ili waweze kuanzisha mashindano mbalimbali ya Michezo na Sanaa kwa vijana wanaoshinda vijiweni bila ajira hali ambayo itasaidia kuibua vipaji vyao vitakavyowawesha kujiendeleza na pengine kujikwamua kiuchumi huku wakiondokana na fikra za kujiingiza kwenye uhalifu.

Takwimu zinaonyesha kiwango cha matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa mkoani hapa kwa kipindi cha miezi sita mwaka huu zinaonekana kupata mafanikio makubwa ambapo matukio yalikuwa 654 tofauti na mwaka 2017 kipindi cha Januari hadi Juni ambapo kulikuwa na matukio 996 hivyo yalishuka kwa asilimia 20.7.
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad