RC KIGOMA ATOA MAAGIZO KWA WAKUU WA WILAYA, WAHANDISI KUUSIMAMIA MRADI WA MAJI MUHANGE - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

RC KIGOMA ATOA MAAGIZO KWA WAKUU WA WILAYA, WAHANDISI KUUSIMAMIA MRADI WA MAJI MUHANGE

Share This
Na Rhoda Ezekiel, Kigoma

MKUU wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Generali Mstaafu Emanueli Maganga amewaagiza wakuu wa wilaya za Kibondo na Kakonko pamoja na Wahandisi wa Wilaya hizo kuweka kambi katika Kata ya Muhange kuhakikisha wanasimamia mradi wa maji wa Muhange unatoa maji kwa wananchi ndani ya wiki mbili.

Kauli hiyo aliitoa wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi ya maji ndani ya Wilaya ya Kakonko ambapo amesikitishwa na kitendo cha mradi wa maji Muhange kutokamilika licha ya kwamba ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2012 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na ulitarajiwa kukamilika Desemba mwaka 2013.

Brigedia Maganga amesema ni jambo la kushangaza kuona wananchi wanaendelea kupata shida ya maji huku mradi ukiwa umefungwa kwa changamoto ndogondogo ambazo zinaweza kufanyiwa marekebisho na ukizingatia mradi huo unasimamiwa na Wilaya mbili na Wahandisi wawili.
Hivyo amewataka kutenga muda wa siku mbili kufika katika Kijiji cha Muhange kushirikiana na wananchi kukamilisha mapungufu ya mradi huo. 

"Ukiwa Mhandisi kazi yako ni kukaa sehemu ya mradi hadi mradi utakapo kamilika, kama mngekuja kukaa hapa changamoto hizi zisingejitokeza mme waachia wakandarasi wafanye mradi kwa kiwango cha chini, wananchi wanapampu maji yana ishia chini na haya wafikii na wananchi wanaendelea kuteseka", amesema Brigedia Maganga.

Ameongeza kuwa " Wakuu wote wa wilaya mbili kaeni na hii kamati ya watumia Maji na wataalamu wenu mje hapa na Jumuiya ya Watumia maji kama tatizo la mabomba mtafute maeneo yanayo vuja yafanyiwe ukarabati kama kuna tatizo la kisiasa litajulikana suala ni kwenye utendaji na utekelezaji mpaka maji yaende kwenye gati zote 24 wananchi wapate maji".

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya kakonko Kanali Hosea Ndagala alipokea maelekezo hayo na kuahidi kwenda kukaa pamoja na viongozi hao na kujadili mbadala wa kufanya haraka ilikuweza kukamirisha lengo la Serikali kufadhili miradi hiyo kwa wananchi .

Nae Mhandisi wa Wilaya ya Kibondo Michael Nguruwe amesema mradi huo ulikuwa ukisimamiwa na Wilaya hiyo na Mradi uliukaguliwa ,baada ya kukamilika Kwa mradi huo wakati wa kufanya majaribio mradi ulitoa maji kwa magati yote 24 na matatizo hayo yamejitokeza baada ya wananchi kuanza kutumia mradi huo.

Amesema mradi unapokuwa hautumiki kwa muda mrefu matanki yanakauka na miundombinu inaharibika hali hiyo inaweza kusababisha mabomba kupasuka na tanki kuanza kuvuja na aliomba wakae pamoja na wataalamu wa Wilaya ya kakonko kufanya marekebisho na kupita kila eneo ambalo linavuja.

Diwani wa Kata ya Muhange Ibrahimu Katunzi amesema ukweli ni kwamba maji wanapo yaruhusu kwenda kwa wananchi bomba zinapasuka, bomba zilizowekwa hazina ubora na wanapata hasara kwa kuwa maji yote yanaishia njiani na hayawafikii wananchi na kufanya jumuia ya watumia maji kushindwa kuendesha mradi huo.

Amesema kwenye chanzo kinachotakiwa kuruhusu maji kuingia kwenye tanki tanki halina chujio hivyo tope na vyura vinajaa kwenye tanki na hivyo kupelekea maji kusukumwa kwa kasi ndogo hali iliyo pelekea Wananchi wa Kata hiyo kuukataa mradi huo.Nao baadhi ya wananchi wa vijiji vya Muhange ya juu na chini Simoni Matulane na Anitha Ntibagomba wamesema wananchi wanapata shida kufuata maji wengine wanaamka saa 11 alfajiri kufuata maji baadhi mpaka wanaingilia mito iliyoko mipakani kwa ajili ya kufuata maji.

Wameiomba Serikali kuwasaidia wananchi kukamilisha mradi huo na utakapo kamilika wananchi wataendelea kuchangia na kuendesha miradi hiyo kama inavyo elezewa.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma pamoja na Mradi huo alitembelea miradi miwili ya Nyagwijima na Gwanumpu ambapo katika miradi hiyo yote alibaini baadhi ya mapungufu na kuahidi kupeleka mafuta katika mradi wa Nyagwijima kupampu maji na kuhakikisha kama maji yanawafikia Wananchi na Wataalamu wanatakiwa kurejebisha miradi hiyo wananchi waanze kupata huduma. 
MKUU wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Generali Mstaafu Emanueli Maganga akizungumza na baadhi ya viongozi wakiwemo wakuu wa wilaya za Kibondo na Kakonko pamoja na Wahandisi wa Wilaya hizo kuweka kambi katika Kata ya Muhange kuhakikisha wanasimamia mradi wa maji wa Muhange unatoa maji kwa wananchi ndani ya wiki mbili. 
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga katikati akioneshwa moja ya tanki la maji na Muhandisi Michael Nguruwe (kushoto),katika Katika Kata ya Nyagwijima wilayani Kakonko Mkoani Kigoma Jana,pichani kulia ni Muhandisi Elinatha Elisha

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad