Dk Kigwangalla aiagiza mikoa ya nyanda za Juu Kusini kuandaa mkakati wa pamoja kutangaza utalii - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

Dk Kigwangalla aiagiza mikoa ya nyanda za Juu Kusini kuandaa mkakati wa pamoja kutangaza utalii

Share This
Songwe: Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amezindua rasmi maonesho ya tatu ya Utalii Karibu Kusini 2018 yatakayofanyika mkoani Iringa Septemba 26 hadi 30 mwaka huu, huku akiwataka wakuu wa mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini kuandaa kalenda ya pamoja itakayoainisha matukio ya kimkakati katika kutangaza vivutio vya utalii katika mikoa hiyo.

Agizo hilo, Waziri Kigwangalla alilitoa mwishoni mwa wiki mkoani Songwe wakati akifunga rasmi maonesho ya utalii ya Kimondo yaliyoratibiwa kwa mafanikio makubwa na Mkoa huo huku pia akitumia fursa hiyo kuzindua rasmi Maonesho ya tatu ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanayohusisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupitia uratibu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii.Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni Iringa,Mbeya,Songwe,Ruvuma,Njombe,Katavi na Rukwa.

Akifafanua kuhusu agizo hilo, Dk Kigwangalla alisema ipo haja ya mikoa hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuhakikisha kwamba inabuni kalenda ya pamoja itakayoainisha matukio ya kiutalii kwa kila mkoa kisha kuyapanga katika mtiririko maalumu katika kipindi cha mwaka.

"Uwepo wa kalenda ya pamoja kwenye hili utawasaidia kufahamu mkoa upi unafanya nini kwa wakati fulani na hivyo kuwa rahisi kwa mikoa jirani kuweza kutoa ushirikiano kuhakikisha tukio hilo linakuwa kubwa zaidi bila muingiliano lakini pia itatoa fursa kwa walengwa ambao ni watalii na wadau wengine kufahamu kipi kinaendelea katika ukanda huu kwa wakati husika ili na wao pia waweze kujipanga'' alifafanua.

Alisema wingi wa vivutio vya utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ni sababu tosha kuweza kuvutia zaidi idadi kubwa ya watalii haswa kama mikoa hiyo itashirikiana kuvitangaza kwa pamoja kupitia matukio ya kimkakati yakiwemo maonesho ya Utalii Karibu Kusini ambayo yanafanyika mara ya tatu mkoani Iringa.

Akizungumzia agizo hilo la Dk Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alisema tayari mazungumzo yameanza miongoni mwa wakuu wa mikoa hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania(TTB) kuangalia namna bora ya kuandaa kalenda itayoainisha matukio makubwa ya kiutalii na kiuwekezaji kwa kila mkoa ili yaingizwe kwenye agenda ya pamoja.

"Mheshimiwa Waziri tayari tumeshaanza mazungumzo ya awali kuhusu uwepo wa kalenda ya pamoja ambapo kila mkoa utajipambanua kwa tukio lake kubwa litakalotambuliwa na mikoa mingine ndani ya kanda yetu ili kuongeza ushirikiano na hivyo kufanya kila tukio la mkoa husika miongoni mwetu liwe kubwa zaidi kwa kuwa litahusisha ushiriki wa pamoja.'' alisema

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William alisema katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini kwa mwaka huu mkoa huo umejipanga kushirikisha wadau kutoka mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na kutoa mwaliko kwa mikoa jirani ili kuhakikisha kwamba vivutio vyote vya utalii katika ukanda huo vinatangazwa kupitia maonesho hayo.

Akifafanua kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema pamoja na maonesho ya Utalii yatakayoanza Septemba 26 hadi 30 mwaka huu, pia maonesho hayo yatahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa gofu utakaoanza Julai 27 hadi 29 wilayani Mufindi.

"Kuanzia Septemba 26 hadi 30 ndio kutakuwa na mfululizo wa matukio mengi zaidi ikiwemo kongamano la Utalii Nyanda za Juu Kusini, Mbio za baiskeli, mashindano ya kumpata ya mlimbwende wa utalii kanda yetu, maonesho ya ngoma za asili na mwisho kabisa tutakuwa na nusu marathon itakayofanyika Septemba 30 ambayo ndio siku ya kufunga maonesho yetu,'' alifafanua.

Mratibu wa maonesho ya Utalii Karibu Kusini kutoka Kampuni ya Capital Plus Internantional (CPI) inayoshirikiana na Mkoa wa Iringa kuratibu maonesho hayo, Bw Clement Mshana alisema kwa mwaka huu yana maboresho makubwa ambapo mbali na kuongeza uhusishwaji wa sekta binafsi wao, kama waratibu wamejipanga kuhakikisha yanaandaliwa katika viwango vya kimataifa.

"Kwa kushirikiana na ofisi ya mkoa wa Iringa tumejipanga kuhakikisha kwamba maonesho ya mwaka huu yanakuwa na tofauti kubwa sana kuanzia kwenye ubora wa maandalizi, idadi ya washiriki si tu kutoka ndani ya nchi bali pia kutoka nje ya nchi na mwisho kabisa kuhakikisha kila tukio la kimchezo kwenye maonyesho haya si tu linafana bali pia linaleta tija tunayohitaji katika kutangaza utalii wa Nyanda za juu Kusini,'' alisema.Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanalenga kutangaza vivutio pamoja na fursa za kitalii katika mikoa hiyo huku yakiwa na kauli mbiu "Utalii ni Nguzo ya Uchumi wa Viwanda''.
 Baada ya uzinduzi huo ikawa  ni furaha tupu!
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla akikata utepe kuashiria uzinduzi wa maonesho ya tatu ya Utalii Karibu Kusini 2018 yatakayofanyika Septemba 26 hadi 26 mwaka huu mkoani Iringa wakati wa hafla ya ufungaji wa maonesho ya Utalii ya Kimondo yaliyohitimishwa  mkoani Songwe mwisho wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga ( wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa (kulia kwa waziri Kigwangalla) na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw Richard Kasesela (kushoto).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad