WAHANDISI CHANGAMKIENI UWEKEZAJI WA VIWANDA-MWIJAGE - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

WAHANDISI CHANGAMKIENI UWEKEZAJI WA VIWANDA-MWIJAGE

Share This
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amewataka wahandisi nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji katika viwanda nchini ili kuiwezesha Serikali kufikia lengo la uchumi wa kati na jumuishi ifikapo 2025.

Akifungua kongamano la siku moja la wahandisi kuhusu mchango wa Wahandisi katika Sekta ya viwanda jijini Dodoma leo, Mhe Mwijage amesema mchango wa wahandisi ni muhimu sana katika kipindi hiki ili kuwezesha taifa kufikia uchumi wa kati wenye uwiano kati ya pato la nchi na uchumi wa mwananchi.

“Tumejipanga kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na hivyo kugusa uchumi wa wananchi wengi” amesema Mhe. Mwijage.

Amesema uwekezaji katika viwanda vya sukari, mafuta na vifaa vya ujenzi ambavyo vyote malighafi zake zinapatikana nchini, utawezesha idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania kupata ajira na hivyo kufikia lengo la Taifa la uchumi wa kipato cha kati. Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Nchini (ERB), Eng. Profesa Ninatubu Lema ameiomba Serikali kuthubutu kuwaamini wahandisi wazalendo kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hapa nchini.

Prof. Lema amesema wahandisi wako tayari hata kupewa sehemu kidogo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (Standard Gauge), ili nao waweke alama ya uzalendo katika mradi huo mkubwa unaotekelezwa nchini. “Tunapoadhimisha miaka 50 ya ERB tuko wahandisi tuliosajiliwa zaidi ya Elfu 21 tunaweza kufanya kitu kama alama kwa taifa na vizazi vijavyo”, amesema Prof. Lema.

Amewataka wahandisi kutathmini namna gani wanaweza kuendeleza kilimo na viwanda nchini ili kuweza kubadili uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla katika miaka ijayo.

Kaimu Msajili wa ERB, Eng. Patrick Barozi amesema kongamano la wahandisi kuhusu uchumi wa viwanda ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya wahandisi yanayofanyika katika sekta mbalimbali za kihandisi yatakayofikia kilele chake mwezi Septemba mwaka huu yakiwa na lengo la kuwaweka wadau wa uhandisi pamoja kutafakari na kuhamasishana kuhusu namna bora ya kuendeleleza taaluma ya uhandisi kukuza uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja.

Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (kulia) akimweleza jambo Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Nchini (ERB) Eng. Profesa. Ninatubu Lema kabla ya kufungua kongamano la siku moja la wahandisi kuhusu mchango wa Wahandisi katika Sekta ya viwanda jijini Dodoma leo.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akisisitiza jambo wakati akifungua kongamano la siku moja la wahandisi (hawapo pichani) lililowakutanisha kujadili kuhusu mchango wa Wahandisi katika Sekta ya viwanda jijini Dodoma leo. Kulia ni Kaimu Msajili wa Wahandisi, Eng. Patrick Barozi.
Sehemu ya wahandisi wakimsikiliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku moja la wahandisi kuhusu mchango wa Wahandisi katika Sekta ya viwanda jijini Dodoma leo.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (kulia) akifurahia jambo na wahandisi mara baada ya kufungua kongamano la siku moja la wahandisi kuhusu mchango wa Wahandisi katika Sekta ya viwanda jijini Dodoma leo.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad