Tanzania inahitaji maonyesho ya kitalii katika kila ukanda - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

Tanzania inahitaji maonyesho ya kitalii katika kila ukanda

Share This

Na Jumia Travel Tanzania

Jumia Travel ilibahatika kuhudhuria maonyesho ya utalii ya KARIBU KILIFAIR 2018 yaliyofanyika kuanzia Juni 1 mpaka Juni 3 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.


Haya ni miongoni mwa maonyesho makubwa ya Utalii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati ambapo zaidi ya washiriki 350 walishiriki kuonyesha bidhaa na huduma zao, zaidi ya mawakala 300 wa ndani na kimataifa walikaribishwa, pamoja na takribani wageni 4000 walihudhuria ndani ya siku tatu za maonyesho.
Ni dhahiri kwamba kuendelea kufanyika kwa maonyesho haya kila mwaka kunazidi kukuza vivutio vya kitalii na watalii kwa ujumla nchini. Tanzania imebarikiwa na vivutio lukuki vya kitalii kwa upande wa nyanda za Kaskazini vikiwemo Mlima Kilimanjaro (mlima mrefu zaidi barani Afrika) na Hifadhi za Kitaifa za Mbuga za Wanyama (Arusha, Mkomazi, Ziwa Manyara, Serengeti, na Tarangire). 

Kufanyika kwa maonyesho kadhaa ya kitalii katika ukanda huo hususani Kilimanjaro na Arusha kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuvitangaza vivutio vilivyopo maeneo yale, kukuza uwekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na kuneemesha wananchi kwa ujumla. 

Licha ya kuwepo kwa vivutio vya kitalii pia miundombinu katika mikoa ya Kaskazini ni rafiki kwa watalii kufika kwa urahisi. Ukiachana na uwepo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ambao ndio kiungo kikuu cha watalii wanaofikia jijini Dar es Salaam na nchi jirani lakini pia kuna barabara nzuri za lami, hoteli nyingi zinazokidhi viwango vya kitalii, mawakala wa shughuli za kitalii pamoja na hali ya hewa nzuri inayowapendeza watalii wa aina mbalimbali.
Umeshawahi kujiuliza ingekuwaje endepo kila ukanda nchini Tanzania ungekuwa na onyesho angalau moja kwa mwaka? 

Tanzania inayo mikoa takribani 30 kwa sasa ukijumuisha pamoja na ya Visiwani Zanzibar. Katika upande wa shughuli za kitalii Tanzania bara imegawanywa katika kanda nne ambazo ni Ukanda wa Kaskazini - unaoundwa na Hifadhi za Taifa za Mbuga za Wanyama (Arusha, Mkomazi, Ziwa Manyara, Serengeti, Tarangire na Mlima Kilimanjaro); Ukanda wa Magharibi - unaoundwa na Hifadhi za Taifa za Mbuga za Wanyama (Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane); Ukanda wa Kusini - unaoundwa na Hifadhi za Taifa za Mbuga za Wanyama (Kitulo, Mikumi, Ruaha na Udzungwa) na Ukanda wa Mashariki - unaoundwa na Hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Wanyama ya Saadani. 

Tayari Ukanda wa Kaskazini unawakilishwa vema na maoinyesho ya KARIBU KILIFAIR, ambapo kuanzia mwaka huu wametangaza rasmi kuwa yataanza kufanyika kwa kupokezana. Mwaka 2018 yamefanyika Moshi, Kilimanjaro na mwakani 2019 yatafanyika mkoani Arusha.

Kwa upande wa Ukanda wa Mashariki, kuna maonyesho ya S!TE (Swahili International Tourism Expo) ambayo huandaliwa na Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB) kila mwaka ifikapo mwezi Oktoba. Kwa mwaka huu maonyesho haya yatafanyika kuanzia Oktoba 12 mpaka 14 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Jiji hili ni mashuhuri kwa shughuli za kibiashara nchini Tanzania na kwa asilimia kubwa ndipo shughuli mbalimbali za kiuchumi zinapofanyika na wawekezaji walipo. 
Kwa upande wa Zanzibar kuna matamasha makubwa mawili ya Sauti za Busara na Zanzibar International Film Festival (ZIFF) ambayo hufanyika kila mwaka. Ingawa matamasha haya hayahusiani na utalii moja kwa moja lakini shughuli za kitalii hutumika kwa asilimia kubwa kuwavutia wahudhuriaji. Uwepo wa fukwe safi, utajiri wa kihistoria na tamaduni, hoteli zenye hadhi ya juu, uwanja wa ndege, usafiri rahisi na nafuu wa maji pamoja na ukaribu wake na Dar es Salaam ni sababu tosha kwa wahudhuriaji na watalii. 

Kwa mara ya kwanza visiwani humo, mwaka huu yatafanyika Maonyesho ya Utalii ya Zanzibar (Zanzibar Tourism Show) kuanzia Oktoba 17 mpaka 20, yakiwa na lengo ya kutangaza vivutio vilivyopo pamoja na kuvutia wadau kwa ujumla.

Vipi kwa upande wa kanda za Kusini na Magharibi? 

Kwa muda mrefu mikoa ya Kusini na Magharibi imekuwa ipo kimya hususani kwenye upande wa maonyesho ya shughuli za kitalii. Licha ya kuwa na vivutio vya kila aina vilivyopo bado kuna jitihada hafifu za kuvitangaza na kuwavutia wadau wengi.Mikoa inayopatikana kwenye kanda hizi mbili imebarikiwa na vivutio vya kipekee ambavyo havipatikani maeneo mengine nchini. Hivyo basi, hivi ni vigezo tosha kwa serikali na wadau wa utalii kutupia jicho maeneo haya ili taifa linufaike na wananchi wa maeneo ya karibu.
Kwa mfano, yanapofanyika maonyesho kama KILIFAIR wanaonufaika moja kwa moja si wadau wa utalii pekee. Katika msimu wa tamasha hili wafanyabiashara wa mahoteli, migahawa, usafiri wa bodaboda na teksi, huduma za kibenki na sehemu za starehe hunufaika kwa kiasi kikubwa kwani huduma zao huwa zinatumika kwa viwango vikubwa.

Kwa kuhitimisha, utamaduni wa maonyesho kama haya ungesambaa nchi nzima angalau kuwe na onyesho kubwa mara moja kwa mwaka, watalii wa ndani na nje wangejua vivutio vya kila pembe ya Tanzania. Lakini hatutoweza kufanikiwa hilo endapo hatutohamasisha ujengaji wa hoteli za kisasa zinazokidhi vigezo vya kitalii, viwanja bora vya ndege, barabara nzuri za lami pamoja na huduma nyinginezo za jamii kama vile benki, hospitali nakadhalika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad