POLISI MORO WATOA UFAFANUZI MWANAMKE ALIYEJIFUNGUA NJIANI - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

POLISI MORO WATOA UFAFANUZI MWANAMKE ALIYEJIFUNGUA NJIANI

Share This
Na John Nditi, Morogoro

POLISI mkoani Morogoro inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu mwanamke aliyejifungua mtoto wakati akiwa njiani kupelekwa Kituo cha Afya Mang’ula, wilaya ya Kilombero mkoani humo mara baada ya kutolewa mahabusu ili kubaini kama kuna uzembe wowote umefanywa na watendaji ama askari na ikibainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Mugabo Wekwe ,alisema hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari juu ya tukio la kujifungua mtoto njiani mwanamke Amina Rafael Mbunda (27) mkazi wa Kijiji cha Kiswanywa , Tarafa ya Mang’ula , wilayani Kilombero , mkoa wa Morogoro.

Alisema , Polisi inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio la mwanamke huyo aliyefikishwa katika kituo cha Polisi Mang’ula kwa kosa la kukutwa na mali ya wizi kisha kujifungua akiwa njiani kuelekea katika Kituo  cha Afya Mang’ula.

Alisema , Mei 31, mwaka huu ilifunguliwa kesi ya wizi wa samani mbalimbali zenye thamani ya Sh 1,040,000 katika kituo cha Polisi Mang’ula kilichopo wilayani Kilombero mkoani Morogoro zilizoibwa kwa vipindi tofauti katika karakana ya Joseph Mdee iliyopo maeneo ya Posta Mang’ula .

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huyo alisema, baada ya tukio uchunguzi ulianza mara moja na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja alitwaje Ridhiwani Athuman na kukiri kuiba kisha kuwauzia watu mbalimbali akiwemo Abdallah Mohamed Mrisho (40) mkazi wa Kijiji cha Kiswanywa ,Tarafa ya Mang’ula.

Alisema ,askari walifika nyumbani kwa Mrisho kwa ajii ya upekuzi wakiwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na mlalamikaji na kumkuta mke wake aitwaye Amina Rafael Mbunda na kujitambulisha kisha kumweleza kuwa wanahitaji kufanya upekuzi.

Alisema , wakati wa upekuzi huo mlalamikaji alibaini kuwa fumbati “ base” ya mbele ya kitanda ikiwa katika kitanda kilichofungwa ni ya kwake na ilichukuliwa kama kielelezo pamoja na mwanamke huyo kwani ndiye aliyekutwa na mali hiyo ya wizi kisha kupelekwa kituo cha Polisi Mang’ula siku hiyo ya Mei 31, mwaka huu majira ya saa 12 jioni kwa hatua zaidi.

Alisema , kabla ya kuondoka na mtuhumiwa huyo, Mwenyekiti wa kijiji pamoja na askari walimjulisha mume wa mama huyo kwa njia ya simu kuwa mke wake amechukuliwa baada ya kukutwa na mali ya wizi na kupelekwa kituo cha Polisi Mang’ula na dhamana iko wazi na mume wa mama huyo aliahidi kuwa atafika kituoni akitoka katika shughuli zake.

Kaimu Kamanda huyo alisema ,mume wa mama huyo hakufika kituoni hapo na hakukuwa na ndugu wala jirani aliyefika kituoni kwa ajili ya kumwona au kuomba dhamana , hivyo ililazimika awekwe mahabusu kwa mujibu wa taratibu.

Alisema , ilipofika saa tisa usiku mama huyo ( Mtuhumiwa) alianza kulalamika kuwa anajisikia vibaya na anadhani huwenda ikawa ni uchungu ndipo askari walitafuta gari la kumpekea katika kituo cha afya na kutofanikiwa kuupata usafiri huo .

Kaimu Kamanda wa Polisi huyo alisema , mmoja kati ya askari aliyopo kituoni hapo aliamua kuchukua pikipiki yake kumbeba mama huyo pamoja na kukodi pikipiki nyingine ( Bodaboda) kisha kumpakia mama mmoja aliyeishi jirani na eneo la tukio aitwaye mama Kipangula kuelekea katika kituo cha afya Mang’ula.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi huyo ,mara tu baada ya kutoka Kituo cha Polisi wakielekea kituo cha Afya mama huyo alilalamika kuwa anataka kujisaidia , waliposimamisha pikipiki na mama huyo (mtuhumiwa )alishuka ndipo alipoanza kijifungua na kusaidiwa na mama Kipangula kisha kukimbizwa katika Zahanati iliyokuwa jirani na eneo hilo iitwayo Lugusha na kupatiwa huduma ya kwanza.

Alisema ,mara baada ya huduma hiyo, mama huyo aliwahishwa katika Kituo cha Afya Mang’ula ambapo alipokelewa akiwa salama yenye pamoja na mtoto ambaye ni wa kike na kuendelea kupata huduma kama akina mama wengine wanaojifungua nje ya Hospitali.

Katika hatua nyingine Mganga wa Kituo cha Afya Mang’ula ,Samweli Msomba akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema licha ya yenye kutokuwepo siku ya tukio hilo , lakini mama huyo aliletwa katika Kituo hicho akiwa tayari amejifungua na kulazwa kwa uangalizi kwa muda wa siku tatu na baadaye aliruhusiwa kwenda nyumbani.

‘ Alisema , mtoto huyo ni wakike na alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 3.5 na kwamba mama wa mtoto huyo hakuwa na tatizo baada ya kujifungua na alilazwa wodini kwa siku tatu ili kuona kama yapo madhara aliyapata wakati wa kujifungua .

“ Hakuwa na tatizo lolote baada ya kulazwa kwa muda wa siku tatu na aliruhusiwa , ambapo hali ya mwanake na mtoto walikuwa ni salama “ alisema Dk Msomba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad