Maonesho ya Utumishi wa Umma Kuanza Juni 18 Muhimbili - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

Maonesho ya Utumishi wa Umma Kuanza Juni 18 Muhimbili

Share This

Hospitali ya Taifa Muhimbili  (MNH) inatarajia kufanya maonesho ya Utumishi wa Umma-siku tatu mfululizo ambayo yatafanyika ndani ya hospitali hiyo kuanzia Juni 18 hadi 20, 2018.

Maonesho hayo ambayo yatazinduliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu yamebeba kaulil mbiu inayosema “Mapambano dhidi ya rushwa kwa kushirikisha wadau na kujenga uongozi bora ili kufikia malengo ya ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika  na malengo ya maendeleo endelevu’’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Bw. Aminiel Aligaesha amesema Hospitali itafanya maonesho hayo kwa kipindi cha siku tatu kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa11jioni ili wananchi waweze kuona shughuli zinazofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Wananchi watapata elimu juu ya utaratibu wa kupata huduma, kutoa elimu ya afya kuhusiana na magonjwa mbalimbali na pia kuwapa fursa wananchi kutoa maoni na malalamiko juu ya huduma tunazotoa,’’amesema Bw. Aminiel.

Kupitia kauli mbiu hiyo amesema MNH  itaeleza ni namna gani wanapambana na vitendo au viashiria vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi na pia kuwaeleza wananchi mipango iliyopo katika kutoa huduma za afya ambazo ni endelevu.

Katika maonesho hayo watalaam waliobobea kutoka maeneo mbalimbali ya Hospitali watakuwepo ambao ni washauri,wachunguzi,tiba na upasuaji ili kukutana na wananchi watakaojitokeza.

Maadhimisho hayo ni moja ya matukio katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi wanachama huadhimisha kwa kufanya maonesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na taasisi zake na pia kongamano kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma.

Maonesho hayo huratibiwa na Ofisi ya Rais Menejiment ya Umma na Utwala Bora ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha akiwaonesha waandishi wa habari idara mbalimbali zitakazoshiriki kwenye maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2018. Maonesho hayo yanatarajiwa kuanza tarehe 18 hadi 20 Juni, mwaka huu kwenye viwanja vya Muhimbili.
 Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo leo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha akisisitiza jambo kwa waandhishi wa habari.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad