NIDA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI UNAOENDANA NA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

NIDA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI UNAOENDANA NA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Share This
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe Alexander Mnyeti amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) na kusifu jitihada kubwa za Kaimu mkurugenzi Mkuu NIDA ndugu Andrew W. Massawe ambaye ndani ya kipindi kifupi ameweza kuleta mabadiliko makubwa ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya kuwasajili wananchi kupata Vitambulisho vya Taifa.

Hayo ameyasema wakati alipofanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida ofisi kwake; katika ziara ya Mkurugenzi huyo kukagua maendeleo ya zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu linaloendelea mkoani Manyara.  

Akitoa majumuisho ya maendeleo ya zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu linaloendelea mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara amesema mpaka sasa zaidi ya wananchi 650,000 wameshasajiliwa katika wilaya zote tano za mkoa wake.

“ Idadi hii ni zaidi ya  asilimia 84 ya makisio ya idadi halisi ya wananchi wenye umri wa miaka 18 wanaotazamiwa kusajiliwa, idadi iliyobaki tumejipanga kukamilisha usajili mwishoni mwa mwezi Juni, 2018” alisisitiza.

Amesema mwitikio wa watu ni mkubwa kutokana na wananchi wengi kutambua umuhimu wa kuwa na Vitambulisho vya Taifa, ambapo mpaka sasa Wilaya ya Hanang’ na Mbulu zimeshamaliza zoezi la Usajili huku wilaya za Babati, Kiteto na Simanjiro zitakamilisha zoezi hilo mwishoni mwa mwezi Juni,2018. Kwa zile Wilaya ambazo usajili umekamilika wananchi ambao hawakusajiliwa watapashwa kwenda makao makuu ya Wilaya hizo kupata huduma.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA amemshukuru Mkuu wa Mkoa huo kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wa Manyara wanasajiliwa pamoja na kufanikisha Usajili wa wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya Tanzanite - Mererani ambapo jumla ya wachimbaji wadogo 10,495 walisajiliwa na kupatiwa Vitambulisho.

Amesema hatua hii imeleta mafanikio makubwa katika kuhakikisha kupitia Kitambulisho cha Taifa, watakaonufaika na Uchimbaji na biashara katika migodi hiyo wanakuwa watanzania hususani katika kipindi hiki ambacho ukuta katika machimbo hayo umekamilika.

Akifafanua mipango ya Mamlaka kwa sasa; Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA amesema moja ya malengo ya ziara yake Manyara ni kukagua maendeleo ya zoezi la Usajili na kuanza kazi kwa vituo vya Uchakataji taarifa ambavyo vitawezesha taarifa za wananchi zilizokusanywa kuhakikiwa na kutumwa kwenye kituo kikuu cha Uzalishaji makao makuu kwa ajili ya hatua za uzalishaji Vitambulisho. Lengo ni kuhakikisha malengo tuliyojiwekea yanakamilika ndani ya wakati.

“ kiujumla nimeridhishwa sana na utendaji katika mkoa wa Manyara; na jinsi Mkuu wa Mkoa na wakuu wa Wilaya walivyojipanga katika kuhakikisha zoezi la Usajili mkoa wa Manyara linakamilika na wananchi wanapata Vitambulisho. Ndiyo maana umeona hata kituo cha kuchakata taarifa kipo kwenye ukumbi karibu kabisa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuonyesha uwepo wa ufuatiliaji wa karibu wa zoezi hili. Kwa hili nimefarijika sana….” alisisitiza

Katika ziara hiyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu (NIDA) aliambatana na Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho ndugu Alphonce Malibiche, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati Bi. Rose Joseph na Meneja Mifumo ndugu Edson Guyai ambaye pia ni msimamizi wa usajili mkoa wa Manyara.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe Alexander Mnyeti akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) Bw. Andrew W. Massawe ofisini kwake
  Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe Alexander Mnyeti akiongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) Bw. Andrew W. Massawe ofisini kwake
Zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu likiendelea Mkoani Manyara ambapo mpaka sasa zaidi ya wananchi 650,000 wameshasajiliwa katika wilaya zote tano za mkoa huo.
Zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu likiendelea Mkoani Manyara ambapo mpaka sasa zaidi ya wananchi 650,000 wameshasajiliwa katika wilaya zote tano za mkoa huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad