MKAZI WA NYAMAGANA ASAIDIWA BAISKELI YA MIGUU MITATU - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

MKAZI WA NYAMAGANA ASAIDIWA BAISKELI YA MIGUU MITATU

Share This
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA.

Mkazi wa Mtaa wa Nyerere A katika Kata ya Mabatini wilayani Nyamagana katika Jiji la Mwanza, Fred Kaseko (47) amepata msaada wa baiskeli ya miguu mitatu (wheel chair) itakayomsaidia kwa usafiri.

Kaseko alipata ulemavu wa miguu uliosababishwa na ajali ya gari miaka tisa iliyopita na kusababisha ashindwe kutembea baada ya miguu kukosa mawasiliano kutokana na neva za mgongo kuathiriwa.

Akipokea msaada huo jana uliotolewa na familia ya Mohamed Abass Mahamoud Abbas Mohamud Damji yenye asili ya Kiasia ya jijini Dar es Salaam,Kaseko alisema ameteseka kwa miaka tisa akitembea kwa kujivuta kwa kutumia mikono.

Alisema alipata ajali na taratibu miguu ilianza kupoteza uwezo wa kutembea wala kusimama na alipokwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) na kufanyiwa vipimo iligundulika kuwa disc za mgongo zilikuwa zimekandamiza mishipa ya fahamu baada ya kupata ajali.

“ Wakati nikifanya kazi ya ukaguzi wa tiketi kwenye kampuni ya mabasi ya AM nilipata ajali iliyonisababishia tatizo hili. Nilipokwenda hospitali daktari alinieleza kuwa disc za uti wa mgongo zilipanda kwenye mishipa ya fahamu pamoja na misuli na hivyo kusababisha miguu kupoteza mawasiliano. Tiba pekee niliambiwa ni kufanya mazoezi ambayo hunigharimu sh. 5,000 kwa siku,” alisema Kaseko.

Alisema kwa mujibu wa daktari aliyemuhudumia matatizo hayo husababishwa na madhara yatokanayo na ajali bila kufanyiwa vipimo na kupata tiba ambapo aliwashukuru wafadhili waliotoa msaada huo pamoja na Mwenyekiti The Desk & Chair Foundation Sibtain Meghjee.

Mwenyekiti huyo wa The Desk & Chair Foundation alisema familia ya Mohamed Abbas Mohamud Damji iliguswa na tatizo la Kaseko na hivyo ikatoa baiskeli hiyo yenye thamani ya sh. 350,000 kupitia taasisi yake.

“Hii ni baiskeli ya 386 kutolewa na taasisi yetu na imetolewa na familia ya Damji ikiwa ni sadaka ya kumrehemu mtoto wao aliyefia nchini Canada akiwa masomoni iweze kumsaidia Kaseko.Misaada hii ni endelevu, inatolewa kwa watu wenye mahitaji kama haya ya ulemavu wa viungo hasa wa miguu inapotokea,”alisema Meghjee.

Hata hivyo Kaseko licha ya kupata msaada huo wa baiskeli bado anakabiliwa na changamoto ya kukatiwa huduma ya maji na Mamlaka Maji safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA) kutokana na malimbikizo ya ankara ya malipo ya maji kiasi cha sh.325,000 pamoja na fedha za kuhudhuria mazoezi ya viungo
 Fred Kaseko , mkazi wa Mtaa wa Nyerere A Mabatini kabla ya kupata msaada wa baiskeli ya miguu mitatu alikuwa akitambea kwa kutumia  mikono.
 Sheikh wa Bilal Muslimu Mission of Tanzania Hashim Ramadhan (kulia) akimkabidhi baiskeli ya miguu itatu Fred Kaseko.Nyuma ni familia ya Kaseko ambaye anasumbuliwa na miguu kupooza baada ya kupata ajali. Baiskeli hiyo imetolewa na familia ya Mohamed Abass Mahamoud Damji . Picha Na Baltazar Mashaka


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad