MADAKTARI WAZALENDO WAPATIWA MAFUNZO YA SIKU TATU UBONGO NA UTI WA MGONGO - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

MADAKTARI WAZALENDO WAPATIWA MAFUNZO YA SIKU TATU UBONGO NA UTI WA MGONGO

Share This

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar 

Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amesema kuwepo kwa Taasisi ya kutibu maradhi ya mishapa ya fahamu na uti wa mgongo (Neuro) hapa Zanzibar ni heshma kubwa na amewashauri wananchi wanaokabiliwa na matitizo hayo kutumia fursa ya kuwepo taasisi hiyo kwenda kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu kwani kinauwezo mzuri wa kutibu maradhi hayo.

Amesema Taasisi hiyo itasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wachache waliopo Zanzibar wanaoshughulika na magonjwa hayo na imeipunguzia Serikali gharama ya kuwasafirisha wagonjwa nje ya Zanzibar.Waziri wa Afya ameeleza hayo katika Taasisi ya Neuro iliyopo Hospitali kuu ya Mnazimmoja, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya madaktari wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo kutoka nchi za Afrika zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesema kuwepo Taasisi hiyo Zanzibar imeipunguzia Serikali kiasi cha shilingi milioni kumi kwa mgonjwa mmoja kumsafirisha kwenda kufanyiwa matibabu nje ya Zanzibar na wagonjwa wengi wenyematatizo ya mishipa ya fahamu na uti wa mgongo wanatibiwa bila kutoa malipo.

Waziri Hamad Rashid ameongeza kuwa taasisi hiyo inahitaji madaktari bingwa wazalendo sita na hivi sasa wapo watatu tu na utaratibu wa kuitumia taasisi hiyo kufanya warsha za Kimataifa itawasaidia madaktari wa Zanzibar kuwajengea uwezo zaidi.Amewashauri wananchi wa Zanzibar kujenga utaratibu wa kuvitumia vituo vya afya vya Wilaya na Mikoa kwa matatizo madogo ya kiafya ili Hospitali Kuu ya Mnazimmoja itumike kwa matatizo makubwa yaliyoshindikana kwani Serikali imevijengea uwezo vituo vya vijijini kwa vifaa tiba na dawa muhimu.

Daktari bingwa wa maradhi ya ubongo na uti wa mgongo kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi Kenya Dkt. Mahmood Qureish ambae anaratibu mafunzo hayo amesema Taasisi ya Neuro ya Zanzibar imekuwa maarufu kwa nchi za Afrika Mashariki na wagonjwa kutoka mataifa hayo wanafika kwa ajili ya matibabu.

Amesema mafunzo ya Taasisi ya Neuro ya Zanzibar ambayo ni ya kwanza kufanyika yataendeshwa darasani na vitendo katika vyumba vya upasuaji ili kuwajengea uwezo washiriki kufanya matibabu ya ubongo na uti wa mgongo watakaporejea nchini mwao.Mafunzo hayo yanawashirikisha madaktari wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo kutoka Kenya, Sudan, Afrika Kusini, Zimbabwe Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed akifungua warsha ya siku tatu ya Madaktari wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo kutoka mataifa ya Afrika chini ya Jagwa la Sahara inayofanyika Taasisi ya Neuro iliyopo Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Madaktari wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo kutoka mataifa ya Afrika chini ya Jagwa la Sahara waliohudhuria katika mkutano unaofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed katikat alievalia suti rangi ya krimu akipiga picha ya pamoja na Madaktari wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo kutoka mataifa ya Afrika chini ya Jagwa la Sahara (Picha na Abdalla Omar 
Daktari bingwa wa maradhi ya ubongo na uti wa mgongo kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi Kenya Dkt. Mahmood Qureish ambae anaratibu mafunzo hayo akizungumza na waandishi wa habari (Picha na Abdalla Omar  Maelezo – Zanzibar).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad