Je, ni salama kusafiri kwa ndege kipindi cha mvua? - JIACHIE

JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad

Je, ni salama kusafiri kwa ndege kipindi cha mvua?

Share This

Na Jumia Travel Tanzania

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, usafiri wa ndege ndio njia salama zaidi ya usafiri kuliko zote duniani ukilinganisha na nyinginezo kama vile gari, reli, pikipiki na maji. Tafiti zimezingatia kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo vya abiria vinavyosababishwa na njia ya usafiri husika.

Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (IATA) lilitoa ripoti yake ya tathmini ya mwaka 2017. Ripoti hiyo imeonyesha kuwa sekta ya usafiri wa anga imeboresha masuala ya usalama kwa asilimia 54 ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita. Kiwango cha ajali kwa mwaka 2016 kilikuwa ni 1.61 kwa safari milioni moja za ndege, ukilinganisha na kiwango cha 3.53 karibuni muongo mmoja uliopita, yaani mwaka 2007, na kupungua kwa zaidi ya asilimia 10 mwaka 2015. Mwaka 2016, abiria zaidi ya bilioni 3.7 walisafiri salama kwenye safari za kibiashara zaidi ya milioni 40.1.

Pamoja na takwimu hizo bado kwa baadhi ya abiria inakuwa ni changamoto kuutumia usafiri huo hususani kwenye kipindi cha mvua kubwa kama tunavyoshuhudia sasa katika maeneo mengi nchini Tanzania. Jumia Travel imekukusanyia mambo yafuatayo ya kufahamu na kufuata ili kukutoa hofu pindi utakapoamua kusafiri kwa ndege.

MAMBO UNAYOTAKIWA KUYAFAHAMU

Ni salama kusafiri kipindi mvua inanyesha. Kwa sababu umekutana na changamoto mbalimbali ukiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege haimaanishi hali itakuwa hivyo hivyo angani. Mashirika mbalimbali ya ndege duniani huendesha shughuli zao kipindi cha mvua. Huwa kunakuwa na sheria na taratibu zinazofuatwa ipasavyo kufanya hivyo, waongoza ndege hawawezi kuruhusu ndege kuondoka endapo hali ya hewa ni mbaya. Hivyo basi ondoa shaka kwamba ukiona ndege inapaa uwanjani, ujue safari yako ipo salama.

Tegemea mitikisiko ya kiasi. Kama ilivyo njia ya barabara au bahari kuna wakati unakutana na miinuko na kona za hapa na pale au mawimbi, vivyo hivyo na angani pia. Kusafiri kipindi cha mvua kubwa au upepo mkali kunaendana na mitikisiko kiasi ya ndege angani. Fahamu kuwa hali hiyo ni ya kawaida. Mitikisiko hiyo haimaanishi kwamba itaharibu chombo cha usafiri au kuhatarisha usalama wa abiria wake.

Radi haiwezi kudondosha ndege. Wataalamu wanabaisha kuwa ni hali ya kawaida ndege kukutana na radi mara kadhaa kwenye safari zake ndani ya mwaka. Na hata kama ikitokea, haimaanishi kwamba itaunguza ndege au abiria wake. Ndege nyingi zimeundwa kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia vifaa maalum kwa teknolojia ya hali ya juu. Rubani anaweza kuamua kutua ndege kwa tahadhari zaidi.

Ndege zimeundwa kukabiliana na changamoto tofauti. Hali mbaya ya hewa haiwezi kuharibu ndege. Kila kifaa kwenye ndege kimeundwa madhubuti kukabiliana ipasavyo na changamoto za angani. Mabawa yake yameundwa kukabiliana na hali ngumu kama ilivyo sehemu ya kukaa abiria. Tofauti na unavyofikiri, ndege inaweza kubadilika na kukabiliana na hali tofauti hususani linapokuja suala la usalama wa abiria wake.

Marubani na wahudumu wamefundishwa kukabiliana na misukosuko ya angani. Si jambo la kushangaza kwa abiria waoga kusafiri angani kustaajabu ni kwa namna gani marubani na wahudumu wa ndege wanakuwa kwenye hali gani kipindi cha msukosuko angani. Wao pia kama binadamu wanakuwa na hofu hiyo. Lakini cha muhimu kufahamu ni kwamba watu hao ni wabobezi na wamefundwa ipasavyo kuhakikisha unasafiri na kufika salama.  

MAMBO UNAYOTAKIWA KUYAFUATA

Kama hauiamini hali ya hewa, ziamini takwimu. Ni hali ya kawaida kuwa na wasiwasi kusafiri kipindi ambacho hali ya hewa ni hatarishi. Inashauriwa kama hauiamini hali ya hewa basi amini takwimu zilizofanyika kabla. Takwimu na tafiti kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kuaminika duniani zimeonyesha kuwa usafiri wa anga ndio njia salama zaidi ya usafiri kuliko zote. Ni mara chache kusikia ndege imeanguka ukilinganisha na ajali za gari au pikipiki.   

Epuka tafiti nyingi kupita kiasi. Kuna msemo maarufu wa Kiswahili unaosema kwamba, ‘ukimchunguza s
ana bata hautomla.’ Uoga wa kusafiri angani unaweza kukupeleka kufanya tafiti kutosha. Ili kujua usalama wake, tahadhari za kuchukua na pengine namna ya kujiokoa. Kumbuka kwamba wewe sio mtaalamu kwenye sekta hiyo, iamini timu nzima ya marubani na wahudumu wake katika kukusafirisha salama. Chumba na chombo wanachokitumia marubani na timu yao kwenye ndege ndicho kinachopokea taarifa halisi juu ya hali iliyopo mbele yao na namna bora ya kuendesha chombo walichopewa dhamana.  

Watazame wahudumu wa ndege. Kama ni mara ya kwanza na una hofu kubwa pindi ndege itakapopaa na kuwa angani, unashauriwa kuwatazama wahudumu wa ndege namna wanavyofanya shughuli zao bila ya wasiwasi wowote. Kwa kufanya hivyo kutakupunguzia na kukuondelea wasiwasi kama abiria ukiwa kwenye ndege.

Tii maagizo. Hiki ni kipengele muhimu cha kuzingatia. Kwa kiasi kikubwa hofu na ghasia ndizo husababisha majeraha ndani ya ndege. Na mara nyingi huwa ni abiria au watumishi wengine ndani ya ndege ambao hawakufunga mikanda yao. Unaweza kuona ni sahihi kupuuza ishara za kukutaka kufunga mkanda ndani ya ndege kwa kuwa mambo ni shwari. Zingatia kuwa hizo ishara zimewekwa kwa makusudi maalum. Hakikisha kuwa unafuata maagizo na miongozo yote kutoka kwa wahudumu wa ndege hususani mafundisho ya alama za usalama yanayotolewa ndani ya ndege.

Usafiri wa ndege nchini Tanzania unakua kwa kasi na kuwa kiungo muhimu katika nyanja tofauti hususani za kiuchumi kama vile ajira, biashara na utalii. Ni rahisi kusafiri kupitia Jumia Travel ambapo imekukushanyia huduma za mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi sehemu moja mtandaoni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad