728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Sunday, June 18, 2017

  WAZIRI MKUU MAJALIWA AONGOZA HARAMBE YA UJENZI WA KANISA PAROKIA YA ZUZU, DODOMA

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya familia yake akimkabidhi Mchango wa Shilingi Milioni Kumi, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda Kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Nyumba ya Paroko pamoja na kufanyia Ukarabati wa Kanisa Parokia ya ZUZU Dodoma. Kushoto ni Msaidizi wa Askofu Jimbo la Dodoma Baba Chesco Msaga . Harambe hiyo imefanyika June 17, 2017 katika Makazi ya Waziri Mkuu Mstaafu Pinda yaliyopo ZUZU nje kidogo ya Mjini Dodoma.
  Waziri Mkuu Mstaafu,  Mizengo Pinda akiwaonyesha Wageni waalikwa (hawapo pichani) Shilingi Milioni Kumi Mchango aliokabidhiwa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kwa niaba ya Familia yake , Kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Nyumba ya Paroko pamoja na kufanyia Ukarabati wa Kanisa Parokia ya Zinje (ZUZU) Dodoma. Kushoto ni Msaidizi wa Askofu Jimbo la Dodoma Baba Chesco Msaga . Harambe hiyo imefanyika June 17, 2017 katika Makazi ya Waziri Mkuu Mstaafu Pinda yaliyopo ZUZU Nnje kidogo ya mjini Dodoma.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (Kushoto) akiwa ameongozana na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Mkewe Tunu Pinda walipo mpokea katika makazi yao yaliyopo Zuzu nje Kidogo ya Mjini Dodoma June 17, 2017, kuhudhuria Misa ya kumbukumbu ya Marehemu Mzee Exavery Pinda Baba Mzazi wa Mizengo Pinda, Pamoja na kuongoza Uchangiaji wa Ujenzi wa Nyumba ya Paroko na Ukarabati wa Kanisa la Parokia ya ZUZU. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.


           TAIFA LA WATU WAADILIFU HUANZIA KWENYE FAMILIA - WAZIRI MKUU   

  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi. 

  “Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.

  Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Juni 17, 2017) wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma. 

  Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda. Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi.

  Waziri Mkuu alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili. “Kupitia funzo tulilolipata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?,” alihoji.

  “Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.

  Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia sh. milioni 10 ambapo jumla ya sh. milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, sh. 111,150,000 zilikuwa ni ahadi, sh. 38,447,000 zilikuwa ni fedha taslimu na sh. 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.


  Mapema, akiongoza ibada ya shukrani, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwani hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu ya akili zake.  

  “Hata sisi tunasahau kumshukuru Mungu hasa pale mambo yetu yanapotunyookea. Tunadhani ni kwa akili zetu ndiyo mambo yetu yananyooka. Tunapaswa tukumbuke kuwa maishayetu yapo mikononi mwa Mungu, na yeye ndiye anajua njia zetu,” alisema akirejea mfano wa wakoma 10 walioponywa na Bwana Yesu na mmoja tu ndiye alirudi kushukuru.

  Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia. 

  “Sasa hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu. 

  “Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo. 

  IMETOLEWA NA:
  OFISI YA WAZIRI MKUU,
  S. L. P. 980,
  40480 - DODOMA.            
  JUMAPILI, JUNI 18, 2017.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: WAZIRI MKUU MAJALIWA AONGOZA HARAMBE YA UJENZI WA KANISA PAROKIA YA ZUZU, DODOMA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top