728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Sunday, June 18, 2017

  WATENDAJI HAKIKISHENI MNASAFISHA TAARIFA CHAFU ZA WATUMISHI KWENYE MFUMO WA HCMIS  Mkurugenzi Idara ya Uchambuzi na Ushauri kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw.Micky Kiliba,akitoa ufafanuzi kuhusu ujazaji wa fomu za OPRAS zinazopima utendaji kazi wa Mtumishi wa Umma.
  wat2
   Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Susan Mlawi akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya mbeya alipofanya ziara ofisini hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2017.
  …………………………………………………………………………….
  Watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wametakiwa kuhakikisha suala la taarifa chafu za Watumishi linamalizika haraka iwezekanavyo ili kurahisisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).

  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Susan Mlawi alisema hayo katika kikao kazi na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na  Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2017.

  “Sitegemei tena kusikia Halmashauri au Mkoa una taarifa chafu za watumishi wake, hivyo nawaagiza Maafisa Utumishi na Watendaji katika Mikoa na Halmashauri mhakikishe suala hili linafikia ukingoni” Bi.Susan alisema.

  Aliongeza kuwa suala la uhakiki wa taarifa chafu za watumishi limefanyika kwa muda mrefu sasa, hivyo halitakiwi kuzungumzwa tena katika kipindi hiki.
  Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu ,Ofisi ya Rais-UTUMISHI  Bw.Leornad Mchau aliongeza kuwa taarifa chafu za watumishi ni eneo ambalo linasabisha uwepo wa watumishi hewa.
  “Unakuta taarifa za mtumishi hazionyeshi cheo chake wala hazionyeshi tarehe yake ya kuzaliwa, hili ni tatizo” Bw. Mchau alisema.

  Alifafanua kuwa jitihada za kufanyia kazi taarifa chafu za Watumishi wa Umma zilianza toka mwaka 2010 ambapo Maafisa Utumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaohusika na Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS)  baadhi yao waliwajibishwa kwa kuzembea kufanyia kazi taarifa chafu.

  Bw.Mchau alisisitiza kuwa Watumishi wa Umma watakaoonekana taarifa zao hazieleweke kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) watafutwa mara moja.

  “Mwezi uliopita tuliondoa watumishi kadhaa ambao taarifa zao hazieleweki kwenye mfumo wa HCMIS na hakuna mtumishi hata mmoja aliyekuja kulalamika kuondolewa kwenye mfumo.” Bw. Mchau alisema na kuongeza kuwa kuanzia mwezi Julai 2017 takriban watumishi 16,000 ambao vyeo vyao havijulikani kwenye mfumo wa HCMIS wataondolewa.

  Bw. Mchau alitoa rai kwa Watumishi wa Umma kuhakiki taarifa zao za kiutumishi kwa kujisajili katika Tovuti ya Watumishi (Watumishi Portal) na kuangalia kama zipo sahihi kabla hawajaondolewa kwenye mfumo na pia kila mtumishi ahakikishe anajiandikisha na kupata kitambulisho cha Taifa ili utambulisho wake wa Taifa ujulikane.

  “Mtumishi wa Umma ambaye hana kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho wa Taifa tutamhesabu kuwa ni mtumishi hewa na yeyote ambaye ana mshahara usioeleweka ifikapo Julai 15, 2017 mfumo wa HCMIS utamtoa kimfumo (Automatically).

  Hatima ya Watumishi walioghushi vyeti
  Akitoa ufafanuzi kuhusu hatma ya Watumishi wa Umma walioghushi vyeti Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Susan Mlawi alisema kuwa inasubiriwa taarifa kutoka Baraza la Mitihani Tanzania ambayo itakuwa imejumuisha matokeo ya rufaa za Watumishi walio kwenye orodha ya vyeti vya kughushi.

   Katika hatua nyingine Bi. Susan aliainisha kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI imeandaa mapendekezo ya namna ya kushughulikia suala la watumishi walioghushi vyeti.

   Upungufu wa Watumishi
  Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Susan Mlawi alisema Serikali inaangalia namna ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika baadhi ya Halmashauri na Mikoa.
  “Zipo baadhi ya ofisi ambazo zina watumishi wa ziada na nyingine zina watumishi wachache kwa maana hiyo ofisi yenye watumishi wa ziada itatakiwa iwahamishie kwenye ofisi nyingine yenye upungufu wa watumishi”Bi. Susan alisema.
  Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS)
  Mkurugenzi Idara ya Uchambuzi na Ushauri Kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw.Micky Kiliba alisema UTUMISHI inaangalia namna ya kufanyia marekebisho fomu za OPRAS za walimu, makatibu muhtasi na madereva ili kuhakikisha kuwa zinaendana na mipango mikakati yao ya kazi kwa mwaka mzima.
  Wiki ya Utumishi wa Umma inatarajia kufikia kilele tarehe 23 Juni, ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika huitumia kutambua mchango wa watumishi katika utendaji kazi, na kuhudumia jamii. Ofisi ya Rais-UTUMISHI mwaka huu 2017 imepanga kuadhimisha kwa kukutana na Watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kujua changamoto wanazokutana nazo katika kutatua kero za Watumishi wa Umma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: WATENDAJI HAKIKISHENI MNASAFISHA TAARIFA CHAFU ZA WATUMISHI KWENYE MFUMO WA HCMIS Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top