728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, June 20, 2017

  NDOA NA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO

  Meneja wa Utekelezaji wa miradi wa asasi ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC) James Mlali 
   
   
  Zipo sababu nyingi na ushahidi mwingi wa kisayansi, unaonyesha kuwa, ndoa na mimba katika umri mdogo wa msichana chini ya umri wa miaka 18 ni hatari kwa afya na mstakabali wa maisha yake na mtoto wake.
   
  Wasichana wengi wakati huu licha ya kuanza kupevuka wanakuwa hawajakomaa kiakili na uwezo wao ni duni katika maamuzi juu ya kufaa kwa mtu atakayekuwa mwenzi sahihi wa maisha.

  Kimwili pia wasichana katika umri huu wanakuwa hawajawa tayari kuyakabili majukumu ya uzazi na unyumba, nyonga za wasichana wanaoendelea kukuwa mara nyingi huwa changa na finyu kiasi kwamba husababisha matatizo mengi ya uzazi wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida.

  Wasichana wengi huchelewa kujifungua au huchukuwa saa nyingi za uchungu kabla ya kujifungua, hali hii inaweza kusababisha kifo cha mama au mtoto au wote wawili kama matibabu ya dharura ya upasuaji kwa ajili ya uzazi hayakufanyika. Idadi kubwa ya akina mama wanaojifungua kwa njia ya upasuji ni wale walio na umri mdogo.

  Meneja wa Utekelezaji wa miradi wa asasi ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC) James Mlali anasema tatizo jingine linaloambatana na mimba katika umri mdogo ni pamoja na kutokwa na damu nyingi pale mimba inapoharibika au wakati wa kujifungua. Wasichana wengi hukabiliwa na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kupata uambukizo wa bakteria katika njia ya kizazi pamoja na kupata kifafa cha mimba.

  Wasichana wadogo mara nyingi huzaa watoto wenye uzito pungufu au njiti, watoto namna hii hukabiliwa na na hatari pamoja na changamoto nyingi za kiafya katika umri wao chini ya miaka mitano. Watoto wengi hupata matatizo ya mtindio wa ubongo na taahira ya akili. Wasichana wengi wanaozaa katika umri mdogo hupata hali ya aibu na hisia ya kudharauliwa mambo ambayo huongeza mzigo kwa wote mama na mtoto.

  Mlali anongeza kuwa wasichana wanao olewa au kupata mimba za utotoni hupeteza fursa na haki ya elimu. Wengi wao hufukuzwa shuleni au wazazi wao hupoteza imani kwao kiasi kwamba, husita kuwaendeleza kimaisha hata baada ya kujifungua, hali hii hufungua mlango kwa msichana kuingia katika umaskini na kuzaa ovyo bila mpangilio. Mzigo huongezeka pale msichana anapolea watoto peke yake kama hakubahatika kuolewa au kama ataachika baada ya kuolewa.

  Wasichana wanaoolewa kutokanan na kukosa uwezo wa kukabili matakwa ya unyumba na majukumu yake, wengi hukabiliwa na unyanyasaji, ukatili pamoja na udhalilishaji wa kijinsia ndani ya ndoa. Wengi hupata vipigo vinavyo wasababishia ulemavu wa maisha au vifo.Wengi hutukanwa na kubezwa.Wengi hulazimishwa kuolewa na watu wenye umri mkubwa bila hata kupima damu kwa ajili ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kabla ya ndoa.

  Hali hii huwafanya wasichana wanaoolewa katika umri mdogo kukabiliwa na hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI na wengi huwa wajane kabla ya kuwa watu wazima. Wale wanaoachika huwa na uwezekana mkubwa wa kuachika tena pale wanapoolewa kwa mara nyingine. Hii hutokana na athari za kisaikolojia zinazowajengea wasichana hawa doa la kitabia katika jamii na kuwafanya wasione umuhimu wa kudumisha mahusiano ya ndoa kutokana na uzoefu mbaya walioupata katika ndoa za awali.

  ‘Mara nyingi wasichana wadogo hawana elimu ya kutosha kuhusu muda wa vipindi ambavyo wanaweza kupata ujauzito.. Wengi wao pia kutokana na sababu mbalimbali za kibinafsi na za kijamii, hawapati fursa za kutumia huduma za afya ya uzazi wa mpango’, anaongeza Mlali

  Wasichana wengi wanaojihusisha na ngono kabla ya ndoa hupata mimba zisizopangwa, zisizotakiwa na zisizotarajiwa. Jambo hili huleta mzigo mkubwa wa kihisia kwa msichana hasa pale anapokuwa mwanafunzi. Wasichana wengi wanaojikuta katika hali hii hufikiria kutoa mimba kama njia pekee ya ufumbuzi wa tatizo. Wengi hutoa mimba katika mazingira hatarishi na kwa njia zisizozingatia afya na usalama. Hii hutokana na ukweli kuwa, utoaji mimba ni kosa la kisheria na kimaadili katika nchi nyingi.

  Wasichana wengi wanaopata watoto katika umri mdogo, hukabiliwa na tatizo la kulea watoto peke yao kwa vile wengi huwa hawajaolewa. Na hata kama wataolewa, wengi huachika mapema. Wengi wao hawana maandalizi kwa ajili ya ndoa na majukumu ya kutunza watoto.
   
  Watoto wengi wa akina mama hawa hupata matatizo ya kihisia hasa pale wasipowaona baba zao pale nyumbani kama ilivyo kwa watoto wenzao. Jambo hili huwasababishia athari ziambatanazo na huzuni, fedheha, msongo wa mawazo, kuumwa mara kwa mara, kutofanya vizuri katika masomo yao, kukosa usingizi mara kwa mara na kukosa mapenzi ya baba.

  Kutokana na hali, Mlali anasema kuwa ingawa kuachana na ngono kabisa ni jambo zito kwa wasichana wengi wa kizazi kipya kutokana na shinikizo la utandawazi, lakini bado inawezekana. Kinachohitajika ni kujifunza na kujua jinsi ya kutumia uzazi wa mpango kwani ndio njia pekee ya kuepuka mimba za utotoni. Na kwa sababu hiyo kwa wasichana wadogo wataweza kuendelea na elimu na hatimaye kuwa na maisha mazuri ya ukubwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: NDOA NA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top