728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, May 23, 2017

  Wachimbaji wadogo wa madini nchini watakiwa kuepuka ajali zisizo za lazima

  Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuepuka ajali zisizo za
  lazima kwani tangu mwaka 2008 hadi Mei 2017 zimetokea ajali 125 kwenye
  migodi yenye leseni na vifo ni 213.

  Ajali zilizotokea kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wasio na leseni
  nchini (maeneo ya mifumuko ya uchimbaji madini) katika kipindi hicho
  ni 56 na kusababisha vifo vya wachimbaji 140.

  Kamishna wa madini nchini, mhandisi Benjamin Mchwampaka aliyasema hayo wakati akizungumza na mameneja na wamiliki wa migodi mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

  Mhandisi Mchwampaka alisema ajali nyingi kwenye migodi ya wachimbaji
  wadogo zinasababishwa na uzembe, kwani kwa mwaka huu pekee hadi Mei 15 ajali zilizotokea ni 11 na kusababisha vifo 26.

  Alisema kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani,
  ajali zilizotokea kwa wachimbaji wadogo kwa kipindi cha 2008/2017 ni
  31 na wachimbaji wadogo waliopoteza maisha ni 40.

  Alisema uchambuzi wa takwimu za ajali hizo unaonyesha kuwa vyanzo
  vikubwa ni kuangukiwa na vifusi kwa kukatika kwa ngema, kulipukiwa na
  baruti, kukosa hewa, kuteleza na kuangukia mgodini.

  Alisema hawatafumbia macho ajali za uzembe kwenye migodi na
  wataifungia mara moja na kumchukulia hatua meneja na mmiliki,
  haitafunguliwa hadi mkaguzi mkuu wa migodi atakapojiridhisha.

  “Tunapaswa kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa usalama na kauli mbiu
  ya wachimbaji wadogo nchini iwe usalama kwanza, familia zetu
  zinatuhitaji na Taifa linatuhitaji,” alisema mhandisi Mchwampaka.

  Mkaguzi mkuu wa migodi nchini, mhandisi Ally Samaje alisema lengo la
  mafunzo hayo ni kupunguza matukio ya ajali zinazoweza kuepukwa na
  wachimbaji wadogo hivyo mafunzo hayo yatawajengea uwezo.

  Mhandisi Samaje alisema kila mmiliki wa leseni ya madini anazingatia
  maelekezo yote waliyoyatoa kwa kufanya kazi zao kwa usalama, kwani
  ajali hizo zimesababisha vifo na vilema vya maisha.

  “Kamishna wa madini ameshatoa maelekezo ya kuimarisha masuala ya
  usalama, afya na utunzaji mazingira hivyo wamiliki wa migodi wawape
  majukumu mameneja wayasimamie hayo,” alisema Samaje.

  Mmoja kati ya wamiliki wa migodi Hamis Juma aliishukuru wizara ya
  Nishati na Madini kwa kuendesha mafunzo hayo kwa mameneja na wamiki wa migodi kwani elimu hiyo itasaidia kupunguza ajali mgodini.

  “Kupitia elimu hii tumekumbushwa wajibu wetu na pia mameneja na
  tunatarajia watatekeleza hayo kwa faida ya wachimbaji wenyewe na jamii
  inayoishi maeneo yanayozunguka migodi yetu,” alisema Juma.
  Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Chama cha wachimbaji wadogo wa Madini Mkoani Manyara, (Marema) na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wakiwa kwenyemafunzo ya usalama migodini.
  Kamishna wa madini Tanzania, mhandisi Benjamin Mchwampaka akizungumza na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kuhusiana na usalama kwenye migodi yao.
  Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Chama cha wachimbaji wadogo wa Madini Mkoani Manyara, (Marema) na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wakiwa kwenye
  mafunzo ya usalama migodini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Wachimbaji wadogo wa madini nchini watakiwa kuepuka ajali zisizo za lazima Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top