728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, May 26, 2017

  UVCCM MKOA WA IRINGA WAMPONGEZA RAIS DKT MAGUFULI, WATAKA MAFISADI KUJIONDOA WENYEWE


  Viongozi wa UVCCM mkoa wa Iringa wakiunga mkono utendaji kazi wa Rais Dkt John Magufuli leo baada ya kumalizika kwa zoezi la kutoa tamko la kumpongeza Rais kwa kazi nzuri ,kutoka kulia ni mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah ,katibu UVCCM Iringa mjini Alophonce Munyinga , mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza , katibu UVCCM mkoa James Mgego , katibu UVCCM Iringa vijiji Ignas Kinyowa na viongozi wengine .

  Vijana walioshiriki zoezi hilo

  Vijana wa UVCCM wakiwa katika zoezi hilo la kumpongeza Rais Dkt Magufuli  Vijana wakiajiandaa kutoa tamko lao leo

  Katibu wa UVCCM mkoa wa Iringa James Mgego katikati akiwa na makatibu wake wa wilaya kushoto ni katibu wa Iringa mjini Alophonce Munyinga na kulia ni katibu wa UVCCM Iringa vijijini Ignas Kinyowa  Na MatukiodaimaBlog


  UMOJA wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa umepongeza hatua ya Rais Dkt John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo baada ya ripoti ya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu na kataka mawaziri zaidi watakaohusishwa na ufisadi kutumbuliwa .


  Huku mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akidai kuwa mkoa wake hauzui wananchi kumpongeza Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwatumikia ila hatapenda kuona wananchi wanaunga mkono maamuzi mbali mbali ya Rais kwa kufanya vurugu na kuandamana barabarani .


  Akizungumza na wanahabari leo ofisini kwake juu ya tamko hilo la kumpongeza Rais Dkt Magufuli kwa kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya Taifa katibu wa UVCCM mkoa wa Iringa James Mgego alisema vijana mkoani hapa wamepokea kwa mikono miwili uamuzi huo wa Rais wa kumuondoa waziri Prof Muhongo na kutaka mawaziri na viongozi wengine wa umma kuwajibika kwa faida ya umma na si vinginevyo.


  “ Umoja wa vijana mkoa wa Iringa unaungana na kaimu katibu mkuu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka kupongeza hatua iliyochukuliwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt John Pombe Magufuli kwa hatua alizozichukua za kizalendo kwa maslahi ya watanzania kwa kutengua uteuzi wa waziri wa Nishati na madini ….Rais amefanya jambo zuri ambalo linapongezwa na kila mtanzania kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo “


  Alisema kuwa Rais Dkt Magufuli amechukua uamuzi sahihi wakati sahihi kwani nchi ilikuwa ikipoteza raslimali nyingi kwa ajili ya kuwanufaisha wachache kwa maslahi yao wenyewe na sio jamii ya kitanzania .


  Hivyo alisema kuwa umoja wa vijana wa CCM mkoa wa Iringa umeona ni vema kujitokeza mbele ya vyombo vya habari kupinga vikali vitendo vya rushwa na ufisadi ,dhuruma na wizi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wasio wazalendo na Taifa .


  Mgego alisema UVCCM mkoa wa Iringa haitasita kuwafichua wale wote ambao wanaikwamisha serikali kwa kufanya vitendo vya ufisadi ama dhuruma dhidi ya watanzania kwa kutumia nafasi zao za uongozi walizo pewa .


  Aidha alisema kwa kuwa ripoti ya pili ya kiuchunguzi dhidi ya mchanga huo wa madini inakuja ni vizuri wale wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine kujitafakari na kuchukua hatua ya kujiuzulu nafasi walizopewa kabla ya kutumbuliwa na Rais .


  Pia katibu huyo aliwataka vijana kuendelea kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbali mbali ndani ya chama hicho na kutowasikiliza mafisadi ambao wapo kuona CCM inakwama katika uchaguzi huo wa ndani ya chama .


  Katibu wa UVCCM wilaya ya Iringa mjini Alphonce Muyinga alisema kuwa wanazo taarifa za wote wanaohujumu uchaguzi wa CCM mkoani Iringa na kuwa dawa yao inachemka kwani hawataona haya kuwashugulikia watu hao wanaotaka kukwamisha uchaguzi huo wa CCM .


  Mkuu wa mkoa wa Iringa Masenza ambae alialikwa katika zoezi hilo la utoaji wa tamko alipongeza hatua ya vijana hao kutambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt Magufuli na hata kutoa tamko hilo la pongezi .


  Masenza alisema kuwa kumekuwepo na maombi kutoka kwa wananchi wa kawaida maeneo mbali mbali ya mkoa wa Iringa kuomba kufanya maandamano makubwa ya kumpongeza Rais Dkt Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na maamuzi mbali mbali yenye lengo la kuwakomboa watanzania na kuwa hakuna kiongozi anaye zuia wao kukutana kutoa pongezi zao kwa Rais ila si kwa kuandamana mitaani .


  “ Mimi kama mkuu wa mkoa wa Iringa nawapongeza pia wananchi wangu ambao wametambua kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu katika Taifa ….nawaomba sana wananchi wenye pongezi kwa rais ruksa kuzitoa ila utaratibu ambao wanapaswa kuutumia ni kukutana katika vikao vya ndani kama walivyofanya vijana wa CCM na sio kufanya maandamano mitaani”
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: UVCCM MKOA WA IRINGA WAMPONGEZA RAIS DKT MAGUFULI, WATAKA MAFISADI KUJIONDOA WENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top