728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, April 13, 2017

  MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME CHA MTERA

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amesimama kwenye kituo cha Kufua Umeme cha Mtera akiwa njiani kuelekea Dodoma ambapo Meneja wa Kituo hicho Mhandisi John Sikauki alimpa taarifa ya kituo ambapo alimueleza kuwa kina cha maji kipo chini sana na wanapokea maji kutoka Mto Ruaha Mdogo na Kisigo (hasa wakati wa mvua)na kwa sasa hawapati maji kabisa kutoka Mto Ruaha Mkuu.

  Makamu wa Rais alisikitishwa na taarifa hii na aliahidi kuwa Kikosi Kazi cha Kitaifa alichozindua cha kunusuru ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kitatoa majawabu ya tatizo hili na aliomba Tanesco kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi hiki.

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akipokea taarifa ya kina cha maji katika kituo cha kufua umeme cha Mtera kutoka kwa Meneja wa Kituo hicho Mhandisi John Sikauki wakati akiwa njiani kuelekea Dodoma baada ya kumaliza shughuli za kuzindua Kikosi Kazi cha Taifa cha kunusuru ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu mjini Iringa. (PichA na Ofisi ya Makamu wa Rais)
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyakazi wa kituo cha kufua umeme cha Mtera akiwa njiani kuelekea Dodoma baada ya kumaliza shughuli za kuzindua Kikosi Kazi cha Taifa cha kunusuru ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu mjini Iringa.


   
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza Viongozi wa mikoa wa mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya kukabiliana na tatizo la kilimo karibu na mito ambacho kimechangia kupungua kwa maji kwenye bwawa la Kufua Umeme la Mtera.

  Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara fupi katika bwawa la Kuzalisha umeme la Mtera wakati akielekea Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi wa Bwawa hilo baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya Siku Tatu mkoani Iringa.

  Makamu wa Rais amesema uharibifu mkubwa unaondelea kwenye mito inayotiririsha maji kuelekea Bwawa la Mtera ndio chanzo cha maji kuendelea kupungua mwaka hadi mwaka hivyo hatua za kukabiliana na hali hiyo ni lazima zikuchuliwe ili kukokoa bwawa hilo kukauka.

  Amesema bwawa la kufua umeme la Mtera ni muhimu kutokana na uzalishaji wake wa umeme ambao unatumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi hivyo Serikali haitakubali hata kidogo bwawa lisitishe kuzalisha umeme kutokana na uharibifu huo wa mazingira.

  Makamu wa Rais amewahimiza wafanyakazi wa kituo hicho kufanya kazi kwa uzalendo ili kuhakikisha kituo hicho kinaendelea kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa pamoja na changamoto zinazojitokeza.

  Akitoa Taarifa ya Hali ya Uzalishaji Umeme kwenye kituo hicho kwa Makamu wa Rais, Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera Mhandisi John Sikauki amemueleza Makamu wa Rais kuwa hali ya mitambo ni nzuri ambapo mpango wa matengenezo kwa kuzingatia umri wa mitambo wa miaka 28 umekwiza anza.

  Amesema matengenezo makubwa katika kituo hicho yamefanyika ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Jenereta Mbili.

  Mhandisi Sikauki ameeleza kuwa kina cha maji kwa sasa katika bwawa hilo hadi kufikia Aprili mwaka 2017 ni mita 693.76 juu ya usawa wa bahari na kina hicho cha maji kina uwezo wa kuzalisha umeme hadi mwisho mwa Octoba mwaka huu.

  Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera amesema jitihada za sasa zinazofanywa na Serikali za kunusuru Hifadhi ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu maana ndio chanzo cha kuaminika cha kufanya Bwawa la Mtera kuwa na maji ya uhakika na hivyo kutaleta ufanisi katika ufuaji wa umeme katika kituo hicho na cha Kidatu kwa mwaka mzima.

  Imetolewa na
  Ofisi ya Makamu wa Rais
  Iringa 13-April-2017.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME CHA MTERA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top