728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, April 25, 2017

  MAHAKAMA YA WATOTO SULUHISHO LA KESI ZA WATOTO

  Mwuonekano wa jengo la Mahakama ya Watoto iliyopo katika Jiji la Mbeya.

  Na Magreth Kinabo – Mahakama ya Tanzania


  Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu habari za vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.

  Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa matamko ambayo yanaitaka jamii kufahamu haki za mtoto ikiwa ni hatua ya kuwaepusha watoto wasiathiriwe na tabia hatarishi.

  Miongoni mwa viongozi hayo ni Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Afya,Jinsia na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Ummy Mwalimu akiwemo Naibu wake. Dkt. Hamis Kingwallah na baadhi ya viongozi wengine mbalimbali.

  Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa asasi za kiraia na dini mbalimbali wameungana ili kuhakikisha watoto hao, wanakua katika maadili mema na kuweza kutimiza ndoto zao.

  Mbali na hilo, kuhakikisha kwamba watu wanaowarubuni watoto wanachukuliwa hatua za kisheria.

  Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano yaani 2015/16 hadi 2019/20, imejenga Mahakama nyingine ya watoto ambayo iko katika Jiji la Mbeya.

  Kupitia mpango huo, hivi sasa Tanzania ina mahakama mbili za watoto ambazo moja iko katika jiji la Dares Salaam na nyingine jiji la Mbeya.

  Mahakama hizi mbili ziko katika maeneo ya katikati ya jiji, ikiwa dhamira ya Mahakama ya Tanzania, kuhakikisha kwamba inaboresha huduma za utoaji haki na kusongeza huduma zake karibu na wananchi.

  Mahakama ya Watoto ni Mahakama ambayo imeanzishwa kisheria kwa lengo la kushughulikia kesi maalum zinazohusu watoto.

  Umri ambao Mahakama hiyo mtoto ni mtu aliye na umri wa chini ya 18 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyosema sura ya kwanza, kifungu cha 5.-(1) na ilivyo katika Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake, marekebisho ya mwaka 2006.

  Mahakama hii inashughulikia makosa mbalimbali ambayo yanaweza kufanywa na watoto kama shuleni, mitaani na sehemu nyinginezo.

  Kuna mambo mbalimbali ambayo pia Mahakama hii inayashughulikia mfano vile taratibu za kuasili watoto na mambo ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na mchakato mzima wa kufanya hivyo, ikiwemo kupokea mashauri ya madai.

  Usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hii, hufanyika faragha. Lengo la usikilizaji wa mashauri haya kusikilizwa kwa siri ni kulinda maslahi ya mtoto.

  Hivyo jamii inapaswa kuzifahamu haki za mtoto kama vile haki ya kuishi, kupata huduma bora za afya, mahali pa kuishi.kupata elimu, haki ya kutambuliwa, haki ya kurithi mali, haki ya kutonyanyaswa, ikiwemo kutofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

  Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba Nkinga, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Ukeketaji,iliyofanyika Desemba 5, mwaka jana, Sihaba Nkinga, alisema hali bado ni mbaya.

  Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba taarifa zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu wa kike na mtoto mmoja wa kati ya saba wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono.

  Kupitia maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, Bi Zainabu Issa ametaka jamii ipige vita vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ili kuwawezesha kufikia ndoto zao ikiwa ni hatua ya kuwawezesha ustawi wa maisha yao na hatimaye kulijenga taifa la kesho.

  “Ninasema kesi dhidi ya ukatili wa watoto sasa zisizidi miezi sita au mwaka, kesi zisikae, muda mrefu Mahakamani.Ninasema sasa mtu akipatikana na hatia ya kuumpa ujauzito mwanafunzi au kubaka afungwe miaka 30 jela,” alisema Mkuu huyo wa wilaya wakati siku ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Mkoani Tanga, wilaya ya Pangani.

  Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Appi akizungumza maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, alipiga marufuku vitendo vya baadhi ya walimu kuwafungia mageti wanafunzi wanapochelewa kufika mashuleni kwa kuwa vinaweza kuwasababishia watoto kujiunga na makundi yenye tabia hatarishi.

  Alisema ili kuweza kuwaepusha watoto kutoathiriwa na tabia hatarishi, Mkuu huyo alipendekeza walimu watumie adhabu mbadala pale baadhi ya wanafunzi wanapofanya makosa wakiwa mashuleni.

  Alisema adhabu mbadala zinaweza kutolewa na walimu, wakati wa kipindi cha mapunziko.

  Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mjini Mbeya, Mhe. Onesmo Zunda akizungumzia kuhusu uzoefu wa usikilizaji kesi za watoto zinazohusiana na madai alisema amekuwa akisikiliza kesi za ndoa na talaka nyingi kutoka vijijini kuliko mjini.

  “Kuna changamoto katika kusikiliza kesi hizi. Miongoni mwa changamoto tunazokabiliana hizo ni mgawanyo wa mali hasa pale inapotoa mtu anapokuwa amefariki dunia au wazazi kutengana mmojawapo akiwa ana fedha au mali au kaoa mke mwingine. Nyingi hivyo mgawanyo wa mali huwa unaleta malalamiko katika baadhi ya familia,” alisema Mhe. Zunda.

  Alifafanua kwamba katika kesi hizo ni Baba anapotaka kubaki na watoto halafu mama hataki. Hata hivyo anasema Mara nyingi mama huwa anataka kubakia na watoto, lakini baba hataki kutokana na tabia ya mama.

  “Hivyo tunatumia sheria pale ndoa inapotaka kuvunjika tunachoangalia zaidi ni maslahi ya mtoto hata kama mtoto ana umri wa zaidi ya miaka 7,” anasititiza Mhe. Zunda.

  Akitolea mfano wa kesi mojawapo, ambapo alisema alitoa maamuzi kwamba mtoto abaki kwa baba kwa sababu mama alikuwa na tabia ya ulevi. Alisema uamuzi huo kwa mujibu wa shuhuda za watoto.

  Ingawa kulingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni jukumu la baba kuwapa watoto matunzo japo jukumu la kuwalea watoto ni la wazazi wote. Hatahivyo, mwanamke anatakiwa achangie katika kuhudumia watoto. Iwapo wazazi wametengana amri ya matunzo hutolewa na Mahakama ili baba asiyeishi na mtoto.

  Matunzo hayo huwa ni pamoja na kutoa nguo, chakula, kugharamia masomo shuleni na matunzo yataendelea hadi kufikia umri wa miaka 18.

  “Licha ya changamoto tunazozipitia tunajitahidi kuzitatua kwa kutumia sheria ,hakuna rufaa zinazofunguliwa,”alisema Mhe. Zunda.

  Mhe. Zunda alizitaja takwimu za kesi za ndoa na talaka walizozipokea kwa kipindi cha mwaka huu yaani Januari hadi Machi 23,mwaka huu, kuwa 26 na hivyo kati ya hizo 11 bado zinaendelea kushughulikiwa na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi.

  Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa, Mhe. Happiness Chuwa, alisema ili kukabiliana na tatizo la kesi zinazo husiana na watoto ni vema jamii ikiwa ina tabia ya kuwatambulisha watoto na kuandika wosia.

  Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, iliyopo eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Devotha Kissoka, akizungumza wakati wa Wiki ya Sheria iliyofanyika mwaka huu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, alisema mtoto akikosa anaweza kupelekwa katika makao ya watoto.

  Ikiwa kuna tatizo, ambalo limeleta mabishano kuhusu mtoto baba yake au wazazi wake ni wakina nani? Mahakama hiyo inatoa amri Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya utambuzi (DNA testing).

  Alizitaja takwimu zinazohusu kesi za madai katika Mahakama hiyo za kipindi cha mwaka 2016 ni 154 na katika kipindi cha mwaka 2015 zilikuwa kesi 19.

  Hakimu huyo alifafanua kwamba sababu ya kuongezeka kwa kesi hizo ni hali ya uchumi, hivyo hali hiyo imetokea kwa watoto walio nje ya ndoa.

  Alisema Mahakama hiyo, pia huwa inasikiliza kesi za jinai mfano wizi wa kutumia silaha, kujeruhi na kuua.

  Mhe. Kissoka aliongeza kwamba ieleweke kwa mujibu wa Sheria, mtoto aliyechini ya umri wa miaka kumi hawezi kutenda kosa la jinai.

  Desemba 5, mwaka huu Tanzania iliazimisha Maadhimsho ya Kupiga Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto, mfano kufanyishwa kazi ngumu, kubaka na kuolewa chini ya umri mdogo, au kutopewa fursa ya kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.

  Mtoto ana haki ya kupata dhamana katika mashitaka yote isipokuwa yale, ambayo sheria imemtaka hayana dhamana.

  Mhe. Kisoka alizitaja adhabu ambazo hutolewa kwa mtoto, miongoni mwa adhabu hizo ni kuachiwa kwa masharti kwa kipindi fulani, lakini kisizidi miaka mitatu, adhabu ya kulipa faini, adhabu ya kuripoti kwa Afisa Ustawi wa Jamii, adhabu ya kupelekwa katika shule maalum.

  Pamoja na adhabu hizo mahakama ina uwezo wa kutoa amri mbalimbali kama vile kulipa faini, kuachiwa bila masharti yoyote.

  Kutokana na maoni ya watu mbalimbali mfumo mmoja wa kisheria na nguvu za pamoja zitasaidia kupunguza au kutokomeza vitendo vya kikatili na unyanyasaji dhidi ya watoto. Hii inatokana na sababu bado umri wa mtoto bado ni tatizo kwa kuwa mtoto ana weza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 au kuoa wakati huohuo mtu anaitwa mtoto akiwa na umri chini ya miaka 18.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MAHAKAMA YA WATOTO SULUHISHO LA KESI ZA WATOTO Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top