728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, March 24, 2017

  Watanzania kunufaika na gesi asilia

  Benjamin Sawe-Maelezo

  Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema mpaka kufikia mwaka 2020 litawawezesha watanzania kutumia gesi majumbani mwao hivyo kupelekea upungufu wa uharibifu wa mazingira nchini.

  Kaimu Mkurugenzi wa TPDC Eng. Kapuulya Musomba amesema muda mrefu kumekuwa na uharibifu wa mazingira hivyo kupatikana kwa nishati ya mafuta na gesi kutaiwezesha Tanzania kuwa mahali salama kimazingira ikiwa ni pamoja na ukuaji wa sekta ya uchumi.

  Alisema katika robo ya pili ya mwaka 2017 shirika limekamilisha usambazaji wa mabomba ya gesi kwa matumizi ya majumbani jijini Dar es Salaam na zaidi ya viwanda 300 vimeunganishwa na nishati ya gesi hapa nchini hivyo kupelekea upatikanaji wa umeme wa uhakika.

  Kuhusu upangaji wa Bei kwa matumizi ya gesi itakayosambazwa majumbani Eng. Musomba amesema Taasisi yake itashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura), kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu.

  Hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya umeme uliopo katika Gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia hivyo mipango ya Serikali ni kulifanya Shirika hilo kuchangia zaidi mapato Serikalini yanayotokana na rasilimali hiyo.Alisema Eng. Musomba

  Alisema TPDC imejipanga kuwekeza kwenye shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi ili Taifa linufaike na rasilimali hiyo.

  Akitolea mfano mradi mkubwa wa kusindika gesi asilia (Liqufied Natural Gas-LNG), Eng. Musomba alifafanua kwamba itachukua takribani miaka 8 hadi 10 kabla ya mzigo wa kwanza wa LNG kusafirishwa kwenda katika soko la dunia kwa mauzo.

  Alisema kukamilika kwa mradi wa (Liqufied Naturla Gas- LNG)utakuwa ni fursa kwa watanzania kupata ajira katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kuchangia pato la mwananchi,wawekezaji na Taifa kwa ujumla.

  Alisema uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi ni wa gharama kubwa na hata mafaniko kwa maana ya mapato makubwa kwa Serikali huchukua muda mrefu kuonekana hivyo amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuilinda miundombinu inayopita maeneo yao.

  TPDC inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ikiwa na lengo la kuongeza uelewa zaidi katika sekta hiyo ya gesi na mafuta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Watanzania kunufaika na gesi asilia Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top