728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, March 29, 2017

  WANAOPEWA MIKOPO NA SERIKALI WAKUMBUSHWA KUPELEKA MAREJESHO KWA WAKATI

            Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
  Wanawake na vijana wanaopewa mikopo na Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro wamekumbushwa kupeleka marejesho kwa wakati ili kuwapa fursa na wananchi wengine kupata mikopo hiyo.

  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Christopher Msimbe ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu nafasi ya vijana walemavu waliomaliza mafunzo kupitia Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International.

  Msimbe amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali, Halmashauri inatambua nafasi ya vijana katika jamii hasa vijana wenye ulemavu na ndio sababu wanawakumbuka katika fursa nyingi zinazokuja katika Halmashauri hiyo kutoka kwa wadau  mbalimbali.

  “Katika Halmashauri yetu tumebahatika kupata mradi wa YEE unaowashirikisha hata vijana wenye ulemavu, mradi huo unalenga kuwapatia mafunzo ya ufundi vijana ili waweze kujitegemea hivyo sisi kama Serikali tumetoa jumla ya shilingi 4,000,000 kwa vikundi viwili vya vijana wenye ulemavu ili waweze kuinua shughuli zao,”alisema Msimbe.

  Amefafanua kuwa Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo vijana na wanawake ili kuwasaidia kujikwamua kimaisha kwa kuendelezea biashara zao lakini asilimia kubwa wamekuwa hawapeleki marejesho kwa wakati na kusababisha Halmashauri kushindwa kutoa mikopo kwa watu wengine.

  Nae, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiungwile “A” iliyopo wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Sama amesema mradi huo umewasaidia vijana wengi kwa sababu kabla ya mradi huo vijana walikuwa wakizurura mitaani bila kazi yoyote pia vijana walemavu walikuwa wakikaa ndani bila kujua hatima yao.

  “Mtaani kwangu nina vijana watano waliopewa mafunzo na shirika hili ambao wamefanikiwa kuunda kikundi chao kijulikanacho kama ‘Baraka Farmers Group’ ambacho kinatumia elimu waliyoipata pamoja na mkopo wa shilingi 1,500,000 kutoka katika Halmashauri yetu kujiendeleza kiuchumi, nawashkuru vijana hawa kwani wanatumia vizuri fursa waliyopewa na kurejesha fedha walizokopeshwa kwa wakati,”alisema Sama.

  Sama ametoa rai kwa wananchi wanaopewa mikopo na Serikali hasa wananchi wasio na ulemavu ambao wanaweza kufanya kazi kwa uhakika kurejesha fedha za mikopo kwa wakati ili Halmashauri iweze kuendelea kuwasaidia wananchi wengine na watakaokaidi watachukuliwa hatua stahiki ili warudishe fedha hizo.
  Mradi huo wa miaka mitatu umeanza mwaka 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: WANAOPEWA MIKOPO NA SERIKALI WAKUMBUSHWA KUPELEKA MAREJESHO KWA WAKATI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top