Wananchi wakitoa maoni kwa wataalamu kutoka TGDC na TANESCO wakati wa mkutano wa kujadili athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kweye mazingira na kwa jamii.
Mtaalamu wa Sosholojia Bi. Vaileth Kimaro akizungumza na vikundi vya wanawake wakati wa kujibu maswali na kupokea maoni kuhusu athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii na mazingira.
Mhandisi Leonard Masanja (aliyesimama kushoto) akijibu hoja za wananchi wa Kata ya Ndanto wakati wa mjadala wa athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii na mazingira, aliyeshika kipaza sauti ni Afisa Maendelea ya Jamii wa Wilaya ya Rungwe Bi. Rachel Mbelwa
Na Johary Kachwamba -TGDC
Wananchi
wa Wilaya za Rungwe na Mbeya Vijijini pamoja na wadau wengine wa mradi
wa jotoardhi wa Ngozi wametoa maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuuliza maswali ya msingi kabla ya zoezi la uchorongaji visima vya
uchunguzi na baadae uvunaji mvuke wa kuzalisha umeme utakaotokana na
nishati ya jotoardhi.
Wananchi
walipata fursa ya kutoa maoni yao kati ya tarehe 6 hadi 11 Machi, 2017,
wakati timu ya wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka Kampuni ya
kuendeleza Jotoardhi Tanzania (TGDC) na TANESCO walipotembelea eneo la
mradi, ikiwa ni matakwa ya kisheria ya kushirikisha wadau na jamii
itakayopitiwa na mradi husika, wakati wa kufanya tathmini ya athari za
mradi katika mazingira na jamii.
Maoni
yao ilikuwa ni pamoja na kuiomba Serikali kusimamia taratibu za ajira
wakati wa zoezi la uchorongaji visima vya jotoardhi, akizungumza Ndugu
Yohana Julius wa Kata ya Swaya Vijijini alisema “wanaomba ajira
zisizohitaji ujuzi wapatiwe wakazi wa eneo la mradi ili wanufaike moja
kwa moja kwa kujiongezea kipato”
Bibi
Mary Gwamaka alisema “wanaomba mradi huu usiwaache nyuma wakina mama,
kwani wanao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali, hivyo wanaomba
wasibaguliwe” Akijibu moja ya maswali ya wananchi, Mhandisi wa Mazingira
kutoka TANESCO Bw. Fikirini Mtandika alisema sheria na taratibu zote za
mazingira zitazingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa mradi chini ya
usimamizi wa Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja
na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira.
“TGDC
inaandaa mikakati mbalimbali ya kupunguza na kuziondoa kabisa baadhi ya
athari za mradi huu katika mazingira yetu” aliongezea Mhandisi
Mtandika.
Wananchi
wa maeneo yote yanayozunguka mradi wa jotoardhi wa Ngozi wameridhia
hatua ya uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uzalishaji umeme na
wako tayari kutoa ushirikiano. Kata zinazopitiwa na mradi huu ni Ijombe,
Swaya-Mbeya vijijini, Swaya Rungwe na Ndanto.
0 comments:
Post a Comment