728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, March 23, 2017

  RC MOROGORO ATOA RAI KWA VIJANA KUUNDA VIKUNDI

  Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kebwe S. Kebwe ametoa rai kwa vijana kujiweka katika vikundi ili wapate fursa za kupata mikopo kutoka Serikalini na kwa wadau mbalimbali. 

  Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo leo mkoani Morogoro alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya maendeleo ya vijana wenye ulemavu waliopo chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na shirika la Plan International.

  Mhe. Kebwe amesema suala la vijana na wanawake kuunda vikundi ni la muhimu kwani Serikali kupitia Halmashauri zote nchini ina utaratibu wa kutenga asilimia kumi kutoka katika mapato ya ndani ya Halmashauri husika kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na vijana ili waweze kujikwamua hasa katika nyanja ya kiuchumi.

  “Serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu hivyo kupata mradi kama huu wa kuwasaidia vijana kiuchumi kutoka Umoja wa Ulaya ni fursa nzuri kwa vijana kujikomboa na njia rahisi ya kuoneka mna uhitaji ni dhahiri kuwa mnatakiwa muwe katika vikundi,”alisema Mhe. Kebwe.

  Mhe. Kebwe ameongeza, uundwaji wa vikundi unasaidia kufahamu ukubwa wa kikundi, kiasi cha msaada, eneo kikundi kilipo na aina ya shughuli inayofanywa na kikundi husika.

  Amefafanua kuwa kwa hali halisi fedha za mradi haziwezi kutolewa kwa mtu mmoja mmoja bali ni kwa njia ya vikundi ili kurahisisha ufatiliaji na kupunguza gharama za uendeshaji hivyo vijana wasitarajie kupata mkopo au kusaidiwa na shirika wakiwa wamekaa vijiweni.

  Aidha,amewasisitiza vijana hasa walemavu kujitokeza kwa wingi katika awamu ya mwisho ya mradi huo kwani mradi huo upo kwa ajili ya vijana wote.

  Mradi huo wa miaka mitatu (2015/2018) unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: RC MOROGORO ATOA RAI KWA VIJANA KUUNDA VIKUNDI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top