728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, March 28, 2017

  MAHAKAMA KUU TANGA YAWEKA MIKAKATI KUONDOSHA MASHAURI KWA WAKATI

  Na Lydia Churi- Mahakama, Tanga

  Mahakama Kuu Kanda ya Tanga inakusudia kuwanunulia Mahakimu wake 67 kompyuta Mpakato (Laptops) ili kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika Mahakama mbambali za mkoa wa Tanga.

  Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Bwana Farid Mnyamike amesema kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa Mahakimu katika kuandika hukumu ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati.

  Alisema katika kanda yake, baadhi ya Mahakama zina uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu pamoja na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa Mahakimu kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.

  Aidha, Afisa Utumishi huyo alisema hivi sasa Mahakama Kuu kanda ya Tanga inao mpango wa kuhakikisha inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa Umeme vijijini (REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati.

  Mahakama ya Tanzania ilimwekea malengo kila Hakimu nchini ya kuhakikisha anasikiliza kesi zaidi ya 250 kwa mwaka ili kuondosha mrundikano wa mashauri yaliyoko kwenye Mahakama mbalimbali nchini.

  Bwana Mnyamike aliitaja mipango mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania kuwa ni kuwapeleka Mahakimu wenye mashauri machache kwenye Mahakama zenye mashauri mengi ili kuhakikisha mashauri yote ya muda mrefu yanaondoshwa na yaliyofunguliwa yanamalizika kwa wakati.

  Ili kuleta mabadiliko ndani ya Mahakama, Mahakama ya Tanzania iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2015-2020 unaotekelezwa kupitia nguzo tatu ambazo ni Utawala bora, Upatikanaji wa Haki kwa Wakati na pamoja na kurudisha na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MAHAKAMA KUU TANGA YAWEKA MIKAKATI KUONDOSHA MASHAURI KWA WAKATI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top