728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, November 10, 2016

  RAIS DKT. MAGUFULI AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MWILI WA MZEE JOSEPH MUNGAI JIJINI DAR LEO


   Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima zake za mwisho kwa  mwili wa aliyekuwa Waziri wa Zamani na Mbunge Mzee Joseph Mungai katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam leo Novemba 10, 2016

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 10 Novemba, 2016 amewaongoza viongozi na wananchi wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa Waziri na mbunge Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph James Mungai katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.

  Pamoja na Rais Magufuli Viongozi wengine waliofika kuuaga mwili wa Marehemu Mungai ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Tluway Sumaye, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Viongozi wengine mbalimbali wa Serikali na Siasa.

  Mhe. Joseph James Mungai alifariki dunia tarehe 08 Novemba, 2016 katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua ghafla na mwili wake utasafirishwa kesho Ijumaa kwenda Mafinga Mkoani Iringa kwa Mazishi.

  Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Sewahaji iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam wakiwemo Waziri na Balozi Mstaafu wa Tanzania Mhe. Omar Ramadhan Mapuri na Mkewe Mama Janeth Magufuli.

  Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo wamemshukuru Rais Magufuli kwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kuboresha hospitali ya Taifa Muhimbili na wamebainisha kuwa licha ya kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali pia wanapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na wauguzi.

  Mapema leo asubuhi, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mfadhili wa Taasisi ya Gatsby Tanzania Lord Sir David Sansburg na kumuhakikishia kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza kilimo, wajasiriamali na viwanda ambazo zinafanywa na Taasisi hiyo.

  Dkt. Magufuli amesema atafurahi kuona Taasisi hiyo ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima wa pamba na chai kupata mbegu bora na kusindika mazao yao, inapiga hatua zaidi kwa kuanzisha viwanda vya nguo na kwamba Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo.

  Gerson Msigwa
  Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
  Dar es Salaam
  10 Novemba, 2016

  Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimpa pole mjane wa Marehemu Mzee Joseph Mungai.
  Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin Mkapa akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mzee Joseph Mungai, aliewahi kuwa Waziri katika Wizara mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuanzia Awamu ya kwanza mpaka ya nne, ulioagwa leo katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es salaam.
  Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed Gharib Bilal akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mzee Joseph Mungai, aliewahi kuwa Waziri katika Wizara mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuanzia Awamu ya kwanza mpaka ya nne, ulioagwa leo katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es salaam.
  Rais Dkt. John Pombe Magufuli (wa nne kushoto), Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin Mkapa (wa tatu kushoto), Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed Gharib Bilal (wa tatu kulia), Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye (kushoto), Mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mama Salma Kikwete (kulia) pamoja na viongozi wengine wakifatilia wasifu wa Marehemu Mzee Mungai, uliokuwa ukisomwa na Mtoto wake Mkubwa, Jimmy Mungai.
   Sehemu ya familia ya aliyekuwa Waziri wa Zamani na Mbunge Mzee Joseph Mungai katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemy katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam  leo Novemba 10, 2016

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: RAIS DKT. MAGUFULI AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MWILI WA MZEE JOSEPH MUNGAI JIJINI DAR LEO Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top