728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, November 17, 2016

  Muhimbili Yaadhimisha Siku ya Watoto Njiti Dunia

  Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji, Dk Julieth Magandi akikabidhi cheti kwa Mary Kundi, mkazi wa Dar es Salaam baada ya kufuzu kumtunza mtoto wake aliyezaliwa kabla ya wakati (njiti). 

  Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Julieth Magandi akizungumza katika siku ya watoto njiti duniani ambayo inafanyika Novemba 17, kila mwaka. Kulia ni Mwanzilishi wa Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali hiyo, Dk Agustino Massawe na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Watoto Njiti wa hospitali hiyo, Dk Edna Majaliwa. Maadhimisho hayo yamefanyika Leo katika Jengo la Watoto katika hospitali hiyo.
  Mkuu wa Kitengo cha Watoto Njiti wa hospitali hiyo, Dk Edna Majaliwa akizungumza kwenye mkutano huo Leo. 


  Kinamama walioudhuria siku ya watoto njiti duniani wakiwa katika picha ya pamoja Leo katika Jengo la Watoto lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Kaimu.


  Na John Stephen, MNH


  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo imeadhimisha siku ya watoto njiti duniani, huku hospitali hiyo ikiwa imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto kutoka asilimia 28.8 mwaka 2014/2015 mpaka kufikia asilimia 19.8 2015/2016. Vifo vimepungua kutokana na juhudi zinazofanywa na wataalamu wa hospitali hiyo wakiwamo madaktari na wauguzi.

  Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji, Dkt. Julith Magandi akisoma hutuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru amesema kwamba Kitengo cha Kangaroo kimekuwa kikipokea watoto wenye uzito wa gramu 700 hadi gramu 1500 na kufanikiwa kuwatunza watoto hao na asilimia 99.5 wameruhusiwa na kurejea nyumbani. “Kumekuwapo kwa ungezeko kubwa la uzito kwa watoto ikiwa ni gramu 10-30 kila siku ikilinganishwa na wale wanaotunzwa kwenye incubator,” amesema Dk Magandi.

  Dk Magandi amesema mpango huo umefanikiwa kupunguza msongamano wa watoto katika wodi ya watoto wachanga wanaolazwa kwenye chumba chenye incubator kwa asilimia kubwa.

  Amesema kutokana na uwezo mkubwa wa kuwatunza watoto njiti, kitengo cha Kangaroo kimefanikiwa kuwatunza watoto njiti kutoka 30 mwaka 2012 hadi kufikia 1500 mwaka 2015/2016. Mkurugenzi huyo amesema kitengo hicho kitaendelea kutoa huduma bora ili kuhakikisha watoto njiti wanaruhusiwa kwenda nyumbani wakiwa na uzito uliokubalika kitaalamu.

  “Kitengo cha Kangaroo kitaendelea kufuatilia matunzo ya watoto njiti wanaokaa nje ya Jiji la Dar es Salaam. Tutaendelea kutumia mfumo wa tracking system kwa kutumia simu (by phone referral system) na kutumia mfumo mzuri wa kuwapa rufaa kutoka kitengo kimoja hadi kitengo kingine kwa kutumia sera za hospitali na zile za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,” amesema Dk Magandi.

  Akizungumzia manufaa ya huduma za kitengo cha Kangaroo, Dk Magandi amesema watoto njiti wanapaswa kutunzwa vizuri kwani baada ya kuzaliwa wanahitaji uangalizi wa hali ya juu, ikiwamo kupata joto na kuwasaidia kupumua.

  “Kwa vile watoto wanaozaliwa njiti mapafu yao yanakuwa hayajakomaa wanahitaji kusaidiwa ili waweze kuishi,” amesema. Amesema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili itaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha inatoa huduma bora za watoto wachanga ikiwamo kutoa huduma kwa kiwango cha ubobezi kwa watoto wachanga.

  “Kwa sasa tumeweza kufanikisha kwa mara ya kwanza kupatikana kwa dawa ya kukomaza mapafu kwa watoto waliozaliwa njiti kwa watoto waliolazwa katika wodi ya wachanga,” amesema. Amesema hospitali hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamefanikiwa kupata mashine 10 za kupumulia watoto wachanga.

  “Tunatoa wito kwa Wizara ya Afya Maendeleao ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kuongeza vitengo vya kutunza watoto njiti ikiwemo huduma ya kangaroo ambayo ni muhimu sana kwa kupunguza vifo vya watoto wachanga na hii ni huduma ya gharama nafuu haihitaji utaalamu wa hali ya juu na vifaa wala vifaa tiba vya gharama kubwa,” amesema Dk Magandi. Kinamama 28 leo wamekabidhiwa vyeti baada ya kufuzu kumtunza mtoto wake aliyezaliwa kabla ya wakati (njiti).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Muhimbili Yaadhimisha Siku ya Watoto Njiti Dunia Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top