728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, November 17, 2016

  Mashindano ya Ma-DJ Jijini Dares Salaam kuhamasisha upandaji miti


  Na. Lilian Lundo - MAELEZO


  Chama cha Muziki wa Disco Tanzania (TDMA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wameandaa mashindano ya Ma-DJ ngazi ya Mkoa yanayolenga kuhamasisha wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na vitongoji vyake kupanda miti na kutunza mazingira.

  Katibu Mkuu wa chama hicho Asanterabbi Mtaki ameyasema hayo, leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa mashindano hayo yanayotajiwa kuzinduliwa Ijumaa Novemba 18, 2016 katika ukumbi wa JM Night Club uliopo Tiptop Manzese.

  “Mashindano ya Ma-DJ kwa mwaka 2016 yana lengo la kuwahamasisha wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na vitongoji vyake kupanda miti, maua pamoja na kuyatunza mazingira yanayowazunguka kwa kuyaweka katika haili ya usafi, usalama na ya kuvutia ili kuuweka Mkoa wa Dar es Salaam katika madhari nzuri na ya kupendeza,” alifafanua Mtaki.

  Aliendelea kwa kusema kuwa, mashindano hayo yatakuwa na raundi tatu za mtoano ambapo raundi ya kwanza itafanyika tarehe 18, ya pili tarehe 25 na ya tatu tarehe 2 mwezi wa 12 ambayo ndiyo itakayowapata washindi watakaoingia robo fainali.Hivyo basi, mashindano hayo yatawakutanisha Ma-DJ mahiri toka wilaya za Temeke, Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kigamboni.

  Aidha mashindano hayo yatawawezesha Ma-DJ chipukizi kujitambua kuwa ni sehemu ya kundi muhimu katika jamii ya Watanzania kutokana na shughuli wanayoifanya ya kuchezesha muziki ambayo ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwenye mikusanyiko ya jamii ya wapenzi wa muziki.

  Vigezo vya mashindano hayo ni nidhamu, unadhifu, umahiri wa kuchezesha nyimbo na kuzichanganya, kulitawala jukwa la DJ pamoja na kuonyesha kazi za kutumia mikono (handswork).DJ wa kwanza atazawadiwa shilingi 500,000, wa pili shilingi 300,000 na wa watatu shiingi 200,000 ambapo zawadi zote hizo zimedhaminiwa na JM Hotel ya jijini Dar es Salaam.

  Mgeni rasmi wa mashindano hayo anatarajiwa kuwa Afisa Michezo wa Mkoa wa Dar es Salaam Adorph Halii.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Mashindano ya Ma-DJ Jijini Dares Salaam kuhamasisha upandaji miti Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top