728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, November 8, 2016

  HIMIZENI WAWEKEZAJI KUTOKA UINGEREZA – MAJALIWA

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Mheshimiwa Sarah Cooke, ofisini kwake bungeni mjini Dodoma Novemba 8, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

  …………………………………………

  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Uingereza ihamasishe wawekezaji zaidi kutoka nchini humo ili waje kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.

  Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Novemba 8, 2016) wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Bibi Sarah Cooke alipokutana naye ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma.

  “Mheshimiwa Balozi utusaidie kualika wawekezaji wengi zaidi kwenye maeneo ya kilimo, viwanda vya usindikaji mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, sekta ya mafuta na gesi, nishati na ujenzi wa makazi hasa kwa mkoa wa Dodoma ambako hivi sasa ni Makao Makuu ya Serikali,” amesema.

  Amemweleza Balozi huyo kwamba Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati na hivyo imejipanga kuwa na viwanda vya kutosha ili iweze kusindika mazao yake hapa nchini na itoe ajira kwa wananchi wake.

  Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo pia kuishukuru Serikali ya Uingereza kwa msaada wake mkubwa wa ujenzi wa nyumba za walimu na shule mkoani Kagera zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.

  Kwa upande wake, Balozi Cooke ambaye alifika kujitambulisha rasmi, amesema ameguswa na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na masuala ya ufisadi na rushwa. “Kaulimbiu yenu kwamba rushwa haikubaliki (zero tolerance on corruption) inaonyesha jinsi mlivyodhamiria kupambana na baa hili,” amesema.

  Amesema Uingereza inaongoza miongoni mwa nchi zenye wawekezaji wengi hapa nchini na kwamba inaendeleza mpango wake wa uwekezaji ambao unalenga maeneo makuu manne ambayo ni gesi na mafuta; kilimo; nishati jadidifu na uimarishwaji wa mazingira ya kufanya biashara.

  Balozi Cooke alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Serikali kutokana na msiba wa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo, Tabora, Mheshimiwa Samwel Sitta kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 7, mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: HIMIZENI WAWEKEZAJI KUTOKA UINGEREZA – MAJALIWA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top