728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, November 18, 2016

  HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI YAHOFU KUTOWEKA KWA BAADHI YA WANYAMA ADIMU KUFUATIA WANYAMA WENGI KUGONGWA NA MAGARI

   Waandishi wa habari  wanawake kutoka Mikoa mbalimbali wakimsikiliza Ofisa wa Tanapa Abdallah Choma akiwapa maelezo juu ya hifadhi ya Mikumi
   Mkuu wa hifadhi ya Mikumi Donat Mnyagatwa akiongea na waandishi wa habari wanawake waliofanya ziara katika hifadhi ya mikumi
  Baadhi ya vivutio vilivyopo katika hifadhi ya Mikumi

  Na Editha Karlo wa blog ya jamii,Mikumi.

  HIFADHI ya Taifa ya Mikumi imeelezea hofu yake ya kutoweka kwa baadhi ya wanyama adimu katika hifadhi hiyo kutokana na kasi ya kuuwawa kwa kugongwa na magari ya abiria, binafsi, mizigo yanayopita bara bara ya kutoka dar es salaam na kwenda nyanda za juu kusini iliyopo ndani ya hifadhi hiyo.

  Uwepo wa barabara ya lami inayopita katikati hifadhi hiyo na kuongeza kasi ya kugongwa wanyama kila mwaka huku na kutia hofu ya kutoweka kwa baadhi ya wanyama adimu iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

  Hofu hiyo inatokana na takwimu zinazoonyesha kuwa wastani wa mnyama mmoja anagongwa kila siku huku pia zikionyesha kuwa kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita hadi kufikia mwaka 2015 wanyama wa aina mbalimbali zaidi ya 3,435 walikufa kwa kugongwa na magari.

  Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya mikumi , Donat Mnyagatwa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari wanawake waliotembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kuitangaza zaidi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku kumi katika hifadhi za taifa za Saadan, Mikumi, Udzungwa na Ruaha mkoani Iringa.

  Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo wanyama waliogongwa kuazia mwaka 1992 walikuwa 72 idadi ambayo imekuwa ikingezeka kwa kasi kila mwaka ambapo kwa kipindi cha mwaka jana 2015 wanyama wa aina mbalimbali waliogongwa na kufa ni 237.

  Hata hivyo Mnyagatwa alitaja takwimu za miaka tisa iliyopita ikianzia na mwaka 2007 waliokufa kwa kugongwa ni wanyama 43, 2008 wanyama 82, 2009 wanyama 45, 2010 wanyama 19, 2011 wanyama 125, 2012 wanyama 111, 2013 132 na mwaka 2014 wanyama 351.

  “Hifadhi hii ina ukubwa wa Kilomita za mraba 3230 lakini barabara imepita Km 50 ndani ya hifadhi inaweza kukadiriwa ama kuonekana ni jambo dogo lakini lina athari kubwa mno kwani tunaweza kupoteza baadhi ya aina ya wanyama kutokana na ongezeko la kasi la kufa kwao kutolingana na kasi ya kuzaliana”alisema.

  Aidha mhifadhi Mnyagatwa alitaja changamoto nyingine za uwepo barabara hiyo kuwa ni pamoja na hifadhi hiyo kupoteza mamilioni ya fedha kwa kufa wanyama, uchafuzi wa mazingira pamoja na kufanyika utalii wa bure ambao unapoteza mapato mengi ya serikali .

  "Ndugu zangu waandishi wa habari tunaomba sana mtusaidie hili suala la changamoto ya barabara hili ni tatizo kubwa hivyo tunaamini kuwa mtasaidia katika hili "alisema Mhifadhi Mkuu huyo.

  Alitaja chanagamoto nyingine ni pamoja na ujangili, kuzuka kwa moto, kubadili tabia za wanyama kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiwarushia wanyama matunda na vyakula vya binadamu na kuota kwa mazao ya biashara yanayosafirishwa kupitia barabara hiyo yanapomwagika ndani ya hifadhi hiyo.

  Alisema kuwa baadhi ya madereva nyakati za usiku wamekuwa wakigiiza kuharibika kwa magari katikati ya hifadhi ili waweze kufanya ujangili .

  Akizungumzia kuhusu kutoweka kwa wanyama kipindi cha masika Mhifadhi utalii wa hifadhi ya Mikumi ,Abdalah choma alisema kuwa kipindi kizuri cha kutembelea hifadhi hiyo ni kipindi cha masika ambacho wanyama wengi hujikusanya sehemu moja katika hifadhi hiyo hivyo kutoa fursa kwa watalii kuona wanyama wengi hasa nyakati za asubuhi na jioni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI YAHOFU KUTOWEKA KWA BAADHI YA WANYAMA ADIMU KUFUATIA WANYAMA WENGI KUGONGWA NA MAGARI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top