728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, November 8, 2016

  DIPLOMASIA YAHARAKISHA UKUAJI WA MAENDELEO NCHINI KATIKA MWAKA MMOJA YA JPM MADARAKANI  NA. Immaculate Makilika- MAELEZO

  Kwa mujibu wa mtandao wa wikipedia diplomasia ni taratibu zinazoratibu mahusiano katika ngazi ya kimataifa kati ya nchi na nchi au nafasi za kisheria nyingine zenye hadhi ya kimataifa, aidha mtandao huu unaendelea kusema kuwa diplomasia ianaratibu majadiliano baina ya nchi moja na nyingine hasa pale nchi mbili au zaidi zikipigana, diplomasia husaidia kusimamisha vita, sambamba na mazunghumzo yanayohusu masuala ya haki, na amani.

  Miaka ya hivi karibuni diplomasia inatumika pia kwa masuala ya biashara, uchumi na utamaduni pale nchi zinazoposaini mikataba fulani ya ushirikiano katika masuala mbalimbali, ambayo huitwa diplomasi ya uchumi.

  Katika kipindi cha mwaka mmoja cha utawala wa Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumeshuhudia ugeni wa viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani, ni dhahiri kuwa hayo yote yanafanyika ili kuhakikisha diplomasia inatumika katika kuleta ama kuharakisha maendeleo hapa nchini.

  Oktoba 23 hadi 30 mwaka huu Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco alifanya ziara ya kikazi ya siku nne nchini, kwa lengo la kukuza uhusiano wa kidiplomasia kati ya Morocco na Tanzania , ambapo ilisainiwa mikataba 21 ya ushirikiano baina ya nchi hizo, inayolenga kuboresha sekta za uchumi na teknolojia. 

  Mikataba hiyo ni pamoja na makubaliano ya jumla katika ushirikiano wa uchumi, sayansi, ufundi, na utamaduni iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mheshimiwa Salahddine Mezouar

  Mwingine ni ule wa kuanzishwa kwa Jukwaa la Mashauriano ya kisiasa baina ya Wizara ya Mambo ya Nje yaTanzania na Morocco, mkataba wa ushirikiano katika sekta ya gesi, nishati, madini, uvuvi,sayansi ya miamba pamoja na ushirikiano katika usafiri wa anga na kuwasaidia wakulima wadogo nchini kwa kuendeleza soko la mbolea na kilimo kupitia Shirika la Mbolea la Morocco(OCP) na Shirika la Mbolea la Tanzania.

  Kama hiyo haitoshi, ziara hiyo pia ilitia saini mikataba ya makubaliano ya mashirika ya Bima ya Tanzania na Morocco, pamoja na ushirikiano baina ya Bodi ya Utalii Tanzania, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Ofisi ya Utalii ya Taifa nchini Morocco, ambapo Tanzania inatarajiwa kunufaika zaidi kwa kupata utaalamu hasa katika sekta ya utalii kwa vile nchi ya Morocco imekua ikijipatia pato kwa kiasi kikubwa kutokana na sekta hii.

  “Morocco imepiga hatua kubwa kwenye utalii na kwamba mwaka 2015 ilipokea watalii milioni 10.5 na mwakani wanategemea kupokea watalii zaidi ya milioni 14 na kwamba Tanzania imeshasaini makubaliano kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuendeleza hifadhi za nchi na kuutangaza utalii” anasema Rais Magufuli

  Sambamba na hili, mikataba mingine ni kuhusu maeneo maalumu ya uwekezaji (EPZA), uendelezaji na utangazaji wa viwanda, usafirishaji kwenye reli kupitia kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO) kwa ajili ya ubia kuendeleza reli ya Mtwara – Mchuchuma/ Liganga, ambapo nchi hizo mbili kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwenda Rabat, mji mkuu wa nchi hiyo iliyopo kaskazini mwa Afrika.

  Ziara ya Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamhuri ya Cuba nchini, Mheshimiwa Valdes Mesa aliyewasili nchini mapema mwezi Oktoba, ni sababu nyingine inayodhihirisha kuwa namna gani Tanzania imedhamiria kukuza, kuimarisha na kuangalia maeneo mapya ushirikiano yatakayosaidia kuarakisha upatikanaji wa maendeleoa nchini kupitia mwamvuli wa diplomasia.

  Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Cuba ulianzishwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na viongozi Waaisisi wa mataifa haya mawili Rais Mstaafu wa Cuba Mheshimiwa Fidel Castro na Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, ambapo Cuba imekua ikiisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, utamaduni, elimu, michezo,utalii, nishati, teknolojia na kilimo. 

  Ushirikiano huu unajidhihirisha katika jitihada za Serikali hizi mbili za kupambana na malaria, ambapo zimejenga kiwanda cha Viuatilifu vya kuua Viluwiluwi vya mbu kilichopo kwenye eneo la viwanda wilayani Kibaha, mkoani Pwani. Kiwanda hicho kilichokamilika kinazalisha dawa za majaribio, ambacho kitazalisha lita milioni 6 za viuatilifu kwa mwaka zitakazotosheleza matumizi ya Tanzania na hata kuuzwa nchi nyingine za Afrika na pia kinazalisha ajira kwa watanzania.

  Hadi kufikia Oktoba mwaka huu (2016) sekta ya afya nchini imekuwa na jumla ya madaktari 30 kutoka nchini Cuba wanaofanya kazi katika hositali mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar.Katika sekta ya elimu, kumekuwepo na programu mbalimbali ikiwemo nafasi ya ufadhili wa masomo nchni Cuba kwa wanafuzni kutoka Tanzania kuanzia mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya watanzania 64 wamepata ufadhili wa mafunzo nchini humo katika fani mbalimbali ikiwemo udaktari, uchumi, TEHAMa na michezo. 

  Aidha, pamoja na kutumia fursa ya ziara hiyo katika kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili, Tanzania inatazamia kutumia nafasi hii katika kuanzisha mahusiano kwenyue maeneo mapya ya uwekezaji na biashara.
  Kati ya mataifa matatu yanayoongoza kuwa na uwekezaji mkubwa hapa nchini, ni taifa la Uingereza, taifa la China na kisha taifa la India.

  Ukizunguznia ziara ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi inaonesha nia ya wazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kutumia diplomasia ya uchumi.

  Nchi ya India mbali na uwekezaji ambao imefanya, kampuni mbalimbali za nchi hiyo zimetaka kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali. Kwa upande wa sekta ya Afya, kampuni ya Appolo Group kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi ya Jamii ( NSSF) itajenga hospitali ya kisasa katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam itakayotoa huduma za afya kwa wakazi wa jiji na nchi nzima kwa ujumla.

  Serikali ya India imeeleza nia yake ya kuanzisha Viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu zitakazotibu magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini, uanzishwaji wa viwanda hivyo utasaidia kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi ambavyo vinaigharimu Serikali fedha nyingi.

  “Lengo letu ni kusaidiana na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu”, anasema Waziri Mkuu Modi.Modi aliongeza kuwa Serikali ya India inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.

  Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli anasema Serikali ya India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha ajira 54,176.

  Sambamba na hayo, Serikali ya India ilitoa misaada mbalimbali ikiwani pamoja na mashine ya vipimo vya ugonjwa wa saratani katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa Kanda ya Ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.

  Katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza programu mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.

  Ni katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tunaona viongozi wa nchi za kiafrika wanapata fursa ya kutembelea nchini kwa lengo la kukuza, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuleta maendeleo ya nchi husika.

  Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame alifanya ziara ya siku moja Julai mosi mwaka huu ukiwa ni mwendelezo wa uhusiano mzuri baina ya Rwanda na Tanzania.Kati ya mambo yaliyojadiliwa katika ujio huo, ni pamoja na ushirikiano katika masuala ya biashara ambapo nchi ya Rwanda inatumia zaidi bandari ya Dar es Salaam kwa kupitishia mizigo yake huku ikitazamiwa Serikali kupata mapato zaidi kupitia Bandari hiyo.

  Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk Joseph Pombe Magufuli anasema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watafungua ofisi nchini Rwanda ili kurahisisha uhakiki wa bidhaa kwa wafanyabiashara wa Rwanda wanaoingia nchini.

  Ameongeza kuwa Serikali imetoa eneo la bandari kavu (ICD) kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa kutoka nchi ya Rwanda ili kupunguza urasimu ambao umekuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara hapa nchini na kwa namna hiyo biashara itakua kwani tunategemea uchumi utapanda kutoka asilimia 7 ya sasa mpaka asilimia 7.2.

  Pia amesema kuwa Serikali imepunguza vituo vya ukaguzi barabarani kutoka Tanzania kwenda Rwanda kufikia vitatu na kwa kufanya hivyo itarahisisha safari za magari ya biashara njiani na hivyo kufikisha bidhaa kwa haraka.

  Mawaziri wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Tananzia na Rwanda wamesainia muhtasari wa Tume ya Ushirikiano wa pamoja baina ya nchi hizi mbili, aambapo wamekubaliana kujenga reli ya kisasa (standard gauge) kutoka Dar es salaam hadi Kigali itakayokuwa inasafirisha mizigo kutoka Tanzania hadi Rwanda

  Kati ya Marais ama viongozi waliofanya ziara nchini Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa awamu ya Tano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mheshimiwa Joseph Kabange Kabila.

  Kama ilivyo katika ziara nyingine, hii nayo imelenga katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, sambamba na kutumia diplomasia ya uchumi katika kuleta maendleo ya nchi hizi za Tanzania na Kongo.

  Katika mazungumzo yao kati ya Rais John Magufuli na Joseph Kabila yaliyofanyika Oktoba 4, mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam viongozi hao wamekubaliana kushirikiana pamoja na kuendeza uhusiano wa kindugu uliopo baina ya nchi hizo mbili.

  Ambapo, Mheshimiwa Rais Magufuli anasema kuwa takwimu zinaonesha nchi za Tanzania na Kongo zinafanya biashara kwa kiasi kikubwa na kwa mwaka 2009 biashara kati ya Tanzania na Kongo ilifikia shilingi bilioni 23.1 huku ikiendelea kukua mwaka hadi mwaka hadi kufikia thamani ya shilingi bilioni 393.6 kwa mwaka na hivyo anawakaribisha kwa wingi wawekezaji kutoka nchini Kongo.

  Namalizia makala hii kwa kusema kwamba, Rais wa 35 wa nchi ya Marekani Mheshimiwa John F Kennedy alipokuwa akiapishwa kuwa Rais wa taifa hilo mnamo Februari 2, mwaka 1961 huko Washngton DC nchini Marekani aliwahi kusema “ My fellow Americans, ask not what your country can do for you, ask what you can do for you country”

  Usiulize Marekani itakufanyia nini, jiulize utaifanyia nini Marekani, pengine huu ni wakati muafaka sasa kwa watanzania kujiuliza pamoja na juhudi zote hizi za Serikali ya Awamu ya Tano zilizofanywa kwa kipindi cha mwaka mmoja katika kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla ni nini mchango wako kwa Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: DIPLOMASIA YAHARAKISHA UKUAJI WA MAENDELEO NCHINI KATIKA MWAKA MMOJA YA JPM MADARAKANI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top