728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, October 12, 2016

  ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA AFYA YA AKILI DUNIANI

  Muuguzi Mkuu wa Hospital ya wagonjwa wa akili Ruzuna Abdulrahim Mohammed akisoma risala ya wafanyakazi katika madhimisho ya siku ya Afya ya akili Duniani yaliyofanyika Hospitali ya Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar.
  Kaimu Daktari dhamana wa Hospital ya ugonjwa wa akili Dkt. Zena Kassim Moh’d akitoa taarifa fupi kwa Mgeni rasmi kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo na kumkaribisha mgeni rasmi DKT. Mohd Dahoma kwa niaba ya Katibu Mkuu katika madhimisho ya siku ya Afya ya akili Duniani.
  Mgeni rasmin Mkurugenzi wa huduma za Hospitali Dkt. Muhammed Dahoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya akihutubia katika madhimisho ya siku ya Afya ya akili Duniani yaliyofanyika Hospitali ya Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar.
  Baadhi ya waalikwa na wagonjwa wa akili waliohudhuria madhimisho ya siku ya Afya ya akili Duniani wakimsikiliza mgeni rasmin Dkt. Muhammed Dahoma (hayupo pichani) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
  Kaimu mratibu Afya ya akili Zanzibar Mohamed Joel Mihambo aitoa neno la shukari baada ya hotuba iliyotolewa na Dkt. Dahoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

  ……………

  Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar


  Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili amesema janga la madawa ya kulevya linalowakabili vijana wengi nchini linapoteza nguvu kazi katika kujenga na kusukuma mbele maendeleo.

  Dkt. Juma ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani yalyofanyika kitaifa Hospitali ya wagonjwa wa maradhi hayo Kidongo chekundu katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa huduma za Hospitali Dkt. Mohd Dahoma.

  Amesema pamoja na kuwepo sababu nyengine za kupata matatizo ya akili kama vile urithi, matatizo ya kijamii, majanga ya kimaumbile mafuriko na maradhi bado madawa ya kulevya yanaongoza kwa kuathiri vijana wengi.

  Katibu Mkuu amesema takwimu za wagonjwa wa akili waliosajiliwa na kupewa huduma za afya ya akili katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2006 Zanzibar ni 139,547 ambapo wagonjwa 9239 walilazwa.

  Ameongeza kuwa pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na waingizaji na watumiaji wa dawa za kulevya bado dawa hizo zinaendelea kuingizwa nchini na kutumiwa na vijana wengi.

  Amesema katika kukabiliana na dawa za kulevya, Serikali imeanzisha huduma za masafa ambapo madaktari wanakwenda maskulini kutoa taaluma ya athari ya madawa hayo na kuanzisha utaratibu wa wagonjwa kuishi na jamii.

  Katibu Mkuu amewashukuru wananchi wanaojitokeza kusaidia juhudi za serikali za kuhudumia wagonjwa wa akili kwa kuwapatia msaada wa chakula na dawa.

  Hata hivyo ameeleza kuwa bado kunachangamoto katika kukabiliana na madawa ya kulevya nchini ikiwemo kutokuwa na chombo kimoja kinachohudumia afya ya akili kama ilivyopendekezwa kwenye sheria ya afya ya akili ya mwaka 2001.

  “Bado kuna Idara tatu za Wizara ya Afya zinazoongoza huduma za afya ya akili, Hospitali ya Mnazimmoja inaongoza Hospitali ya Kidongo chekundu, Programa ya afya ya akili inaongozwa na Idara ya Kinga na madawa ya kulevya na Mental Health Pemba inaongozwa na Idara ya Kinga,”alisema Katibu Mkuu.

  Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo ya mwaka 2001 Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo chekundu inatakiwa ijitegemee na kuwajibika kwa matibabu ya afya ya akili yenyewe.

  Aidha ameeleza tatizo jengine ni kutoshirikishwa watu wa afya ya akili katika kutunga sheria na kwamba kunamgongano wa sheria ya afya ya akili ya mwaka 2001 na sheria ya Hospitali ya Mnazimmoja ya mwaka 2004 na ile ya 2016.

  Katika risala ya wafanyakazi wa Hospitali ya wagonjwa wa akili iliyosomwa na Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Ruzuna Abdulrahim Muhammed wamesema wanakabiliwa na upungufu wa dawa wafanyakazi kwa baadhi ya sehemu.

  IMETOLEWA NA MAELEZO/ZANZIBAR
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA AFYA YA AKILI DUNIANI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top