Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa maelekezo ya kuboresha usafi
wa mazingira ya hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakati alipoitembelea
hospitali hiyo Oktoba 1, 2016. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuboresha upatikanaji wa huduma
katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa kuhakikisha inakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.
Ametoa agizo hilo jana
(Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea hospitali hiyo akiwa kwenye
ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema wakati
Serikali ikishirikiana na uongozi wa mkoa huo katika kumaliza changamoto
zinazoikabili hospitali hiyo manispaa nazo zinajukumu la kuboresha utoaji wa
huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya.
“Waziri Afya atawajibika
kuimarisha hospitali ya mkoa na Manispaa waimarishe huduma katika zahanati zote na
vituo vya afya ndani ya mkoa kwa kuziwezesha kuwa na majengo ya kutosha,
kuongeza idadi ya watumishi na kuhakikisha zinakuwa na dawa na vifaa tiba,”
alisema.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka
watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na isitokee
watu wakakosa dawa au vipimo kwa sababu mmoja wao amechukua na kupeleka kwenye
duka lake binafsi.
Pia Waziri Mkuu alimuagiza
Mganga Mkuu wa Mkoa Dk.
James Kiologwe kutafuta vijana watakaoweza kusafisha na kutengeneza bustani ya
maua kwenye eneo lililoko karibu na uzio wa hospitali hiyo ili liwe na mandhari
ya kuvutia.
Awali
Mganga Mkuu wa mkoa, Dk. James Kiologwe aliiomba Serikali kupandisha hadhi
hospitali hiyo na kuwa ya kanda kwa sababu mbali ya mkoa wa Dodoma, hospitali
hiyo inahudumia wagonjwa wengine kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida na
Manyara.
Akizungumzia
upatikanaji wa tiba wakati Serikali imeanza kuhamia Dodoma, Dk. Kiologwe
alisema mkoa huo unaweza kukabiliana na ongezeko la watumishi kwa una hospitali
tano ambazo zina madaktari bingwa wa fani mbalimbali.
“Tunazo
hospitali tano ambazo ni Benjamin Mkapa, Mirembe, DCMC, St. Gemma na hii ya ya
Rufaa ya Mkoa zenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, huduma kwa mama na mtoto,
magonjwa ya moyo, mishipa, figo na saratani na huduma za mionzi,” alisema.
Katika
hatua nyingine Dk. Kiologwe alisema hospitali hiyo imedumia wagonjwa wa nje
158,375 walipatiwa huduma katika hospitali hiyo katika kipindi cha Julai 2015
hadi Juni 2016 ambapo ni sawa na wastani wa wagonjwa 13,198 kwa mwezi.
“Magonjwa
yanayoongoza kwa wagonjwa wa nje ni mivunjiko, shinikizo la damu, kisukari,
homa ya mapafu na upungufu wa damu,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, OKTOBA 02, 2016
0 comments:
Post a Comment