728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, October 5, 2016

  WAZIRI MKUU AHOJI SABABU ZA MAGEREZA KUTENGEZA MADAWATI KWA WATU BINAFSI

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Maofisa na Askari Magereza wa Gereza Kuu la Mkoa wa Dodoma la Isanga baada ya kulitembelea Oktoba  5, 2016. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Taifa wa Parole Augusine Mrema, kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma na aliyekaa kushoto ni Mkuu wa Magereza wa mkoa wa Dodoma, SACP Kirumbi.
   
  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi  badala ya karakana ya Magereza kama  ilivyokusudiwa na Serikali.

  Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawa moja limegharimu sh. 70,000.

  Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 5, 2016) wakati alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.

  Amesema kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.

  “Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali,” amesisitiza.

  Serikali imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija aliongeza

  Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi amesema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.

  Aidha, Waziri Mkuu amemtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.

  Kuhusu changamoto ya makazi kwa askari Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na imeweka mkakati wa wa ujenzi na kwa upande wa askari Magereza wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.

  Wakati huo huo Waziri Mkuu ametembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo katika maeneo ya soko la Sabasaba na Majengo.

   IMETOLEWA NA:
  OFISI YA WAZIRI MKUU
  S. L. P. 980,
  DODOMA.
  JUMATANO, OKTOBA 05, 2016
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: WAZIRI MKUU AHOJI SABABU ZA MAGEREZA KUTENGEZA MADAWATI KWA WATU BINAFSI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top